Pages

Wednesday, October 9, 2013

WACHEZAJI WATANO WATATA LIGI KUU ENGLAND


LONDON, England
KATIKA karne ya 21, kumetokea vituko vingi sana Ligi Kuu England, na hakika vimeleta mshangao kwa mashabiki, viongozi, wanazi wa soka na wengine. Kwa ufupi hapa tunakuletea wachezaji watano wanaotajwa ni wakorofi zaidi walioshangaza ulimwengu wa soka.

5. Lee Bowyer
Huyu alianza soka kwa kuichezea timu ya Leeds United, iliyotamba enzi zake, kabla ya kujiunga na Newcastle United na kumalizia soka lake West Ham United, zote za England.  Utata wa Bowyer ulianzia Charlton, ambapo yeye na wachezaji wenzake walitajwa kuwa wavuta bangi sugu. 

Utata zaidi ulikuja baada ya kufukuzwa katika timu ya Leeds. Kwanza, Bowyer alituhumiwa kwa ubaguzi akiwa kwenye maduka ya McDonalds, kisha mchezaji mwenzake, Jonathan Woodgate alipewa adhabu baada ya kusababisha ajali nje kidogo ya mji wa Leeds, katika klabu ya usiku. 

Kesi hiyo ilimgusa moja kwa moja Bowyer, ndipo uongozi wa Leeds United ukaamua kumfukuza. Bowyer aliwahi kuzipiga kavu kavu na mchezaji mwenzake, Kieron Dyer, na baadaye akafungiwa mechi 6, huku Jeshi la Polisi likimkamata kwa ukorofi. Katika maisha yake ya soka alipewa kadi za njano 80 na kadi nyekundu 5 na alijulikana kwa kukunjana ngumi na wachezaji mbalimbali kwenye mechi za Ligi Kuu England.

4. Ashley Cole
Beki mahiri wa kushoto aliyeanzia soka lake Arsenal na baadaye akajiunga na Chelsea, ambayo anaichezea mpaka sasa. Hivi karibuni Cole ameichezea timu ya taifa ya England mechi 100 na alipewa unahodha siku ya mchezo huo na mingine mara kadhaa.
Soka lake lilianzia Arsenal, na alikulia kwenye timu hiyo akawa mchezaji muhimu wa Arsene Wenger. Lakini maisha yake ya soka awali yalikuwa ni kuwadanganya waamuzi kwa kujirusha kila alipokabiliana na wapinzani wake. 

Akiwa ndiye staa wa timu hiyo, aligundulika kuongea na kocha Jose Mourinho, aliyekuwa akifundisha Chelsea. Cole ni mtata, kwa sababu aliwahi kusema haipendi nchi yake ya England, na hataki hata kuishi nchi hiyo.
Alipopewa ofa ya mshahara wa pauni 55,000 kwa wiki, alikataa mara moja na kuichanganya Arsenal. Cole aliwahi kumdunda mwamuzi Mike Riley wakati alipotaka kumpa kadi kwenye mchezo dhidi ya Hotspurs. Mwaka 2012 alikitukana Chama cha Soka cha England, FA kwa kuwaita kundi la wapumbavu.

3. Eric Cantona
Staa aliyetisha sana kwenye Uwanja wa Old Trafford, lakini anakumbukwa kwa utata mwingi aliowaachia mashabiki wa England. Akiwa England, aliichezea Manchester United, akiwa ni raia wa Ufaransa. Cantona si staa tu wa Man United, pengine anakuwa mchezaji mwenye sifa nyingi kuliko wote waliowahi kucheza ligi kuu England. 

Lakini mashabiki wa timu pinzani hawakumpenda kabisa, sababu alikuwa mtata sana kwenye maamuzi yake. Cantona aliwahi kukwaruzana mara nyingi na mashabiki wa Leeds United kwenye uwanja wa Elland Road. 

Pia anakumbukwa kwa kumpiga mateke shabiki wa Crystal Palace, hali iliyozidisha ukorofi wake. Baada ya kung-fu hiyo, FA ilimfungia kutocheza soka miezi 9. Licha ya kuchukiwa, Cantona aliisaidia Man United kutwaa mataji manne ya Ligi kuu, mawili ya FA na Kombe la Ligi.

2. Luis Suarez
Staa wa timu ya Liverpool, mzaliwa wa Uruguay. Ana kipaji kizuri cha soka, lakini ni mtata kupindukia tangu akiwa ligi kuu Uholanzi. Kabla ya kuzua utata wake Liverpool, alifanya hivyo akiwa na timu yake ya Ajax, aliwahi kumng’ata meno mchezaji wa PSV na kufungiwa mechi 7.

 Mwaka 2010 kwenye fainali za kombe la dunia, Afrika Kusini, alizuia mpira uliokuwa ukieleka wavuni ambao ungeipa ushindi Ghana na kusonga mbele, lakini ni Uruguay ilifanikiwa kutinga nusu fainali.
Licha ya utata, Suarez aliifungia Liverpool mabao 30 msimu uliopita katika mashindano yote. 

Mwaka 2011 alikuwa na utata baada ya kumbagua beki wa Man United, Patrice Evra na kufungiwa mechi nane. Baada ya kukataa kumpa mkono Evra msimu uliopita, alifungiwa kwa kumng’ata mkono Branislav Ivanovic katika mchezo wa timu yake dhidi ya Chelsea na kufungiwa mechi 12, ambapo amemaliza.

1.       Mario Balotelli
Alikuwa mchezaji wa Manchester City, ambako alijiunga akitokea Inter Milan. Mkorofi kweli huyu, sijui tutaanza na tukio gani kukumbuka wakati wake akiwa Etihad. Alianza utata wake kwenye mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Manchester United, ambapo timu yake ilishinda mabao 6-1.

Pambano hilo la watani wa jadi lilimshuhudia Balotelli akishangilia bao kwa kuonyesha fulana yenye maandishi “Why Always Me?” Baadaye katika mchezo muhimu wa kuamua bingwa wa ligi kuu England dhidi ya Tottenham Hotspurs, Balotelli alimpiga kichwa kiungo wa Spurs, Scot Parker. 

Lakini jambo zuri kwenye mchezo huo alifunga bao kwa njia ya penalti, ambalo liliipa timu yake matumaini ya ubingwa. Pia aliwahi kugombana na Kolo Toure, pamoja na aliyekuwa kocha wake, Roberto Mancini. Januari mwaka huu alijiunga na AC Milan, lakini ligi kuu England haitamsahau nyota huyo.

No comments:

Post a Comment