Pages

Saturday, August 22, 2015

YONDANI AIPASHA YANGA YATWAA NGAO YA JAMII




YANGA leo imeanza vizuri msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara wa mwaka 2015/16 baada ya kuwafunga Azam FC kwa penalti 7-6 katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa.

Mbali na Yanga kulipa kisasi cha kufungwa na Azam kwa penalti 5-4 katika robo fainali ya Kombe la Kagame hivi karibuni, ushindi huo pia umeendeleza uteja kwa Azam baada ya kuendelea kufungwa katika mechi za Ngao ya Jamii.

Yanga iliifunga Azam FC 1-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii mwaka 2013 kabla ya kushinda tena 3-0 mwaka jana na kuibuka na ushindi wa penalti 7-6 mwaka huu na kuwa washindi wa kihistoria katika Ngao ya Jamii baada ya kushinda mara tano.

Katika mchezo huu penalti za Yanga zilifungwa na Haruna Niyonzima, Deus Kaseke, Amiss Tambwe, Andrey Coutinho, Godfrey Mwashiuya, Thabani Kamusoko na Mbuyu Twite, huku nahodha wao Nadir Haroub alikosa penalti ya kwanza.

Kwa upande wa Azam waliofunga ni pamoja na Kipre Tchetche, John Bocco, Himid Mao, Agrey Morris, Jean Mugiraneza, Erasto Nyoni na Shomar Kapombe wakati waliokosa ni Pascal Wawa na Ame Ali.

Mchezo huo ulianza kwa kasi kwa Yanga kulishambulia lango la wapinzani wao na katika dakika ya pili nusura wafunge baada ya Amissi Tambwe kukosa bao licha ya kuwa katika nafasi nzuri.

Azam FC walijibu mapigo katika dakika ya sita wakati John Bocco baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga na kupiga shuti kali lililodakwa na kipa Mustapha.

Katika dakika ya 15 Said Juma alioneshwa kadi ya njano baada ya kumchezea rafu Farid Mussa.

Dakika ya 19 Yanga walikosa bao kupitia kwa mchezaji wake iliyomsajili kutoka Kimondo ya Mbeya, Geofrey Mwashiuya pamoja na kuwa yeye na kipa wa Azam FC, Aishi Manula.

Erasto Nyoni alioneshwa kadi ya njano baada ya kumchezea vibaya simon Msuva katika dakika ya 47.

Baada ya kosakosa za hapa na pale na Yanga kuonekana kutawala kipindi cha pili, timu hizo zilipigiana penalti.

Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2015/16 unatarajia kuanza Septemba 12 kwa mechi za ufunguzi kwenye viwanja tofauti.

Vikosi Yanga: Ally Mustapha, Mbuyu Twite, Hajji Ngwai, Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Said Juma/Haruna Niyonzima, Simon Msuva/Andrey Coutinho, Thabani Kamusoko, Amiss Tambwe, Donald Ngoma/Deus Kaseke na Geofrey Mwashiuya.

Azam FC: Aishi Manula, Shomar Kapombe, Erasto Nyoni, Aggrey Morris, Pascal Wawa, Farid Mussa, Frank Domayo/Amme Ali, Himid Mao, John Bocco, Kipre Tchetche na Mudathir Yahya/Jean Mugiraneza.

No comments:

Post a Comment