WACHEZAJI
wanaotokea kulipwa fedha nyingi zaidi katika ligi mbalimbali duniani ni viungo,
mawinga na washambuliaji.
Hata kwenye ada
za uhamisho huwa hao ndio wanalipiwa zaidi tofauti na mabeki na magolikipa.
Hata hivyo, hiyo haiondoi umuhimu wa mabeki, wawe wa pembeni au wa kati, kwani
ndizo nguzo muhimu za timu na msingi imara wao.
Hebu tuangalie
mabeki waliokuwa bora zaidi katika Ligi Kuu ya England (EPL), tukizingatia
wastani wa mechi walizocheza na jinsi walivyosaidia timu zao kuondoka na ‘clean
sheet’, yaani kutofungwa bao lolote katika mechi. Hawa tunaowakagua leo ni
kwamba wamecheza zaidi ya mechi 100 EPL.
1.
Richardo Carvalho
Huyu alichezea
Chelsea mechi 135 na katika michezo hiyo, asilimia 48.9 hawakufungwa hata bao
moja, hivyo kwamba kwa karibu kila mechi mbili alizopiga, basi moja wapinzani
hawakufurukuta kufunga bao.
2. Tony
Adams
Mlinzi huyu
alipiga mechi 255 akiwa na Arsenal na asilimia ya mechi ambazo hawakufungwa ni
45.1. tunazungumzia mechi 115 pasipo kufungwa bao kwenye EPL na ndiyo tafsiri
hasa ya mtu huyu. Je, Arsenal watakaa wapate beki wa kati mzuri kama huyu? Ni
kusubiri tu. Ni majuzi mchezaji huyu alitoka kumshambulia Wenger kwamba
amembania asiwe kwenye benchi la ufundi hapo Arsenal zaidi ya mara nne kwa madai
eti anamuogopa kutokana na umaarufu wake. Lakini ni huyu huyu amepewa Granada
wa Hispania, wakashika mkia La Liga na sasa wameshuka daraja.
3.
Nemanja Vidic
Amecheza mechi
211 na asilimia 45 yake hakuruhusu bao, akiwa kwenye ulinzi wa kati, imara sana
pale akishirikiana na wengine kama Rio Ferdinand. Alikuja kuzongwa na majeraha
kabla ya nahodha huyu wa Manchester United kuamua kuhamia Internazionale kabla
ya kustaafu mapema 2016. Alikuwa mgumu wa kweli EPL.
4. John Terry
John Terry ndio
kwanza ameachia ngazi Chelsea, baada ya kuwa amekamilisha mechi nyingi kwenye
klabu aliyokuwa nahodha pia. Walikubaliana na uongozi kwamba kiangazi cha mwaka
huu ni wakati mwafaka kwake kuondoka. Ni mmoja wa walinzi na viongozi wazuri
waliopata kutokea EPL, achilia mbali utovu wa nidhamu ndani na nje ya
uwanja.
5. Daniel
Agger
Akicheza na
Liverpool, Agger alipiga mechi 175, kati ya hizo asilimia 41.7 bao halikutinga
kwenye goli lao. Kwa kiasi kikubwa hakuwa akichukuliwa kuwa mchezaji mkubwa,
lakini takwimu haziongopi na zinaonesha kwamba yupo juu. Ameshahama kwa
sasa.
6. Steve
Bruce
Huyu alicheza
sana kabla ya kuja kuwa kocha wa Hull na aliachia ngazi huko mwaka jana hivi
baada ya wamiliki wa klabu hiyo ya EPL kukataa kumpa fedha za kununua
wachezaji. Matokeo yake timu imeshushwa daraja sasa. Enzi zake alikipiga katika
timu tofauti nchini England, akacheza mechi 148 EPL na asilimia 41.2 mambo
yalikuwa mazuri kwani hakuachia bao. Alikuwa akifunga pia mabao muhimu na
mazuri kwa timu yake.
7. David May
Huyu alicheza
mechi 158 na usafi wa lango lake aliuhimili kwa asilimia 39.9 akiwa na timu za
Manchester United na Blackburn Rovers. Hakudumu sana lakini alikuwa na ufanisi
wa kutosha.
8. Gary
Pallister
Alicheza mechi
261 na asilimia ya kutofungwa bao ilisimama katika asilimia 39.8. Yumo katika
orodha ndefu ya wachezaji wanaoitwa mashujaa wa Manchester United. Beki huyu wa
kati alifanikiwa kutwaa ubingwa wa England misimu minne kati ya sita aliyokuwa
na klabu hiyo kongwe.
9. Paulo
Ferreira
Huyu ni beki wa
pembeni wa Chelsea aliyewachezea mechi 141 na kuwa na 39.7% ya kutoruhusu mabao
kwenye mechi zote hizo. Amekuwa hapati sifa anazostahili, hata hivyo, lakini
ukweli ni kwamba ametwaa mataji 13 katika miaka yake tisa aliyokaa
England.
10. Sami
Hyypia
Wengi watakuwa
wanamkumbuka mlinzi huyu mrefu na aliyetumia vyema umbo lake akiwa kiongozi wa
Liverpool kwa muda mrefu. Alicheza mechi 318 na akazuia mabao kwa asilimia 38.4
ya mechi zote hizo. Alikuwa moyo wa ukuta wa The Reds.
11. Jamie
Carragher
Mtu huyu ambaye
kwa sasa ni mchambuzi yakinifu wa mechi, amecheza mechi nyingi – 508 katika
miaka 17 aliyokaa Liverpool na asilimia yake ya uokozi ni 38.4. Anastahili sifa
kwa muda mrefu aliokaa hapo na kutoka katika mechi 195 bila lango lake
kutikiswa na mpira. Ndiye anaongoza kwa mechi nyingi kiasi hicho.
12. Per
Mertesacker
Mjerumani huyu
mrefu na nahodha wa Arsenal amekuwa pia kwenye Timu ya Taifa ya Ujerumani. Bado
anadunda na ni tegemeo kwa Arsenal akiwa mzima, lakini msimu wote huu amekuwa
nje ya dimba kutokana na kuumia wakati wa maandalizi ya msimu.
Ni mtu mwenye
nidhamu ndani na nje ya uwanja ambapo kabla ya unahodha alikuwa mkuu wa nidhamu
chini ya Arsene Wenger, akikusanya faini kwa wachezaji waliofanya makosa yoyote
ndani na nje ya dimba, ikiwa ni pamoja na kuchelewa kazini.
13. Ashley
Cole
Ashley Cole
amepata kutajwa kuwa mmoja wa mabeki wazurti zaidi wa kushoto, akiwa amecheza
mechi 385 na akazuia mabao katika mechi asilimia 38.2. amezigawanywa kwa
Arsenal na baadaye Chelsea, pamoja na utata unaoyazunguka maisha yake ndani na
nje ya dimba.
14.
William Gallas
Huyu alikuwa
kiongozi hapo Arsenal, akicheza mechi 321 lakini pia akizigawa kwa kuwa Chelsea
na Tottenham Hotspur na kuwa na asilimia 38 ya kutoruhusu mabao. Alikuwa akivaa
namba 10, alijiamini na kupata mafanikio mchanganyiko.
15.
Laurent Koscielny
Mfaransa
mwingine huyu aliyecheza mechi nyingi akiwa na Arsenal. Beki wa kati wa
kimataifa wa Ufaransa ambaye amekaimu unahodha Arsenal muda mwingi. Wapo
wachache wanaohoji uimara wake lakini ni mmoja wa mabeki wazuri wa kati na hata
alitakiwa na Barcelona.
16. Rio
Ferdinand
Huyu ni beki
mrefu wa kati aliyecheza mechi 504 na katika hizo alifanikiwa kwa asilimia 37.5
kwenda bila kufungwa bao. Kwa muda wote amekuwa tegemeo kwa klabu alizokuwa –
Manchester United lakini pia kabla ya hapo Leeds na West Ham, akaja kumaliza
bila mafanikio na Queen Park Rangers (QPR) akashuka nao daraja, akasema na
kustaafu.
17.
Denis Irwin
Huyu ni mtu
aliyekuwa na mechi 308 na asilimia ya mafanikio bila bao kufungwa langoni mwake
ni 37.5. huyu ndiye mchezaji pekee ambaye kocha mahiri Alex Ferguson alisema
kwamba hapana wasiwasi angemweka wkenye kikosi chake cha ‘Best 11’ cha wakati
wote, akisema alikuwa akifanya kosa moja tu katika kipindi cha miaka 10.
18. Lee Dixon
Dixon alicheza
mechi 305 na katika hizo hakuruhusu bao kwenye asilimia 37.4 yake. Alikuwa
mchezaji aliyepewa nafasi mara nyingi katika ukocha wa Arsene Wenger hapo
Arsenal, katika kipindi kile cha mwanzo cha mafanikio makubwa.
19. Gary Neville
Huyu ni mlinzi
aliyepata mafanikio makubwa Old Trafford, akicheza mechi 400 na kufanikisha
‘clean sheet’ kwa kiwango cha 37%. Siku hizi mafanikio hayo yanasahaulika
kutokana na jinsi alivyofanya vibaya kama kocha.
20. Vincent
Kompany
Huyu ni nahodha
wa Manchester City ambaye hana uhakika wa kuwapo kikosini msimu ujao chini ya
Pep Guardiola msimu ujao. Company, Mbelgiji na beki wa kati mwenye nguvu
alikuwa akileta tofauti kubwa sana kwa Man City akiwapo na kutokuwapo; majeraha
yanamsonga na kwa hakika atakuwa akielekea mwisho wa soka ya ushindani katika
ngazi ya juu kwenye klabu kubwa England.
No comments:
Post a Comment