SHINDANO la wazi la mchezo wa gofu (KCB EAST Africa
Golf tour) linatarajiwa kufanyika Agosti 3 mwaka huu katika Viwanja vya Lugalo
Dar es Salaam.
Akizungumza Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa klabu ya
Lugalo, Brigedia Jenerali mstaafu, Michael Luwongo alisema shindano hilo
litashirikisha wachezaji 150 kutoka nchi mbalimbali na klabu za hapa nchini.
Luwongo alisema lengo ni kupata timu ya wachezaji
wanne watakaokwenda kushiriki mashindano Nairobi, Kenya Desemba 6 mwaka huu.
"Maandalizi ya shindano hili yanaendelea vizuri,
mpaka sasa tunaendelea kuboresha miundombinu ya viwanja vyetu ili shindano
lifanyike kwa weledi” alisema Luwongo.
Pia aliipongeza Benki ya KCB kwa udhamini wao na
kuwataka wale ambao hawajathibitisha ushiriki wao wafanye haraka muda umeisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa KCB, Cosmas Kimario
alisema benki hiyo inatoa huduma kwa jamii pamoja na michezo mbalimbali ikiwemo
riadha, mpira wa miguu na ngumi.
"Tuna uhakika hii timu itakayokwenda Kenya
itafanya vizuri na kurudi na ushindi nyumbani, ili fainali ijayo ifanyika hapa
nchini, alisema Kimario.
Alisema wameamua kuwekeza katika michezo kwa lengo la
kukuza vipaji vya vijana wadogo wanaochipukia.
Naye nahodha wa klabu ya Lugalo, Meja Japhet Masai
alisema shindano hilo litachezwa kwa mfumo wa kuhesabu mashimo kwa pointi na atakayepata
pointi nyingi atapata nafasi ya kwenda Kenya.
No comments:
Post a Comment