CAIRO, Misri
KLABU tatu za
Algeria zimepangwa katika kundi moja la michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika,
ikiwa ni mara ya kwanza katika historia ya michuano hiyo kutokea kitu kama
hicho.
Mabingwa watetezi Entente
Setif watakutana na wenzao wa USM Alger na MC Eulma katika mechi za Kundi B,
huku timu ya Al Merreikh ya Sudan ikikamilisha kundi hilo.
Nchi 12 za juu katika
bara la Afrika kawaida hutoa timu mbili kila moja, lakini imekuwa tofauti kwa
Algeria baada ya Entente Setif kushinda taji hilo mwaka jana, nchi hiyo ikapata
nafasi nadra ya kuingiza timu tatu katika michuano hiyo msimu huu.
Ratiba hiyo ya
makundi ilipangwa katika Makao Makuu ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF)
yaliyopo jijini hapa jana.
TP Mazembe Englebert ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ndio timu pekee iliyofuzu kwa hatua hiyo kutoka
nje ya nchi za Afrika Kaskazini zinazozungumza Kiarabu, ikipangwa katika Kundi
A.
Timu zingine zilizomo
katika kundi hilo ni pamoja na Smouha (Misri), Moghreb Tetouan (Morocco) na Al
Hilal (Sudan).
Mechi za hatua hiyo
ya makundi zitaanza mwishoni mwa Juni huku timu mbili za kwanza kutoka kila
kundi zitafuzu kucheza nusu fainali ya mechi mbili za nyumbani na ugenini
Septemba na Oktoba.
Fainali ambayo
itachezwa Oktoba na Novemba nayo itapigwa kwa mtindo wa mechi mbili za nyumbani
na ugenini.
Ratiba kamili:
Kundi A: Smouha (Misri), Moghreb Tetouan (Morocco), TP Mazembe
Englebert (DR Kongo) na Al Hilal (Sudan).
Kundi B: Entente Setif (Algeria, mabingwa watetezi), USM Alger
(Algeria), Al Merreikh (Sudan), MC Eulma (Algeria)
No comments:
Post a Comment