Pages

Saturday, November 5, 2016

KIJEBA CHA CONGO BRAZAVILLE KUCHUNGUZWA NA CAF, HUENDA SERENGETI BOYS......



SHIRIKISHO la mpira wa miguu barani Afrika (CAF) linafanyia uchunguzi tuhuma za timu ya Congo Brazzaville kuchezesha mchezaji aliyezidi umri katika michuano ya vijana U-17.


Congo wamepata nafasi ya kushiriki michuano ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 kwa kuitoa Serengeti Boys katika hatua ya mwisho ya kufuzu fainali hizo zitakazo fanyika nchini  Madagascar mwakani.

Akizungumza na wandishi wa habari, Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas alisema Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania (TFF) liliiandikia CAF barua kulalamikia kuhusu umri wa mchezaji Langa-Lesse Bercy  na kutaka kufanyiwa kipimo cha mifupa (MRI SCAN) kwa ajili ya kubaini umri wake sahihi.

"CAF imeamua kumpeleka Bercy  kufanyiwa vipimo hivyo kwa sababu hata Namibia ambao walitolewa na Congo walipeleka malalamiko kuhusu mchezaji huyo", alisema Lucas
Naye Mkuu wa Kitengo cha Madaktari wa CAF Dk Boubakary Sidiki amethibitisha kupokea barua kutoka TFF kuhusu Bercy  ambaye alifunga bao dhidi ya Namibia na Tanzania pia na kuisaidia Congo kufuzu fainali hizo na sasa atafanyiwa vipimo Novemba,18 jijini Cairo.

Bercy atasafiri kwenda Misri na Daktari wake ambapo  TFF watatakiwa kupeleka madaktari wawili kwa ajili ya kuhakiki majibu ya vipimo hivyo huku pia wakitakiwa kulipia gharama zote za zoezi hilo.

Tayari droo ya michuano hiyo imepangwa ambapo Congo ipo kundi B sambamba na Mali, Angola and Niger.

Timu nne zitakazoingia nusu fainali zitakuwa zimekata tiketi ya moja kwa moja kwenda kushiriki fainali za Dunia zikazofanyika nchini India

No comments:

Post a Comment