SERENGETI BOYS KUCHEKA AU KULIA KESHO?
TIMU ya soka ya taifa
ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kesho itakuwa mgeni wa Congo
Brazzaville katika mchezo wa mwisho wa kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa
vijana wa umri huo.
Serengeti Boys itashuka dimbani ikiwa na
kumbukumbu ya kushinda mchezo wa
nyumbani dhidi ya timu hiyo ya Congo mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Hivyo katika mechi ya leo, Serengeti inahitaji
kulinda mabao hayo huku ikiongeza mengine kwani timu itakayoshinda itafuzu
fainali hizo zitakazofanyika Madagascar mwakani.
Katika kuhakikisha inafanya vizuri kwenye mchezo
huo, Serengeti iliweka kambi ya siku sita Kigali, Rwanda kufanya maandalizi ya
utulivu na kuwajenga wachezaji kisaikolojia kwa ajili ya mchezo huo.
Kocha wa Serengeti Boys, Bakari Shime
akizungumzia mchezo huo alisema hautakuwa rahisi kwani Congo ni timu nzuri
yenye vijana wazoefu na mashindano hayo.
“Mchezo utakuwa
mgumu lakini silaha zangu zipo tayari kwa mchezo, naamini tuna uwezo wa
kushinda, kama wao walipata mabao kwetu, hata sisi tukipambana
tutapata,”alisema.
Awali, Serengeti Boys ilivuka raundi hii ya
mwisho baada ya kuzitoa Shelisheli kwa jumla ya mabao 9-0, ikishinda mchezo wa
nyumbani 3-0 na ugenini 6-0.
Pia, iliitoa Afrika Kusini kwa jumla ya mabao
3-1, ikitoka sare ya bao 1-1 ugenini na kushinda nyumbani mabao 2-0.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Nape Nnauye aliahidi timu hiyo Sh milioni moja kwa kila bao litakalofungwa kama
motisha ya kuonesha juhudi na kuvuka hatua nyingine.
Ikifuzu, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Tanzania
kufika hatua hiyo. Iliwahi kufanya hivyo kwa timu ya wakubwa Taifa Stars mwaka
1980 michuano ya Kombe la Mataifa Afrika ilipofanyika Lagos, Nigeria.
Serengeti Boys iliwahi kufuzu michuano
iliyofanyika mwaka 2005 Gambia, lakini iliondolewa baada ya kubainika kumtumia
mchezaji aliyezidi umri.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment