Pages

Monday, September 2, 2013

HENRY JOSEPH KAZINI SIMBA LEO




KIUNGO Henry Joseph, leo anatarajia kuwapa raha Simba wakati timu hiyo itakapoivaa Mafunzo ya Zanzibar katika mechi ya kirafiki itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
 
Joseph amerejea kwenye timu hiyo baada ya kumaliza mkataba na Klabu ya Kongsvinger ya Norway, hivyo leo atakuwa mmoja wa wachezaji ambaye atatambulishwa kwa mashabiki kupitia mechi hiyo.

Wachezaji wengine ni beki wa Kimataifa Mrundi, Gilbert Kaze na Mshambuliaji mwezake, Amissi Tambwe waliotoka katika klabu ya Vital’O ya Burundi, ambao hawakuwemo katika utambulisho mpya wa wachezaji wa timu hiyo kwenye tamasha lao la  Simba Day.

Akizungumza na BINGWA  jana, Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, alisema baada ya kucheza mechi mbili za Ligi Kuu Tanzania Bara, wamerejea Dar es Salaam kujiandaa na mechi inayofuata dhidi ya Mtibwa Sugar itakayochezwa Septemba 14, mwaka huu.

Kamwaga alisema mechi hiyo itakuwa na faida kwao  kutokana na kujiandaa kuivaa Mtibwa, ikiwa ni baada ya kutoka sare ya mabao 2-2 na Rhino Rangers na baadaye kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya JKT Oljoro.

Alisema mechi hiyo itatoa nafasi kwa wapenzi na wanachama wa Simba, pamoja na mashabiki wa soka kwa ujumla, kupata fursa ya kuwaona kwa mara ya kwanza wachezaji hao ambao hawajawahi kuonekana wakicheza jijini Dar es Salaam.

Viingilio vya mechi hiyo, vitakuwa ni Sh 20,000 kwa VIP A, Sh 10,000 kwa VIP B, Sh 8,000 kwa VIP C na Sh 5,000 kwa mzunguko.

Wakati huo huo, alisema mechi hiyo itatumika na klabu kwa ajili ya mchezaji wake, Kiggi Makassi, ambaye atawaaga kabla ya kwenda nchini India, Septemba 9, mwaka huu, kwa ajili ya matibabu ya goti.

No comments:

Post a Comment