LIGI ya Vijana ya Shirikisho la Miguu Tanzania (TFF)
wenye umri wa chini ya miaka 20, inatarajiwa kuanza Novemba 15, 2016 mwaka huu
kwa kushirikisha timu za vijana U-20 wa timu za ligi kuu.
Uzinduzi utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba
mkoani Kagera kwa timu za vijana za Kagera Sugar na Yanga kuchuana siku hiyo.
Akizungumza na wandishi wa habari, Ofisa Habari
wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Alfred Lucas alisema timu zimepangwa
kwenye makundi mawili yenye timu nane kila moja.
"Kagera na Yanga zimepangwa kundi A na zitaanza
mchezo saa 10.30 jioni ikiwa ni baada ya shamrashamra za uzinduzi wake kwani
kulingana na ratiba iliyotolewa na bodi ya Ligi siku hiyo kutakuwepo na mechi
moja lakini kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Bodi ya Ligi ya TFF kwa siku
kutakuwa na michezo miwili kwa tofauti ya saa", alisema Lucas
Timu nyingine ambazo zipo kundi A ni Stand United na
Mwadui za Shinyanga ambazo zitacheza Novemba 16, 2017 na Novemba 17, Azam itacheza
na Mbao FC saa 8.00 mchana kabla kuzipisha Toto Africans na African Lyon saa
10.30 jioni.
Kundi B kituo chake kitakuwa Dar es Salaam, Simba
itafungua dimba na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Uhuru - mchezo utakaonza saa 8.00
kabla ya kuzipisha timu za JKT Ruvu na Ruvu Shooting kucheza saa 10.30 jioni siku
hiyo hiyo.
Novemba 17, Tanzania Prisons itacheza na Mbeya City
saa 8.00 mchana wakati Majimaji itacheza na Mtibwa saa 10.30 jioni.
Ligi hiyo ya mkondo mmoja, hatua ya makundi
inatarajiwa kufikia ukomo Desemba 12, 2016 ambako timu nne vinara kutoka katika
kila kundi zitapangiwa ratiba mpya na kituo ili kutafuta bingwa wa msimu kwa
timu za vijana.
Kituo hicho kitatangazwa baada ya kumalizika hatua ya
makundi hapo Desemba 12, mwaka huu.
Ujio wa ligi hiyo ni utekelezaji au kukidhi matakwa ya
maelekeo ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) na Shirikisho la
Mpira wa Miguu Afrika (CAF) katika kategori ya uwepo wa timu za vijana
zinazoshindana mbali ya kupata huduma za shule na matibabu kwa timu zote za
Ligi Kuu na Ligi daraja la Kwanza.
No comments:
Post a Comment