Pages

Monday, September 2, 2013

WENGER: BENDTNER ATAZIBA PENGO



London, England

Arsene Wenger huenda akazidi kuwachefua mashabiki wa timu hiyo, baada ya kusisitiza kuwa hawana haja ya kupaniki kutokana na Arsenal kutokusajili, kwani Nicklas Bendtner atarejea Emirates kuziba pengo katika safu ya ushambuliaji.

Bendtner, ambaye hajaichezea 'The Gunners' kwa takribani miaka miwili iliyopita kutokana na kutolewa kwa mkopo Sunderland na baadaye Juventus, alionekana kama angeondoka Kaskazini mwa London majira haya ya joto.

Wenger amebaki na washambuliaji wawili tu, Olivier Giroud na Yaya Sanogo, baada ya Lukas Podolski kuelezwa kuwa atakuwa nje ya uwanja kwa wiki 10, kutokana na kuwa majeruhi kufuatia kuumia kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Fenerbahce ambayo Jumanne walishinda 2-0 .

Ingawa alitoa kipaumbele kwa kusajili mshambuliaji majira haya ya joto, Wenger sasa analazimika kumrejesha Bendtner baada ya kushindwa kuwasajili Luis Suarez, Wayne Rooney na Gonzalo Higuain.

"Nafasi yake ya kuondoka kwa sasa ni ndogo sana, na kama atarejea na nikamuona yupo fiti, nitamtumia," alisema Wenger akimzungumzia nyota huyo wa Kimataifa wa Denmark.

"Hatutapaniki kwa kununua, huo ndiyo uhakika. Unaweza kuniamini. Ninaweza kukupa simu yangu na utaona kuwa nilikuwa na zaidi ya wachezaji 50 nilikuwa natarajia kuwasajili mwisho wa siku.

"Ni mwenye furaha kabisa kwa kile tunachokifanya na kwa namna tunavyofanya mambo yetu. Siwezi kushiriki katika ukosoaji unaofanywa katika mchakato wangu wa usajili kwa timu."

No comments:

Post a Comment