Nguvu ya Arsenal na jibu la Sterling kwa City
*Chelsea watazuilika? Man United kitaeleweka?
MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya England (EPL) unaanza huku timu zikiwa na
mabadiliko kadhaa.
Arsenal wanakuja wakiwa kwenye kiwango kizuri kilichodhihirishwa na
mechi za ziara ya kabla ya msimu, wakijilundikia makombe matatu.
Manchester City bado kwenye
beki
Tuanze na Manchester City walioshinikiza hadi kufanikiwa kumsajili
mshambuliaji kinda wa kati wa Liverpool, Raheem Sterling (20).
Sterling anadhaniwa atawasaidia City kutatua matatizo kadhaa ikiwa ni
pamoja na ukosefu wa kasi, ujana, na mchezaji wa England.
Ndiyo maana City walilipa pauni milioni 49 kama ada kwa Liver lakini
pia na Sterling mwenyewe akalamba mkataba ambao atalipwa pauni milioni 47. Ni
wazi atawaimarisha City haraka.
Hata hivyo, kuna maswali mengine yanabaki bila majibu – nani ni
mshirika wa nahodha Vincent Kompany kwenye ulinzi?
Uhuishaji wa kikosi hiki uko wapi wakati mabeki wote wanne pale nyuma wameshafikisha
umri wa miaka 30? Sterling ni mzuri lakini yeye mwenyewe atamudu kuwapandisha
City?
Arsenal watatoa ushindani wa
kweli EPL?
Arsenal ambao walifanikiwa kuwafunga Chelsea 1-0, ikiwa ni mara ya
kwanza kwa Arsene Wenger katika mechi 14 zilizopita dhidi ya Jose Mourinho,
wamejilundikia makombe matatu ya ‘kishikaji’.
Je, watafanikiwa safari hii kuwa washindani wa kweli wa ubingwa wa
England? Watamudu hilo wakiwa na Olivier Giroud kama tegemeo lao kwenye
upachikaji mabao?
Walimtaka Karim Benzema lakini kocha wa Real Madrid, Rafa Benitez
amewaambia wasahau hilo. Je, hakuna mwingine ambaye angefaa kuongezwa hapo kama
alivyoshauri mkongwe wa Arsenal, Thierry Henry?
Anasema ili kutwaa ubingwa, Arsenal wanahitaji mpachika mabao wa
kiwango cha juu kabisa. Giroud amefanya kazi kubwa na utumishi mwema katika
misimu mitatu iliyopita, lakini utafiti unaonesha kwamba si rahisi awafikie
akina Diego Costa, Sergio Aguero wala Robin van Persie. Sasa timu nyingine
zikiwa na wapachika mabao wakali ni vigumu kwa Giroud kuwazidi. Labda wategemee
nguvu ya Alexis Sanchez, Theo Walcott kama atakuwa na utimamu wa mwili kwa muda
mwingi na Alex Oxlade-Chamberlaini anayetaka kuwa na msimu mzuri ujao.
Manchester United watarejesha
heshima?
Klabu hii ipo kwenye kipindi cha mpito, wakijaribu bado kusimama tangu
waondokane na kocha Alex Ferguson.
Chaguo na mrithi wake, David Moyes alishuhudia akiwaporomosha hadi
nafasi ya saba mwisho wa msimu, akaondoka na nafasi yake kuchukuliwa na Louis
van Gaal ambaye anaifumua na kuifuma upya United.
Zama za wachezaji wa England kung’ara zinaelekea kuisha, kwani naye
anaonekana kwenda kwao na kulundika wachezaji. Anajiamini, anachukua hatua
akishafanya uamuzi na ndiyo maana aliwatupia virago Van Persie na Radamel
Falcao.
Analaumiwa kumuuza kwa Arsenal Danny Welbeck lakini yeye anasonga mbele
akisema hata David De Gea kama vipi bora aondoke kwa sababu ya msigano
unaoendelea, mwenyewe akitaka kurudi kwao Madrid, akachezee Real Madrid
wanaomhitaji.
United walionekana kuwa watupu kwenye kiungo kwa miaka michache
iliyopita na hiyo ndiyo tofauti yao na timu nzuri zaidi England na Ulaya.
Viungo wao walikuwa wazito na vijeba mno kiasi cha kupitwa na wale wa
Manchester City na Chelsea.
Huenda sasa yakawapo mabadiliko, hasa baada ya usajili wa Morgan
Schneiderlin kutoka Southampton na Bastian Schweinsteiger wa Bayern Munich,
wote wakiwa na nguvu, uzoefu na wenye kujiamini.
Wakiungana na Michael Carrick na Ander Herrera, wanatakiwa kuipaisha
timu, kudhibiti mchezo na kuwa na kiwango kizuri kwa ujumla. Kazi ipo kwa LVG
kujua jinsi ya kuwapanga.
Hata hivyo, kocha wa Barcelona, Joseph Guardiola anasema kwamba
Schweinsteiger hajapata kuwa na utimamu unaotakiwa wa mwili katika miaka mitatu
iliyopita, pengine ndiyo sababu alikubali kumuuza.
Chelsea watakamatika msimu huu?
Baada ya shika nikushike ya msimu wa 2013/14, msimu ulipita ulikuwa na
ushindani dhaifu zaidi kiasi cha Chelsea kwenda kwa mserereko kutwaa ubingwa,
licha ya kutangatanga kwao katika mechi za mwisho.
Waliwazidi wenzao hapo juu pamoja na Liverpool na Southampton kwa mbali
hivyo kwamba walifika mahali wakawa kama mwanariadha aliyefika karibu na mstari
wa mwisho kisha akaamua kuketi kusubiri wenzake.
Arsenal na klabu za Manchester wasipojirekebisha na kulianzisha mapema,
Chelsea wanaweza kufurahia tena, japokuwa dhamira kubwa inaonekana hata kutoka
kwa Liverpool, hasa kwa kusajili ‘lundo’ la wachezaji.
Mwisho wa msimu uliopita, kocha wa Chelsea, Jose Mourinho alisema
kwamba msimu huu utakuwa mgumu kutokana na tamaa ya timu nyingine kutaka kuwapokonya
kombe.
Anamtegemea sana nahodha na beki wake wa kati, John Terry ambaye hata
hivyo si jambo la ajabu iwapo msimu utamkataa kwa sababu umri wake unakwenda.
Gary Cahill yupo na jitihada za kumpata John Stones wa Everton hazina
uhakika wa kufaulu, na hata akiwapo Stones, uwapo wa tu tofauti na Terry ambaye
Benitez alipata kumweka benchi akidai ni mzee mambo ni tofauti.
Wanamtegemea sana Diego Costa katika ushambuliaji na hata walimchezesha
pale anapokuwa na tatizo kidogo la utimamu wa mwili.
Alikosa mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Arsenal kwa sababu misuli yake
ya paja imeanza tena matatizo kama ilivyokuwa msimu uliopita. Hali inaweza kuwa
mbaya zaidi na hapo Chelsea watasikitika.
Pengine Mourinho atamtegemea zaidi mchezaji wake mpya aliye hapo kwa
mkopo kutoka Monaco,
Radamel Falcao aliyeahidi kumnoa na kumrejesha kwenye makali yake ya
zamani, baada ya kuvurunda akiwa na Manchester United msimu uliopita.
Karata za Rodgerz zasubiriwa
Liverpool
Msimu wa 2013/14 ulielekea kuwapa ubingwa Liverpool kama si kuvurunda
katika mechi zao tatu za mwisho na kushindwa na Man City.
Ulikuwa msimu wa mwisho kabla ya kumuuza Luis Suarez kwa Barcelona,
pengo ambalo hata sasa hawajaweza kuliziba licha ya kusajili wachezaji wengi,
wakiwamo washambuliaji.
Kiangazi hiki wamempoteza Sterling wakati Daniel Sturridge anaendelea
kujiuguza na huwa anaumia mara kwa mara. Msimu uliopita walifunga mabao karibu
60 pungufu yale ya msimu aliomalizia Suarez. Wamemaliza ligi wakiwa nafasi ya
sita na wakichapwa mabao sita na Stoke.
Wamefanya usajili na matarajio ni kwamba Christian Benteke
aliyesajiliwa kwa pauni milioni 32 kutoka Aston Villa atakuwa mtu wao muhimu
pale mbele. Kuna Roberto Firmino aliyesajiliwa kwa ajili ya kiungo cha
ushambuliaji kwa pauni milioni 29 kutoka Hoffenheim.
Yupo Danny Ings aliyeonesha makali msimu uliopita kabla kocha Brendan
Rodgers hajamsajili.
Timu zilizopanda daraja zina
mtihani
Timu tatu zilishuka daraja msimu uliopita, moja ikiwa ndio kwanza
ilikuwa imepanda, Burnley. Walibaki na kikosi kilichopanda lakini hakikumudu
makeke, kimeshuka.
Queen’s Park Rangers (QPR) ni wengine walioshuka baada ya kupanda msimu
mmoja kabla, wakiwa pia walikuwa wameshuka msimu mmoja tu kabla chini ya kocha
Harry Redknapp.
Mwaka huu Norwich wamerudi EPL wakiwa na kikosi kile kile walichokuwa
nacho huko chini na si tofauti sana na kilichoshuka daraja.
Wapya wengine ni Watford ambao wamesajili majina mapya katika
kujiimarisha. Bournemouth ndiyo mara yao ya kwanza wanaingia EPL na wamekuja na
maingizo machache mapya nay a maana. Tusubiri tuone kama watamudu kupata walau
nafasi za kati za msimamo wa ligi.
No comments:
Post a Comment