Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Alhamisi ya Januari 14 lilitoa taarifa kuwa limevifungia klabu za Real Mdarid na Atletico Madrid kutokufanya usajili wowote mpaka msimu wa 2017 na sababu ya kusajili wachezaji wenye umri chini ya miaka 18 bila kufuata kanuni.
Aidha pamoja na adhabu hiyo pia walipigwa faini na FIFA, Real Madrid ikitakiwa kulipa pesa ya Uswisi, Francs 360,000 sawa na Pauni 250,000 na Atletico Madrid ikipigwa faini ya Francs, 900,000 sawa na Pauni 620,000.
Baada ya FIFA kutoa taarifa hiyo, Real Madrid kupitia kwa Mkurugenzi Mtendaji wa klabu hiyo, Jose Angel Sanchez ilisema kuwa adhabu hiyo siyo sahihi na wanaamini wakienda mahakamani watashinda.
Sanchez ambaye aliongozana na Mkuu wa kitengo cha sheria wa Madrid, Javier Lopez Farre katika mkutano na waandishi wa habari, alinukuliwa na gazeti la Marca kuwa adhabu waliyopewa na FIFA siyo ya kuitarajia na haina ushahidi.
“Siyo sahihi kwamba tulisajili wachezaji U-18 bila kuwasajili RFEF (Chama cha Soka cha Hispania) na hiyo ndiyo sababu kuwa hatujafuata kanuni,
“Klabu hii inafuata sheria na watu ambao wanafanya kazi hapa hawajawahi kuvunja sheria hizo, hoja ambayo wameitoa FIFA ina makosa”,  alisema Sanchez.
Aidha baada ya kutoa taarifa hiyo, Real Madrid wamepanga kwenda kukata rufaa kwenye mahakama sehemu ambayo wanaamini watapata haki yao.