Mabingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, Young Africans na timu nyingine zilizoshiriki katika msimu
ulioisha wa 2015/2016 zitakabidhiwa zawadi zao mapema mwezi ujao na Kampuni ya
mawasiliano ya Vodacom Tanzania ambayo ni mdhamini mkuu wa ligi hiyo.
Meneja Uhusiano wa Vodacom Tanzania, Matina
Nkurlu amesema kuwa ucheleweshaji wa kutoa zawadi hizo baada ya kumalizika, umetokana
na baadhi ya timu zinazoshiriki kwenye mechi za mashindano ya kimataifa kama
vile mashindano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika na kuingia kwa mfungo wa
Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
“Tunaomba radhi kwa timu husika, wachezaji na wadau wa soka kwa
zoezi hili kuchelewa ila tunawahakikishia kuwa
zawadi ziko tayari na zitakabidhiwa
mwezi ujao,” alisema Nkurlu.
Pia alishukuru wadau wote
waliofanikisha ligi hiyo hadi kufikia mwisho ambapo Young Africans ya jijini
Dar es Salaam iliibuka tena bingwa kwa mwaka huu.
“Licha ya changamoto zinazoendeleza
kujitokeza katika ligi yapo mafanikio makubwa na ligi hii inazidi kuwa na
msisimko mkubwa nchini tunawashukuru wadau
wote na tuna imani kuwa itazidi kuwa bora katika siku za usoni,” alisisitiza
Nkurlu.
Alisema kuwa Vodacom Tanzania
itaendelea kutoa udhamini wa ligi hii hata katika msimu ujao kwa mujibu wa
mkataba wake na TFF na aliwataka wadhamini wengine kujitokeza ili kuboresha
zaidi ligi hii ikiwemo kuwawezesha wachezaji kunufaika zaidi katika ushiriki
wake.
No comments:
Post a Comment