RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amefunga kozi ya waamuzi chipukizi wasiokuwa na beji za FIFA barani Afrika.
Kozi hiyo ambayo ilikuwa inafanyika hapa nchini, kuanzia Septemba 23 ambapo jumla ya waamuzi 30 kutoka nchi 28 barani Afrika walihudhuria na kufundishwa na wakufunzi sita kutoka CAF na FIFA.
Akiongea wakati wa kufunga kozi hiyo Malinzi alitoa wito kwa wahitimu kujikita kwenye maadili kwa kuzingatia mafunzo waliyopata ili katika kipindi kifupi wote wapate beji za FIFA na waonekane kweye mashindano makubwa kama fainali za AFCON na mashindano ya Kombe la Dunia.
“Kozi hii iwe chachu kwenu kuzingatia maadili ili katika kipindi kifupi muweze kupata beji za FIFA na mchezeshe fainali za Afrika na kombe la Dunia”, alisema Malinzi
Awali akizungumza, mwakilishi wa CAF, Eddy aliishukuru TFF kwa maandalizi mazuri na usimamizi bora kwa kipindi chote cha kozi, na kuahidi kuleta kozi nyingine kubwa hapa nchini.
Naye mwakilishi wa FIFA, Carlos Hendrique alitoa shukurani zake za dhati kwa TFF kwa kuwa tayari wakati wote kushirikiana na FIFA hali ambayo imefanyika TFF iaminike na itegemewe na FIFA kweye program mbalimbali
Kozi hiyo ya waamuzi imefanyika kwa mara ya kwanza hapa barani Afrika na FIFA iliiteua Tanzania kuwa mwenyeji wa kozi hii kwa nchi zinazozungumza kiingereza.
No comments:
Post a Comment