Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, August 11, 2015

RUFANI YA DR DEVOTA MARWA YATUPWA NA KAMATI YA RUFAA YA TFF



KAMATI ya rufaa ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetupa rufaa ya Dr. Devota John Marwa, juu ya jina lake kuenguliwa kwenye orodha ya wagombea wa TWFA na kamati ya uchaguzi wa soka la wanawake.
Akitoa ufafanuzi wa shauri hilo Mwenyekiti-Kamati ya Rufani za Uchaguzi ya TFF, Julius M. Lugaziya alisema utaratibu wa kuwasilisha rufani ulikiukwa, na hapa ndipo rufaa hii inapokwaa kisiki.  Chini ya Ibara ya 13 (1) cha Kanuni ya Uchaguzi (Electoral Code), mgombea ambaye hakuridhika na maamuzi, atawasilisha rufaa yake ndani ya siku 3 (tatu) tangu uamuzi anaoupinga ulipotolewa.
“Kipengele cha 3 (tatu) cha ibara hiyo kinasema kwamba Mrufani yoyote atakuwa na uhalali endapo rufaa yake imewasilishwa kwa mujibu wa kanuni hizo.  Uamuzi unaolalamikiwa ulitolewa tarehe 22 Julai 2015, sababu za rufaa ziliandaliwa tarehe 27 Julai na sababu hizo za rufaa zililipiwa tarehe 28 Julai, 2015. Ni dhahiri kwamba rufaa ililetwa nje ya muda uliowekwa na kanuni, na kwa hiyo inakosa uhalali kisheria na kikanuni”, alisema Lugaziya.

Pia alisema japo katika mwenedo na maamuzi yake Kamati ya Rufani za Uchaguzi haifungwi na taratibu za kimahakama, suala la muda wa kuwasilisha rufani sio miongoni mwa mambo ambayo Kamati inaweza kutoyazingatia kwa sababu hiyo, Rufaa hii imetupwa, lakini kwa sababu tofauti na zile za Kamati ya Uchaguzi.
Lugaziya alisema Kamati ya Rufani za Uchaguzi inapenda kwa namna ya kipekee kumpongeza mrufani kwa jitihada alizozionesha kutaka kuitumikia TWFA. Ni matumaini ya Kamati kuwa hatokata tamaa, na kwamba atakuwa tayari, akitakiwa kufanya hivyo, kupitia taalum yake, kushirikiana na wenzake katika jitihada za kuendeleza soka la akina mama lililo na changamoto lukuki.
Mwomba rufani, Dr. Devota John Marwa, (Mrufani) ni msomi mbobezi katika taaluma ya michezo, akiwa ni mhadhiri katika kitengo kinachojihusisha na taaluma ya michezo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na aliomba kugombea uenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu wa Wanawake(TWFA).
Maombi yake yalikumbana na pingamizi zilizoletwa na Bi. Chichi Mwidege na Bi. Mwajuma Noty, ambao kwa pamoja walimwekea pingamizi Mrufani, kwamba hakidhi matakwa ya kanuni za kugombea nafasi ya Mwenyekiti katika Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 9 (tisa) kipengele cha 3 (tatu), kinachomtaka mgombea awe amejihusisha na uongozi wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.
 Aidha Ibara ya 28 kipengele cha 3 (tatu), kinamtaka mgombea awe amejihusisha japo miaka miwili katika shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu nchini. 
Kamati ya Uchaguzi iliridhia mapingamizi hayo na kuliondoa jina la mrufani katika orodha ya wagombea wa nafasi hiyo ya Mwenyekiti.

No comments:

Post a Comment