Pages

Monday, June 1, 2015

YANGA YAMTAMBULISHA RASMI BUSUNGU LEO


  Afisa habari wa Yanga Jerry Muro (katikati) akimkabidhi jezi kiungo mshambuliaji wao mpya, Balimi Busungu (kulia) aliyekuwa akichezea Mgambo JKT ya Tanga kwa mkataba wa miaka miwili baada ya kumtambulisha kwa wandishi wa habari leo. Kushoto ni meneja wa timu ya Yanga, Hafidh Salehe. (Picha na Rahel Pallangyo)




UONGOZI wa Yanga umemtambulisha mchezaji mpya waliyemsajili Malimi Busungu huku wakitamba kuhamia katika usajili wa kimataifa.
Busungu ambaye msimu uliopita alifanya vizuri akiitumikia Mgambo Shooting, alisajiliwa mwishoni mwa wiki  kama mchezaji huru kwa mkataba wa miaka miwili baada ya mkataba wake na Mgambo kumalizika mwishoni mwa msimu.
Akizungumza jana na waandishi wa habari Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga Jerry Muro alisema walivutiwa na kiwango cha Busungu alichoonesha katika timu yake ya Mgambo na hivyo kuamini kuwa atawasaidia katika mechi za kimataifa.
“Sisi kama Yanga tunapenda kusema kuwa tulivutiwa na kiwango cha Busungu, kazi tuliyopewa tumaimaliza na tumempa jezi namba 16 ambayo aliichagua mwenyewe,”alisema.
Busungu alikabidhiwa jezi iliyokuwa ikivaliwa na Nizar Khalfan ambaye mkataba wake umekwisha Yanga. Mchezaji huyo inadaiwa tayari amepata ulaji katika timu ya Mwadui Fc na mchezaji mwenzake wa timu hiyo  Jerrison Tegete.
Usajili wa Busungu utafanya idadi ya waliosajiliwa msimu huu kufikia wanne baada ya Deus Kaseke, Benedicto Tinoko na  Haji Mwinyi.
Muro alisema baada ya Busungu wanahamia kimataifa ambapo tayari wamefanya mazungumzo na wachezaji mbalimbali na kwamba  hivi karibuni watawatambulisha.
Miongoni mwa wachezaji ambao wamekuwa wakitajwa kusajiliwa ni Donald Ngoma wa FC Platinum ya Zimbabwe. Alisema usajili wa wachezaji wengi wa kimataifa  utaendelea kutegemea na ombi lao la kusajili wachezaji nane kama litapitishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

No comments:

Post a Comment