TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Mpira wa Miguu 'Twiga Stars', kesho inashuka dimbani kuikabili timu ya Taifa ya Wanawake kutoka Zimbabwe 'Mighty Warriors' katika mchezo wa kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa ya Afrika utakaochezwa katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi nje ya jiji la Dar es salaam.
Twiga Stars ambayo walifanya mazoezi ya mwisho leo asubuhi walionekana kuwa na ari licha ya mvua za rasharasha zilizokuwa zinanyesha.
Akizungumza na wandishi wa habari, Kocha Mkuu wa Twiga Stars, Nasra Juma alisema vijana wake wote wapo katika hali nzuri kuikabili Zimbabwe.
"Nawaheshimu Zimbabwe wana timu nzuri, ndani ya miaka minne tumecheza nao zaidi ya mara nne, mapungufu yaliyojitokeza katika michezo iliyopita nimefanyia kazi na hivyo kesho (leo) nina imani tutafanya vizuri, " alisema Nasra.
Pia kocha Nasra, amewaomba watanzania kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa Azam Complex Chamazi kuwapa sapoti Twiga Stars katika mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Naye nahodha Sophia Mwasikili, amesema wachezaji wote wapo katika hali nzuri, wana ana ari na morali ya hali ya juu na kuwaomba watanzania kujitokeza kwa wingi kuja kuwashangilia uwanjani watakapokuwa wakipeperusha bendera ya Tanzania.
Wapinzani wa Twiga Stars, timu ya taifa ya Zimbabwe waliwasili jana jioni, waamuzi wa mchezo huo kutoka nchini Ethiopia na kamishina wa nchezo huo waliwasili jana.
No comments:
Post a Comment