Pages

Wednesday, October 9, 2013

ZLATAN HUYU, NI TOFAUTI NA IBRAHIMOVIC YULE




Si vibaya, wakati mwingine mtu ukaamua kuishi kama ndege. Maisha hayana maana wakati mwingine, kama tu ukiwa huna maana na maisha yenyewe. Ni bora ukaishi kama ndege tu. Ukiamua kuimba, imba, tena imba kwa sauti bila kujali watu watasikiaje au watajali vipi. Maisha yanakuhitaji mwenyewe kwanza.

Zlatan Ibrahimovic! Hana tofauti na ndege, anaimba sana. Nyimbo zake ni nzuri sana masikioni mwake. Haijalishi  mtu mwingine atasikiaje. Na kwanini apoteze muda kujali hilo? Neno lake ni bora sana katika moyo wake. Hawezi kunyamaza, hawezi kustahamili, ataongea tu. Na ataongea kwa sauti, hajali ni nani atakwenda kulisikiliza.

Ana miaka 32 sasa, kichwani mwake anaamini yeye ni mchezaji bora sana duniani, hakuna kama yeye. Anaamini pia, mkewe, Helena Seger, ni mwanamke mzuri sana duniani, pengine kuliko wanawake wote unaoweza ukawadhania. Kila kitu bora na kizuri katika dunia hii, basi ni lazima kiwe kinamzunguka yeye tu.
Huyo ndiye Zlatan Ibrahimovic ‘ Ibra Cadabra’.  Mfalme wa soka kule nchini Sweden. Anajipenda sana, anapenda kujiongelea yeye tu, na haijalishi kwa ukubwa gani. Ndiyo tabia yake, siyo kosa lake pia! Huenda ndivyo alivyoumbwa hivyo.

John Carew, yule mtu mrefu ambaye kwenye ile miaka ya 2000 hadi 2004 alikuwa miongoni mwa watu walioing’arisha sana Valencia wakati ule. Ukiikumbuka Valencia ya wakati ule, basi utayakumbuka vyema yale mabao hodari ya vichwa yaliyokuwa yakifungwa na John Carew. Msimu uliopita alionekana akiwa na jezi ya West ham. Hayupo kama zamani, lakini bado anaendelea kuitwa John Carew.

John Carew, kwa bahati mbaya sana hamuelewi Ibrahimovic. Hamuelewi kabisa.  Hauelewi uchezaji wake, haelewi pia  kwa nini ‘Ibra Cadabra’ anajiingiza katika kundi la wachezaji bora duniani. Ni kawaida kwa wachezaji kuwaziana hivi. Lakini Ibra alijibu kwa wepesi sana, kuwa alichokuwa akikifanya Carew akiwa na mpira, yeye anaweza kukifanya akiwa na chungwa. Hapa unahitaji akili kiasi kujua Ibra alikuwa anamaanisha nini kwa Carew. Dharau iliyoje hiyo!!

Hampendi Lionel Messi, hampendi sana Pep Guardiola, haipendi kabisa Barcelona. Hawakumjali, hawakumthamini, alipuuzwa. Anajijua yeye ni mkubwa sana. Anapenda iwe hivyo,  siku zote tena kwa mtu yeyote. Vipi Barcelona wampuuze? Anawachukia. Aliwahi kukaririwa akisema kuwa yeye ni sawa na gari ya Ferrari, lakini Barcelona walimtumia kama Fiat.

Zlatan anajijali sana, hajawahi kuamini kama kuna kitu kinapungua katika maisha yake. Pamoja na uchezaji wake wote, hajawahi kuwa na wakala. Anaamini mawakala siku zote wapo kwa ajili ya kumfanya mchezaji mbovu kuonekana wa thamani. Yeye ni mchezaji mkubwa, vipi awe na wakala? Timu kubwa ni lazima zimtafute yeye, kwa kuwa ubora wake hauhitaji mtu wa kumpigia kelele. Zlatan huyo!!

Chistiano Ronaldo, pamoja na madoido yake yote, lakini hajawahi kuifikia Jeuri ya Ibrahimovic. Balotelli, pamoja na utukutu wake wote, lakini hajawahi kumsogelea Ibrahimovic. Nani anaweza kuwa rafiki yake? Kwa lipi? Kwanini? Labda Mourinho! Wanaishi katika fikra moja. Pengine ni rahisi kuelewana.

Wakati Lionel Messi akiwa hajui ni lini anaweza akamsamehe Ibrahimovic, kuna Zlatan Ibrahimovic mwingine, tofauti kabisa na Ibrahimovic anayeishi katika kichwa cha Pep Guardiola. Yule Ibrahimovic mwenye jeuri, dharau, kiburi na kila aina ya majivuno. Zlatan huyu mwingine anashangaza kidogo, siyo Yule Ibrahimovic tunayemjua.

Hajrudin Kamenja, ana umri wa miaka nane. Anatokea katika taifa la Bosnia, katika kitongoji cha Vares, kilomita kadhaa kulifikia jiji pendwa la Sarajevo. Dogo Hajrudin ametushangaza kidogo. Kwa miaka sita sasa, amelazwa tu kitandani. Anasumbuliwa na kansa ya mapafu ‘leukemia’. Na kwa mujibu wa ripoti ya madaktari, wanadai kuwa amebakiza mwezi mmoja tu, kabla ya kufikwa na mauti.

Inasikitisha sana, inaumiza pia. Mama yake Hajrudin ndiye anaumia kuliko wote. Amemwambia mwanae, ni kitu gani cha mwisho angependa amfanyiwe kabla ya kufikwa na mauti? Simanzi inaishia hapa sasa! Dogo Hajrudin amechagua kumuona Zlatan Ibrahimovic, ndiyo kitu cha mwisho anachokipenda katika dunia hii. Hapahitaji mshangao hapa?

Kwanini amekuwa Zlatan? Kwanini hakuwa Justin Beiber? Kwanini hakuwa hata Jaden Smith? Labda Hajrudin anapenda sana mpira, sasa kwanini hakuwa Lionel Messi? Au Christiano Ronaldo? Kwanini sio David Beckham pia? Kwanini Dogo amemchagua Zlatan? Anapenda nini kwa Zlatan Ibrahimovic?

Unahitaji kutulia kidogo, ili uweze kupata majibu yaliyotulia pia. Huenda Dogo Hajrudin naye ameamua kuishi kama ndege, ameimba, tena ameimba kwa sauti, sauti ambayo huenda itamkera sana Pep Guardiola. Ndiyo ukweli wake. Kwanini awe mnafiki? Yule Zlatan jeuri, mwenye dharau na kiburi, ndiye kipenzi chake.

Najua sasa,  Zlatan Ibrahimovic, atakuwa akipoteza muda wake mwingi katika lile jumba lake la kifahari kule Jijini Paris, akili itakuwa ikiwaza mambo mawili tu. Nini afanye kwa Dogo Hajrudin? Na lipi afanye, ili watu waamini kuwa Yeye ni Tofauti na Ibrahimovic tuliyekuwa tukimfahamu? Mimi nasubiri, tena nasubiri kwa hamu, hamu ya kutaka kujua ni nini  ‘Ibra Cadabra’ atafanya.



No comments:

Post a Comment