Pages
▼
Sunday, June 2, 2013
CHEZEA BRAZIL WEWE!! THEO WALCOTT AWEKA MPIRA KWAPANI KWA WATOTO WA KIBRAZIL COPACABANA
RIO DE JANEIRO, Brazil
THEO Walcott akafanya matembezi kidogo na wenzake wa kikosi cha England wakati walipokwenda nchini Brazil kwa ajili ya ajili kucheza mechi ya kirafiki.
Staa huyo wa Arsenal na wenzake wa timu ya taifa ya England, Three Lions, wakajikuta wanaibukia kwenye ufukwe wa Copacabana na alichokiona huko hakuweza kuamini.
Mahali hapo, kwenye ufukwe huo - Walcott alijikuta macho yakimtoka, si kwa ajili ya mabinti warembo wa nchi hiyo waliokwenda kupunga upepo mahali hapo, la, bali ni jinsi watoto wa shule ya msingi, walivyokuwa wakionyesha ujuzi mkubwa wa kuchezea mpira na kuonyesha mbwembwe ambazo yeye Walcott hawezi hata kuiga.
Hapo Walcott aliweka mpira kwapani, maana hakuamini kama kile kilichokuwa kikifanyika kwenye ufukwe huo kinapaswa kufanywa na watoto hao.
Nyota huyo wa Arsenal, Walcott alikiri: “Tulikwenda kujivinjari kidogo ufukweni Alhamisi ile na kuwaona watoto wenye umri kati ya miaka sita au saba wakionyesha utaalamu mkubwa wa kuuchezea mpira, wakitumia mabega na vitu vingine wakati walipokuwa wakicheza ufukweni hapo.
“Mimi binafsi siwezi kufanya kile walichokuwa wakikifanya. Walionyesha ujuzi wa kuchezea mpira ambao wamekuwa nao mahali hapa.”
Wakati England ikianza kujiuliza namna nzuri ya kuboresha soka lao, safari hiyo ya Brazil ni wazi kabisa itakuwa imewafungua macho kwamba kuna watu wanaweza kuufanya mpira uwe sehemu ya viungo vyao.
Fowadi wa Tottenham Hotspur, Jermain Defoe, naye alibaki mdomo wazi kwa kandanda la vijana hao, anasema: “Niliwaona wasichana pia, wakifanya maajabu. Ni balaa. Lakini, nadhani unakwenda Brazil, unatarajia kuona vipaji vya aina hiyo.”
Walcott na Defoe walizungumza hayo Sport Relief, mradi unaoitwa Bola Pra Frente, uliopo jijini Rio de Janeiro, ambao unatoa mafunzo kwa watu wenye umri kati ya miaka sita hadi 24 kutoka katika jamii ya watu wasiojiweza.
Mradi huo ulianzishwa na Jorginho, mshindi wa Kombe la Dunia 1994, aliyekuwa na kikosi cha Brazil. Na staa mwingine wa nchi hiyo aliyekuwa kwenye tukio hilo ni Bebeto.
Ndani ya uwanja wa mazoezi kwenye kituo hicho, waliokuwa wakionekana watoto, ambao walikuwa hawana tatizo la kuuchezea mpira, wakiwa na furaha ya kumiliki mipira na walikuwa na ufahamu wa kutosha wa kufunga mabao. Kulikuwa na msichana mmoja pia alikuwa anapiga mashuti yenye kasi ya hatari.
Defoe akabaki na tabasamu lake na kumzungumzia binti huyo: “Nilikuwa namfikiria msichana yule. Hapana, anatisha, ningependa tuwe naye kwenye timu yetu na kutupigia mipira iliyokufa. Kuwatazama watoto hawa na ujuzi wao ni jambo linalotia raha.”
Defoe anasema kwamba watoto wa Brazil wanakuwa na ujuzi mkubwa wa kucheza mpira kwa sababu wamekuwa wakipelekwa shule wakiwa na umri mdogo.
Kitu kama hicho ndicho kinachopaswa kufanywa na nchi nyingine mbalimbali, hususani England, ambao wenyewe wanaamini ndio maskani ya mpira wa miguu.
Kitu hicho walichokutana nacho wachezaji wa England kwenye ziara yao hiyo ya Brazil kinawapa funzo, licha ya kwamba kwenye msafara wao wa ufukweni Copacabana, baadhi yao waliishia kutumbua macho kwa mabinti wenye mivuto ya ajabu waliokuwa wakipiga mbizi kwenye fukwe hizo.
England kwa sasa ipo nchini Brazil, ambako inakwenda kucheza mechi ya kirafiki itakayofanyika leo kwenye Uwanja wa Maracana. Mwakani, England ina matumaini itakwenda tena Brazil kucheza fainali za Kombe la Dunia.
Na sasa England inafikiria kuwa na DVD zenye ujuzi wa watoto hao ambapo itazigawa kwa wachezaji wake wote wa timu ya taifa ya England ili kuwapa hamasa.
No comments:
Post a Comment