UONGOZI wa
Yanga umemtambulisha mchezaji mpya waliyemsajili Malimi Busungu huku
wakitamba kuhamia katika usajili wa kimataifa.
Busungu
ambaye msimu uliopita alifanya vizuri akiitumikia Mgambo Shooting, alisajiliwa mwishoni
mwa wiki kama mchezaji huru kwa mkataba
wa miaka miwili baada ya mkataba wake na Mgambo kumalizika mwishoni mwa msimu.
Akizungumza
jana na waandishi wa habari Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga
Jerry Muro alisema walivutiwa na kiwango cha Busungu alichoonesha katika timu
yake ya Mgambo na hivyo kuamini kuwa atawasaidia katika mechi za kimataifa.
“Sisi kama
Yanga tunapenda kusema kuwa tulivutiwa na kiwango cha Busungu, kazi tuliyopewa
tumaimaliza na tumempa jezi namba 16 ambayo aliichagua mwenyewe,”alisema.
Busungu
alikabidhiwa jezi iliyokuwa ikivaliwa na Nizar Khalfan ambaye mkataba wake
umekwisha Yanga. Mchezaji huyo inadaiwa tayari amepata ulaji katika timu ya
Mwadui Fc na mchezaji mwenzake wa timu hiyo
Jerrison Tegete.
Usajili wa
Busungu utafanya idadi ya waliosajiliwa msimu huu kufikia wanne baada ya Deus
Kaseke, Benedicto Tinoko na Haji Mwinyi.
Muro alisema
baada ya Busungu wanahamia kimataifa ambapo tayari wamefanya mazungumzo na
wachezaji mbalimbali na kwamba hivi
karibuni watawatambulisha.
Miongoni mwa
wachezaji ambao wamekuwa wakitajwa kusajiliwa ni Donald Ngoma wa FC Platinum ya
Zimbabwe. Alisema usajili wa wachezaji wengi wa kimataifa utaendelea kutegemea na ombi lao la kusajili
wachezaji nane kama litapitishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
No comments:
Post a Comment