Pages

Friday, January 2, 2015

ASHANTI YATOA ZAWADI YA MWAKA MPYA KWA MASHABIKI BAADA YA KUIFUNGA KIMONDO 5-3



 
Mshambuliaji wa Ashanti United ya Ilala, Moses Romward, (katikati) akijaribu kuwatoka mabeki wa Kimondo FC ya Mbeya wakati wa mchezo wa Ligi daraja la kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam, Ashanti ilishinda kwa mabao 5-3


TIMU ya Ashanti ya jijini Dar es Salaam juzi  iliifundisha jinsi ya kusakata kabumbu timu ya Kimondo FC ya Mbeya baada ya kuifunga mabao 5-3 kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza uliochezwa Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.

Kwenye mchezo huo ambao ulikuwa umejawa na vituko toka kwa mashabiki wa Ashanti ulishuhudia Kimondo wakipata bao la mapema kwenye sekunde 40 lililofungwa na Peter Tweve aliyeunganisha mpira uliokuwa unagaagaa kwenye eneo la goli baada ya mabeki wa Ashanti kutegeana kuuondoa.

Baada ya bao hilo Ashanti walicharuka na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 14 lililofungwa na Seleman Sultan aliyewazidi mbio wachezaji wa Kimondo.

Dakika ya 34 Kimondo walipata bao la pili lililofungwa na Mpoki Mwakinyuke na Ashanti walisawazisha dakika ya 36 bao likifungwa na Idd Seleman aliyefunga pia bao la nne kwenye dakika ya 43

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kufanya mabadiliko hali iliyosababisha mchezo kuwa wa kasi na dakika ya 49 Kimondo walifanikiwa kuongeza bao lililofungwa na Mateo Danny lakini Ashanti nao walisawazisha bao hilo dakika ya 66 lililofungwa na mshambuliaji Moses Romward.

Ashanti walifunga Karamu ya mabao dakika ya 87 baada ya Denis Omary kupiga mpira wa faulo akiwa nje ya eneo la penati na kumpira kutinga wavuni moja kwa moja.

Katika hali isiyotegemewa beki wa Ashanti, Mohamed Juma bega la mkono wa kushoto lilichomoka hali iliyofanya madakatari wa huduma ya kwanza kumkimbiza hospitali ya Amana na gari la wagonjwa ambalo lilikiwepo uwanjani.

Akizungumza baada ya mchezo huo, kocha wa Ashanti Mbaraka Hassan aliwapongeza wachezaji wake kwa ushindi walioupata na kusema kuwa ni zawadi tosha kwa mashabiki wao.

No comments:

Post a Comment