Pages

Saturday, August 22, 2015

NIANG AANZA MAZOEZI SIMBA LEO





KOCHA wa viungo wa Simba, Dusan Momcilovic amesema mshambuliaji raia wa Senegal, Papa Niang bado hayuko fiti, hivyo anahitaji muda zaidi wa kufanya mazoezi.

Akizungumza baada ya mazoezi yaliyofanyika kwenye uwanja wa Boko Veterani Dusan alisema anatarajia baada ya wiki tatu hadi tano anaweza kuzungumza uwezo wa mchezaji huyo.

“Papa ameanza mazoezi leo nimeona fitness yake ni ya kawaida, hivyo nahitaji muda zaidi afanye mazoezi niweze kupima uwezo wake na tutakapokuwa Zanzibar nitakuwa na muda zaidi wa kumfuatilia kwa karibu kwani anahitaji mazoezi ya peke yake”, alisema Dusan.

Dusan ambaye ni raia wa Serbia alisema wachezaji wa Simba uwezo wao upo vizuri na watakapoanza ligi anatarajia watafanya vizuri.

Papa Niang aliwasili jijini Dar es Salaam juzi kwa ajili ya kuanza majaribio yake ya kujiunga na klabu ya Simba.

Endapo Niang ataonesha kiwango cha kumvutia kocha mkuu, Dylan Kerr pamoja na benchi zima la ufundi, huenda akapewa mkataba wa kuitumikia klabu hiyo ambayo imekuwa ikihaha kutafuta washambuliaji wa kigeni.

Niang aliyezaliwa Desemba 5, 1988 katika mji wa Matam Senegal ana urefu wa mita 1.81.

Endapo Niang atafanikiwa kusajiliwa Simba basi atasajiliwa kama mchezaji huru kwani mkataba wake na Mounana CF ya Gabona ambayo ilimsajili 2014-2015 ulishamalizika.

Pia aliwahi kuchezea timu za  Al Shabab SC ya Kuwait, FC Vostok ya Kazakhstan, FF Jaro, AC Oulu na FC OPA za Finland.

Niang ambaye ni mdogo wa damu wa Mamadou Niang ambaye kwa sasa anamalizia soka yake FF Jaro baada ya kuwika Ulaya na Asia alisema anafurahi kuja Tanzania na amefurahia mazingira japo kuna tofauti kidogo.

No comments:

Post a Comment