Pages

Saturday, November 5, 2016

KOMBE LA SHIRIKISHO KUANZA NOVEMBA 19 TANGA



UZINDUZI wa michuano ya Kombe la FA 2016 zitafanyika Tanga Novemba 19 katika Uwanja wa CCM Mkwakwani kwa mchezo kati ya Muheza United dhidi ya Sifa Politan ya Temeke.

Msimu huu michuano hiyo itashirikisha timu 84 ambapo mabingwa wa mikoa pia watashiriki tofauti na mwaka jana ambapo timu 64 pekee kabla ya Yanga kuibuka Bingwa kwa kuichapa Azam mabao 3-1.

Akizungumza na wandishi wa habari, Ofisa Habari wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) alisema bingwa wa michuano hiyo ataiwakilisha nchi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
"Ligi itazinduliwa Novemba 19 kule Mkwakwani Tanga kati ya Muheza United na Sifa Politan na mwaka huu timu zimeongezeka tofauti na mwaka jana ambapo tunatarajia ushindani mkubwa," alisema Lucas.
Pia Lucas alisema michuano hiyo itaonyeshwa moja kwa moja  (mubashara) na kituo cha Luninga cha Azam TV ambao ndiyo wadhamini wakuu kwa miaka mitano kutokana na mkataba ulioingiwa na TFF.
Lucas alisema matarajio ya Shirikisho  kuona ligi yenye ushindani baada ya timu kuongezeka kulinganisha na mwaka uliopita.   
Mwaka huu kuna timu 16 za Ligi Kuu Tanzania Bara, timu zote 24 za Ligi Daraja la Kwanza (FDL), timu zote 24 za Daraja la Pili (SDL) na timu 22 za mabingwa wa mikoa na yatakuwa ya mtoani na yataendeshwa kwa raundi tisa.
Raundi ya kwanza itashirikisha timu  22 za Mabingwa wa Mikoa katika makundi manne ya timu sita na timu tano ambako timu mbili za juu zitaingia raundi ya pili.
 Raundi ya pili itashirikisha timu nane zilizofuzu za RCL katika raundi ya kwanza na kujumlisha timu 24 za Daraja la Pili (SDL) kufanya jumla ya timu zote kuwa 32 kwa hatua ya pili.
Raundi ya tatu itashirikisha timu 16 zilizofuzu hatua ya pili kushindana ili kupata timu nane zitakazoingia hatua ya nne.
 Raundi ya nne itashirikisha timu zote za Daraja la Kwanza (24) na kumulisha timu nane zilizoshinda raundi ya tatu kufanya timu zote kuwa 32.
Raundi ya tano, itashirikisha timu 16 zilizofuzu Raundi ya nne na kumuisha timu zote 16 zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na kufanya timu zote katika raundi hii kuwa 32.
Raundi ya sita itashirikisha timu zote 16 zilizofuzu katika raundi ya tano na mzunguko huo utaitwa Hatua ya 16 Bora.
 Raundi ya saba itashirikisha timu nane zilizofuzu katika raundi ya sita na mzunguko huo kutambuliwa kuwa Nane Bora au Hatua ya Robo fainali .
Raundi ya nane ambayo itashirikisha timu nne zilizofuzu raundi ya saba (Robo Fainali) na mzunguko huo utatambuliwa kuwa ni nusu fainali.
Raundi ya tisa itashirikisha timu mbili zilizofuzu raundi ya nane na washindi hao wa nusu fainali na kumpata Bingwa wa Azam Sport Federation Cup kwa msimu wa 2016/2017.
Tanzania mwakani kwenye kpmbe la Shirikisho itawakilishwa na timu ya Azam FC baada ya kupoteza kwenye mchezo wa fainali dhidi ya Yanga ambao watacheza ligi ya Mabingwa Afrika.

No comments:

Post a Comment