Pages

Sunday, June 2, 2013

ROONEY KWENDA ARSENAL SIO DILI?


LONDON, England
MAJINA makubwa kwenye soka yamekuwa yakihusishwa na Arsenal wakati wa majira haya ya kiangazi. Kumaliza ligi ndani ya 'top four' kunawapa Arsenal nafasi hiyo, kwa sababu jambo hilo linawapa tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao.
Lakini, historia ya hivi karibuni ya klabu ya Arsenal linapokuja suala la usajili, uvumi wote unaohusu timu hiyo mara nyingi umekuwa hautimii.
Wakati majina hayo makubwa yakiendelea kuhusishwa na Arsenal, mjadala mkubwa ulioibuka kwa sasa ni kama baadhi ya wachezaji hao wataweza kufiti kwenye mfumo wa Washika Bunduki hao wa London.
Mmoja wa wachezaji hao wenye majina makubwa, anayehusishwa na Arsenal na ni wazi kabisa hataweza kuendana na staili ya kiuchezaji ya timu hiyo kama kweli itamsajili, ni Wayne Rooney.
Sawa, Arsenal inahitaji mshambuliaji, na kipaji cha Rooney hakina mjadala, lakini ukweli wa mambo Mwingereza huyo hataweza kufiti vizuri katika klabu hiyo inayonolewa na Mfaransa, Arsene Wenger.
Na kama kuna kigezo cha kufikiria kwamba Rooney ni mchezaji anayeweza kucheza mahali popote, lakini suala la kuvaa jezi za Arsenal ni jambo ambalo unapaswa kulifikiria katika wigo mpana.
Kitu cha kwanza kabisa kati ya vingi vinavyopaswa kufikiriwa kwenye usajili wa Rooney kwenda Arsenal ni suala la kiuchumi.
Rooney bila shaka anahitaji ada kubwa ya uhamisho na kwa mujibu wa Daily Mail, ni kwamba hata mshahara wake wa wiki utakuwa zaidi ya pauni 200,000. Jambo hilo litamfanya Rooney kuwa mchezaji anayelipwa fedha nyingi zaidi katika kikosi cha Arsenal.
Hicho ni kitu ambacho ni ngumu kuona kinatokea kwa Arsenal kulipa fedha nyingi kiasi hicho na kama itakubali kumsajili, basi atakuwa mchezaji ambaye atawagharimu sana.
Faida ya kuwa na Rooney kwenye kikosi ni kwamba atakuwa ari ya ushindi, kutokana na uzoefu alionao na kwamba kipaji chake kikubwa kitakuwa na thamani ya kutosha kwa Arsenal.
Lakini je, Wayne Rooney ni mchezaji sahihi kutua Arsenal? Je, kiwango chake ni kilekile kama ilivyokuwa zamani? Rooney ana umri wa miaka 27 na hivi punde ataingia kwenye kipindi muhimu kabisa cha maisha ya soka lake, lakini yeye anaonekana bado sana hajafikia kwenye ubora huo.
Kiwango chake kimekuwa kikiibua maswali kwa misimu michache iliyopita na haonekani kama ni mchezaji mwenye uwezo wa kutawala kama alivyokuwa akitarajiwa awali.
Kubadilika kwake ndani ya uwanja, ni kitu kinachomfanya kuwa na sifa kubwa, lakini jambo hilo si Arsenal ambalo wanalitaka. Sawa, anaweza kucheza kama mshambuliaji mkuu, lakini hataweza kuwa mtu sahihi kwa kikosi hiki.
Uwezo wake wa kurudi nyuma kuchukua mipira na kufunga mabao akiwa umbali mrefu kutoka kwenye goli la wapinzani unampa sifa ya kipekee, lakini vitu hivyo vinamfanya kuwa mchezaji bora zaidi kama atacheza No. 10 kuliko aina ya mshambuliaji ambaye Arsenal inahitaji kuwa naye msimu ujao.
Pamoja na ubora wake wote huo, Rooney haonekani kuwa mchezaji anayeweza kuingia kwenye mfumo wa Arsenal, licha ya kwamba ni mshambuliaji wa kweli.
Rooney si mtu wa kuhamahama, si mkokotaji mzuri wa mipira kwenye nafasi finyu na kwamba hata staili yake ya uchezaji haiwezi kuendana na soka la kumiliki mipira linalochezwa na wababe hao wa Emirates.
Amezoea kwenye mfumo wa pasi za haraka haraka kwenye kikosi cha Man United inapofanya mashambulizi, jambo ambalo ni tofauti kabisa na wanavyocheza Arsenal wanapokwenda kushambulia.
Na kwamba ni mchezaji mwenye hasira pindi mambo yanapokwenda kombo, hivyo itakuwa rahisi kukasirishwa na Arsenal pindi itakaposhindwa kuwasambaratisha wapinzani wao.
Nje ya uwanja, Rooney hana historia nzuri na mashabiki wa Arsenal, jambo ambalo litamfanya awe kwenye wakati mgumu wa kupata watu wa kumuunga mkono na hilo linamfanya awe na kazi ngumu ya kufanya kazi yake kwa ufasaha.
Rooney, ni kama kirusi, atahitaji kuwa 'baba lao' kwenye kikosi hicho, kitu ambacho kinaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa kwenye timu hiyo ya Arsene Wenger.
Tofauti na alivyokuwa Robin van Persie wakati alipokwenda kujiunga na United, Rooney hatahitaji kucheza kama mshambuliaji wa pili kwenye kikosi hicho cha Arsenal.
Licha ya kwamba alinyamaza kimya wakati alipokuwa akibadilishwa badilishwa namba na kocha Sir Alex Ferguson, jambo hilo hataweza kuendelea kulikubali kama ataendelea kufanyiwa na Wenger.
Na kama kuna mtu ambaye anadhani kwamba mwaka bora kabisa wa Rooney wa kucheza soka la juu bado haujafika, ifahamike pia kitu kama hicho hakiwezi kutokea kama atakwenda kujiunga na Arsenal.
Uhaba wa mataji unaoikabili Arsenal kwa sasa na hasa katika misimu kadha ya hivi karibuni nalo ni jambo ambalo haliwezi kumshawishi staa huyo wa United kuondoka kwenye timu inayonyakua mataji kila msimu na kwenda kujiunga kwenye ukame.
La, kama Arsenal itaendelea na mpango wake wa kuinasa saini ya fowadi huyo, itakachofanya ni kuingia gharama tu ya kulipa ada kubwa ya uhamisho na mshahara mkubwa kwa mchezaji ambaye hatawapa kitu wanachokitaka zaidi ya kusababisha mpasuko.
Rooney atahitaji awe baba lao kwenye kikosi hicho, kitu ambacho hakitaungwa mkono na wachezaji wengine, huku staili yake ya uchezaji pia kuwa ni tatizo litakalosababisha Wenger kubomoa mfumo wake wote kama atahitaji kumweka kwenye kikosi chake staa huyo.

No comments:

Post a Comment