Pages

Wednesday, October 9, 2013

FIESTA YA BAYERN MUNICH



MUNICH, Ujerumani
SI soka tu. Si chenga za Robben. Si hamasa na ufundi wa Pep Guardiola. Si kasi ya Frank Ribery. Si kukaba kwa Philip Lahm au Rafinha. Lakini Bayern Munich wanajua namna ya kula bata.
Unajua kilichotokea? Pep Guardiola amekuwa mmoja wa watu walioonja raha ya kuifundisha Bayern Munich. 

Kila timu inakuwa na utamaduni wake. Brazil wanapenda sherehe za Samba, lakini Bayern Munich wao wanayo Oktoberfest ambayo inakuwa full bata kila mwaka.
Munich ni mabingwa wa Ulaya. Wanakunywa na kulewa, wanaburudika kwa kila namna, huo ndio utamaduni wao na kutangaza siku yao ya mwaka, Oktoberfest. 

Oktoberfest ni siku ya kifamilia katika timu ya Bayern Munich. Ni sherehe za kila mwaka kama ambavyo hapa Tanzania inavyofanyika Fiesta katika mikoa mbalimbali.
Kocha huyo wa zamani wa Barcelona, alionja utamu wa kuifundisha timu hiyo pale alipolazimika kuvaa mavazi ya kiutamaduni, yeye na mkewe pamoja na wachezaji wote wa Bayern Munich. 

Sherehe hizo zinawaunganisha wachezaji, viongozi, wenyeji na wageni maalumu wanaoalikwa kuhudhuria Oktoberfest. Utamaduni wa sherehe hizo ni kuvaa kofia, kaptula na shati za drafti pamoja na viatu aina ya buti, ambavyo vinakuwa na mwonekano kama askari wa zamani.
Bayern ambayo inaongoza ligi ikiwa na pointi moja mbele dhidi ya wapinzani wake wa jadi, Borussia Dortmund, walionekana kuwa watulivu, huku kocha wao wakionekana kuwashangaza baada ya kuzizoea sherehe hizo mahususi. 

Si kucheza mpira pekee ambao umewapatia ushindi katika mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Ulaya katika kundi D, na ushindi wa kombe la Supercup dhidi ya Chelsea.
Bayern Munich wanaonekana kuzidi kukonga nyoyo za mashibaki kuanzia uwanjani mpaka kwenye sherehe zao za Oktoberfest. 

Kwenye sherehe hizo kunakuwa na wake zao, wapenzi wao, watoto, viongozi wa timu, wageni maalumu na waalikwa mbalimbali ambao hujumuika na wachezaji wa Bayern Munich.
Sherehe za mwaka huu zimetimiza miaka 180 tangu zilipoanza karne moja iliyopita.

OKTOBERFEST 16, WATU MILIONI 6
Utaona wake zao wamependeza, kocha wao anafurahia, watoto wanafurahia, kumbe sherehe hizo zilianza miaka 180 iliyopita.
Kwa mara ya kwanza sherehe za Oktoberfest zilianzia Kaefers Wiesenschaenke. Ni sherehe ya siku 16 ambazo watu wanakula bata ndani ya Jiji la Munich, inaanza wiki ya mwisho ya mwezi wa tisa kila mwaka hadi wiki ya kwanza ya mwezi Oktoba.
Watu milioni 6 husherehekea kila mwaka Oktoberfest, ambapo wenyewe huliita tamasha la ‘full bata” au “die Wies'n” (Theresienwiese). Oktoberfest ilianza mwaka 1810, ni sherehe za utamaduni kama ilivyo Samba Brazil.

Na mara nyingi zinafanyika wakati wa mapumziko ya soka, ambapo timu za taifa zinacheza mechi mbalimbali.
Bayern Munich itacheza mechi ya Ligi Kuu Oktoba 19, ambapo wataikaribisha Mainz kwenye uwanja wa Allianz Arena.

BATA NA KAZI
Wakati Guardiola akiwaongoza wachezaji wake kula bata kwenye sherehe za Oktoberfest, baadhi yao 15 watalazimika kurejea katika timu za taifa.
Kati yao wachezaji 7 wa Bayern Munich wameitwa katika timu ya taifa ya Ujerumani, ambapo wataichezea baada ya kula bata kwenye Oktoberfest. 

Winga Arjen Robben, anaamini kikosi chao kina kiwango bora, na mapumziko yamewapa hamasa zaidi.
“Nina hakika wachezaji wa Bayern tutafanya mambo mazuri na dunia nzima itafahamu zaidi. Baada ya sherehe hizi, tutaingia uwanjani tukiwa na ari zaidi huku mashabiki wetu wakitupa hamasa, na tutawafurahisha,” alisema Robben.

Hii si mara ya kwanza kwa Guardiola kushiriki sherehe kubwa kama hii, lakini kocha huyo anaonekana kukubalika zaidi kuanzia wachezaji, viongozi na mashabiki wa timu hiyo.
Wageni walioalikwa walijawa na hamu ya kukumbatiana na Guardiola wakidai amewapa furaha tangu kuanza msimu huu. 

BIA NA UBINGWA WA 23
Wachezaji wa Bayern Munich walikuwa wakinywa bia ambazo zimesajiliwa kwa jina la Oktoberfest. Wote waliunganisha na kusherehekea ubingwa wao wa 23, ambao waliutwaa msimu uliopita ndani ya uwanja wa Allianz Arena. 

Raha wanayopta Bayern Munich ni ya kipekee, kwani wanasherehekea wakiwa wametulia kwa kila upande.
Ligi ya mabingwa wanaongoza kundi lao. Ligi kuu Bundesliga wanaongoza na zaidi Oktoberfest ni kula bata la nguvu kwa kwenda mbele.


No comments:

Post a Comment