Pages

Sunday, June 9, 2013

SERIE A ITABAKI NINI KAMA MASTAA WOTE WATAONDOKA?

MILAN, Italia
UHONDO na burudani ya mikikimikiki ya Serie A umefika mwisho na sasa unapisha tukio la usajili wa majira ya kiangazi, ambapo majina makubwa ya mastaa wa soka wa ligi hiyo wanahusishwa na mpango wa kutimkia kwingineko.

Kinatachotarajiwa kutokea ni kama kile cha mwaka jana, ambapo ligi ilipokwisha msimu wa usajili ulipoanza, ulishuhudia nyota kama Zlatan Ibrahimovic, Thiago Silva na Ezequiel Lavezzi wote wakihamia Ufaransa na wengine wakitimkia nchi nyingine za Ulaya.

Na sasa ikiwa karibu mwaka mmoja umepita, hakuna kilichobadilika sana juu ya uwezekano wa wachezaji wa ligi hiyo ya Italia wakihusishwa na mpango wa kuhama, licha ya kupata mafanikio kadha kwenye ligi hiyo.
Lakini, orodha ndefu ya wachezaji hao wanaotaka kuondoka Italia baadaye mwaka huu ikizidi kuongezeka, swali lililopo ni jinsi gani klabu za nchi hiyo zitaweza kujipanga upya hasa katika kipindi hiki cha mapinduzi mapya.

Ibrahimovic alikuwa mchezaji muhimu sana katika kikosi cha AC Milan na kwamba walikuwa wakimtegemea staa huyo kuweza kufanya katika michuano mbalimbali iliyoshiriki.
Lakini, kuondoka kwake kulimfanya Stephan El Shaarawy kuibuka na klabu hiyo kulazimika pia kumsajili Mario Balotelli kutoka Manchester City.

Kilichoikuta Milan mwaka jana ni kitu ambacho kinasuburi kuzikuta timu nyingine kutokana na klabu nyingine kutoka nchi mbalimbali za Bara la Ulaya kupanga kuvamia nchini humo na kunyakua wachezaji wao bora.
Orodha ndogo tu ya mastaa wa Serie A wanaowindwa na timu za nchi nyingine ni fowadi wa Fiorentina, Stevan Jovetic na wa Napoli, Edinson Cavani.

Wakali hao wanawindwa na klabu za England, huku nchini Hispania Real Madrid ikiripotiwa nayo kuhitaji saini ya mchezaji huyo.
Cavani ni mchezaji ambaye amekuwa kwenye kiwango bora kabisa kwa muda mrefu na kumeripotiwa kuna ofa ya euro milioni 63 inayomhusu nyota huyo na kwamba jambo hilo linaiweka pagumu Partenopei kuikataa ofa kubwa ya aina hiyo.

Ukiachana na kuwasili kwa Rafa Benitez, anayekwenda kurithi mikoba ya Walter Mazzarri, Cavani amekuwa mchezaji muhimu sana tangu alipojiunga na klabu hiyo ya Naples na ukweli ni kwamba klabu yake itapambana kuhakikisha hata kama anahama, haondoki kwa dau dogo.
Kuondoka kwa mastaa kama hao ni wazi kutaifanya Serie A kupungua ladha yake na hasa ukizingatia wachezaji wa kuchukua nafasi zao wakiwa bado hawafahamiki watakuwa ni wa aina gani.
Kwenye klabu ya Fiorentina napo hali itakuwa hiyo kutokana na Jovetic kuhusishwa na mpango wa kuihama timu hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti la Uingereza, Express, Chelsea ipo tayari kupambana na Arsenal katika kuwania saini ya staa huyo wa Montenegro na maofisa wake walionekana kwenda Fiorentina kufanya mazungumzo.
Kutokana na namna alivyoweza kuiongoza Viola, kuondoka kwa Jovetic kunaonekana kuwa ni pigo kubwa kwa klabu hiyo kama ataondoka. Kuwapo kwa mipango yake kujengwa chini ya Vincenzo Montella, ni suala linaloibua mjadala kwamba klabu hiyo itakuwa kwenye matatizo makubwa.
Katika msimu uliopita, Adem Ljajic, alionyesha kiwango kikubwa na kuonekana kama angekuwa mshambuliaji mahiri wa kati, huku kukiwapo kurejea kwa mshambuliaji Giuseppe Rossi, ambaye alikuwa majeruhi.

Na kama uvumi kama ulivyo, Fiorentina itamfukuzia Burak Yilmaz na Joaquin kuziba pengo hilo kama Jovetic ataondoka.
Claudio Marchisio, naye anahusishwa na mpango wa kutimkia Manchester United, kwa mujibu wa football-italia.net, wakati staa wa AS Roma, Daniele De Rossi kwa muda mrefu amekuwa akiwindwa na klabu za England.
Na kama uhamisho wote huo ukitokea, ni wazi kabisa Serie A itakuwa imepoteza wachezaji wake nyota ambao wangeweza kuwa nembo ya ligi hiyo yenye burudani kubwa.

No comments:

Post a Comment