Pages

Monday, June 10, 2013

WATANZANIA WANG'ARA KWENYE MBIO ZA TAVETA NA KUWASHINDA WAKENYA

Katika kuhakikisha riadha nchini Tanzania inafuta uteja kwa wakimbiaji
wake kwa wafukuza upepo wa Kenya, Klabu ya Holili (HYAC) ya Mkoani
Kilimanjaro imedhihirisha hilo katika Taveta Athletics Championship
kwa kuwabwaga Wakenya katika mbio za meta 5000, 1500, 800 na 100.

Michuano hiyo ya Taveta imefanyika mwishoni mwa wiki katika Kaunti ya
Taita-Taveta katika Mkoa wa Pwani nchini Kenya katika wilaya ya Taveta
kwa kuwakutanisha wanariadha wa nchini Kenya huku Holili Youth
Athletics Club ikialikwa kutoka nchini Tanzania.

Katika Mbio za meta 5,000 alikuwa ni Baraka Williams aliyekimbia kwa
dakika 14:45:22 nafasi ya pili ikishikwa na Mtanzania mwingine
Abubakar  Joel aliyekimbia kwa muda wa 16:00:00  na nafasi ya tatu
ikashikwa na Mkenya Kivoko Makao ambaye alikimbia kwa muda wa
16:34:00.

Wambura Lameck, Mtanzania kutoka katika klabu ya Riadha kwa vijana
(HYAC) alionyesha uwezo katika mbio za meta 100 na 800 kwa wanaume;
katika mbio za meta 100 Wambura alikimbia kwa muda wa sekunde 12:67
akiwatupa Wakenya Walter Kamujalo (13:12), Emmanuel Paulo (13:70) na
Joseph Daudi (14:20).

Mbio za mita 800 Wambura Lameck alikimbikia kwa muda wa dakika 2:02:16
akimwacha Mkenya Ropya Nyingi ambaye alichukua muda wa dakika 2:04::14
na nafasi ya Tatu ikishikwa na Mtanzania kutoka HYAC Paulo Jackson
aliyekimbia kwa muda wa dakika 2:05:98, Wakenya wengine Joseph Daudi
(3:00:00) na Philip Matheka (3:04) walisshika nafasi mbili za mwisho.

Pia Watanzania waliwaonyesha kazi nyingine Wakenya katika mbio za meta
1500 pale Baraka Williams kutoka HYAC alipowakimbiza na kuongoza baada
ya kumaliza kwa muda wa dakika 3:48:77 akifuatiwa na Mkenya Vicent
Daniel kutoka Taveta aliyemaliza kwa kutumia muda wa dakika 4:16:85
nafasi ya tatu ikishikwa na Mtanzania mwingine kutoka HYAC Paulo
Jackson ambaye alikimbia kwa dakika 5:04:66 na Mkenya Tumuna Ludovick
akikimbia kwa muda wa dakika 5:09:07.

Kwa upande wa wanawake Watanzania Furaha Sambeke na Pendo Pamba
walifanya kweli katika meta 800 kwa kushika nafasi mbili za juu.

Furaha Sambeke anayenolewa na Klabu ya Holili Youth Athletics
alikimbia kwa muda wa dakika 2:30:00 na Pendo Pamba akimaliza kwa
dakika 3:10, nafasi ya tatu ilishikwa na Mkenya Emily Wamboi na ya nne
ikishikwa na Mkenya mwingine Cecily Kimale ambao wote walikimbia kwa
kuda wa dakika 3:22:00 na 4:12:00.

Taveta Athletics Championship imefanyika ikiwa na makusudi ya
kutengeneza Timu ya Riadha ya Taifa la Kenya ambako mchujo rasmi
utafanyika Mjini Mombasa kwa watanzania walioshinda katika mbio hizo
nao watakuwemo katika kinyang’anyiro hicho kwa ajili ya kupata uzoefu
zaidi kutokana na ukweli kwamba taifa la Kenya limekuwa bora katika
riadha barani Afrika.

No comments:

Post a Comment