Abdi Banda akitoka Uwanjani baada ya kupewa kadi nyekundu |
YANGA leo
imeendeleza umwamba kwa Simba katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu baada ya
kuinyuka kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika
mchezo wa duru la kwanza baina ya timu hizo kwenye uwanja huohuo Septemba mwaka
jana, Yanga ilishinda kwa idadi kama hiyo ya mabao.
Bao moja
katika kila kipindi kama ilivyokuwa mchezo wa Septemba yalitosha kuwapa furaha
mashabiki wa Yanga na kuanza kuimba nyimbo za furaha kuwasifu wachezaji wao.
“Nyama ya
Simba halali kwa Yanga… Yanga… nani kaua? Tambwe…Tambwe,” vilikuwa baadhi ya
vibwagizo vya mashabiki wa Yanga katika
mchezo huo wa jana.
Yanga
ilianza kuhesabu bao dakika ya 37 mfungaji akiwa Donald Ngoma baada ya beki
Hassan Ramadhan ‘Kessy kurudisha mpira mfupi kwa kipa wake Vincent Angban na
Ngoma kuuwahi na kupachika bao.
Simba
iliyoanza mchezo wa jana kwa kasi kubwa na kuwapa matumaini mashabiki wake,
ilijikuta muda mrefu ikicheza pungufu baada ya beki wake Abdi Banda kuoneshwa
kadi ya pili ya njano iliyofuatiwa na nyekundu baada ya kumchezea madhambi
Ngoma dakika ya 23.
Awali dakika
ya 20 mwamuzi Jonensia Rukyaa wa Kagera alimpa kadi ya njano Banda baada ya
kumchezea vibaya Ngoma, lakini dakika chache baadaye beki huyo alirudia tena
kufanya madhambi na kupewa adhabu hiyo.
Dakika 15 za
kwanza timu hizo zilishambuliana kwa zamu, huku Simba ikifika mara nyingi
golini ikiwa ni pamoja na kupata kona za mara kwa mara, lakini umaliziaji
ulikuwa butu.
Simba
ilipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 16 wakati shuti la Jonas Mkude
lilipookolewa na beki Mbuyu Twite wakati mpira ulipokuwa ukielekea langoni huku
mashabiki wa Simba wakiwa tayari wameamka katika viti kushangilia.
Mshambuliaji
wa zamani wa Yanga, Amis Tambwe jana aliingia katika rekodi nyingine ya
wachezaji waliopata kucheza Simba na Yanga na kufunga mabao katika kila timu
aliyocheza.
Tambwe
aliifungia Yanga bao la pili dakika ya 73 kutokana na pasi ya Godfrey
Mwashiuya, bao ambalo lilifanya mashabiki wa Simba kuanza kutoka uwanjani.
Hata hivyo
bado Kiiza anaongoza katika ufungaji akiwa na mabao 16 akifuatiwa na Tambwe
mwenye mabao 15 na Ngoma mwenye mabao 11.
Yanga
ingeweza kuongeza idadi ya mabao, lakini washamuliaji wake wakiongozwa na
Tambwe, Ngoma na Msuva walishika na papara za miguu kila walipokaribia lango la
Simba.
Licha ya
Simba kufungwa mabao hayo ilionekana kuzindunduka dakika za mwisho na kufanya
mashambulizi ya kushtukiza, lakini bado suala la kutumbukiza mipira nyavuni
lilikuwa tatizo.
Kutokana na
matokeo hayo Yanga imefikisha pointi 46 na kushika uongozi wa ligi hiyo
ikiiacha Simba ikiporomoka hadi nafasi ya tatu ikiwa na pointi 45, baada ya
jana Azam kuifunga Mbeya City mabao 3-0. Yanga ipo nyuma ya Simba kwa mchezo
mmoja.
Kipigo hicho
ni cha kwanza kwa Simba tangu iwe chini ya kocha Jackson Mayanja aliyerithi
mikoba ya Dylan Kerr aliyetimuliwa mwezi uliopita.
Mayanja
ameiongoza Simba kushinda mechi sita mfululizo za Ligi Kuu Tanzania Bara,
ambapo jana ilikuwa mara yake ya kwanza kucheza na Yanga akiwa kocha wa Simba.
Yanga: Ally
Mustafa ‘Barthez’ Juma Abdul, Vincent Bossou, Mbuyu Twite, Mwinyi Hajji
Mngwali, Pato Ngonyani, Deus Kaseke/Godfrey Mwashiuya, Thabani Kamusoko, Amissi
Tambwe Donald Ngoma na Haruna Niyonzima/Simon Msuva.
Simba:
Vicent Angban, Hassan Kessy, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Juuko Murshid, Abdi
Banda, Justice Majabvi, Jonas Mkude, Mwinyi Kazimoto/Novaty Lufunga, Hamisi
Kiiza/Danny Lyanga, Ibrahim Ajib/Brian Majwega na Said Ndemla,
Naye
Mwandishi Alexander Sanga anaripoti kuwa
timu ya JKT Ruvu na Stand United ya Shinyanga jana zilifungana bao 1-1 katika
mchezo wa ligi hiyo Uwanja wa Kambarage.
Stand
ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya saba mfungaji akiwa Elias Maguli kwa
shuti la mbali lililomshinda kipa Shaaban Dihile.
JKT Ruvu
inayoshika mkia katika msimamo wa ligi ilisawazisha dakika ya 13 mfungaji akiwa
Abdulrahman Mussa baada ya makosa ya kipa wa Stand Frank Muwonge.
Nayo Toto
Africans na Kagera Sugar zilitoka sare ya bao 1-1 Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza,
ambapo Toto Africans ilitangulia kufunga bao dakika ya 24 mfungaji akiwa
Japhary Vedastus.
Mfungaji
alimalizia kazi nzuri ya Miraji Athumani
kabla ya Kagera kusawazisha dakika ya 66 mfungaji akiwa Mbaraka Yusuph.
Nayo Azam FC
ambayo ilifungwa mchezo wake uliopita, ilizinduka jana Uwanja wa Sokoine Mbeya
baada ya kuifunga Mbeya City mabao 3-0 na hivyo kufikisha pointi 45 na kuchupa
hadi nafasi ya pili ikitoka ya tatu.
Cio…
No comments:
Post a Comment