SERIKALI ya
Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na ile ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zimepongeza
hatua ya Chama cha Soka cha Zanzibar (ZFA) kupata uanachama wa kudumu katika
Shirikisho la Soka Afrika (CAF)
Akizungumza na
wandishi wa habari jana, Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Rashid Ali Juma alisema anashukuru ushirikiano
wa Serikali ya Muungano wa Tanzania kupitia kwa Waziri Nape kwa kusimamia na kuhakikisha ZFA Inapata uanchama CAF.
“Nashukuru
Zanzibar kukubalika na kupata mwanacham kamili wa CAF majira ya saa 6.45 mchana
kwani umefika wakati sasa kuona bendera ya Zanzibar, wimbo wa Taifa wa Zanzibar
ukipigwa wakati wa mashindano ya kimataifa,” alisema Juma.
Aidha Juma
alisema Wanzazibar wanatakiwa kutekeleza kwa vitendo kile ambacho walikuwa
wanalilia kuonesha vipaji ambavyo walikuwa wanasema hawapati nafasi ya kutosha
na kuahidi ushirikiano kwa ZFA kupata katiba nzuri kuendana na matakwa ya
CECAFA na CAF ili iwe njia rahisi ya kupata uanachama wa FIFA.
Naye
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo wa
Wizara Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Yusuph Singo,
alipongeza juhudi za Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) kuhakikisha Zanzibar
imepata uanachama wa CAF kwani haikuwa kazi rahisi na kuahidi ushirikiano zaidi
kwa TFF na ZFA.
“Zanzibar
kupata uanachama wa CAF ni hatua mojawapo ya kuanza kuomba pia kuwa mwanachama
wa FIFA hivyo nawahakikishia ushirikiano kuhakikisha tunapiga hodi Zurich
kuomba uanachama,” alisema Dkt. Singo.
Aidha Dkt Singo
alisema moja ya sifa ya kuwa mwanachama wa FIFA lazima uwe mwanachama wa
shirikisho la Soka katika bara unalotoka, kwa sasa Zanzibar ina sifa ya kuwa
mwanachama wa fifa na utaratibu wa
kuomba unataanza mara moja.
Naye Rais wa
Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) Jamal Malinzi alisema furaha ya kuona
Zanzibar akiwa mwanachama hawezi kuieleza kwani ni jambo ambalo lilikuwa
linamhuzinisha kuona wanakataliwa uanachama.
“Leo
tunasheherekea Zanzibar kuwa mwanachama furaha ambayo siwezi kuilezea lakini
tulipambana na hatimaye tumefanikiwa na kuhusu wachezaji wanaotoka Zanzibar ni
swala la kikanuni ambalo tutalifanyia kazi watanzania wasubiri wakati kanuni
zikiandaliwa,” alisema Malinzi
Kwa upande
wa mjumbe wa heshima wa Shirikisho la Soka Barani Afrika, Said Elmaamry alisema
ana furaha baada ya Zanzibar kupata uanchama kwani ni kazi ambayo wameipigania
kwa kipindi kirefu ingekuwa watu wengine wangekuwa wamekata tamaa.
“Tusahau
yaliyopita kwani kuna mataifa ambayo yalikuwa hayataki Zanzibar ipate wanachama
wakihofia kuwa sisi ni ndugu tutaachiana kwenye mashindano ya kimataifa lakini
Bara tunatakiwa tujue tunapocheza na Zanzibar ni timu mbili tofauti wasishangae
wakiona Zanzibar wanaonesha ushindani,” alisema Elmaamry
Zanzibar
imekuwa nchi ya 55 kupata uanachama juzi kwenye Mkutano Mkuu wa Caf uliofanyika
Ethiopia ambapo Hamad Hamad wa Chama cha Soka cha Madagascar alichaguliwa kuwa Rais na kumwangusha Issa Hayatou aliyedumu
tangu 1988.
No comments:
Post a Comment