Pages

Sunday, June 2, 2013

FEDHA ZIMEMPOTEZA RADAMEL FALCAO?


PARIS, Ufaransa
RADAMEL Falcao bila shaka ni fowadi namba tatu kwa ubora duniani kwa sasa, ukiwaondoa Cristiano Ronaldo na Lionel Messi. Amewindwa na klabu kubwa barani Ulaya na umri wake wa miaka 27, ndicho kipindi kizuri cha kutamba katika maisha ya soka lake.
Vigogo kadha barani Ulaya, ikiwamo matajiri wa London, Chelsea walikuwa wakihitaji saini yake. Lakini, yeye amejiunga na mabingwa wa Ligue 2, AS Monaco.
Shabiki wa kweli wa mambo ya soka, jambo hilo litamshangaza, lakini kwa mpira wa kisasa uliojaa fedha - kuna atakayeshangazwa hapa?
Ni wazi kabisa fowadi huyo wa zamani wa Atletico Madrid hakutaka kukaa njia panda. Kiwango chake cha soka alichonacho sasa ni kazi yake mwenyewe; ikiwa ni matunda ya kipaji chake na kujituma.
Anastahili kwa mafanikio yake. Anastahili pia kwa utajiri wake (hasa ukizingatia kwamba mchezaji yeyote mwenye kiwango kikubwa anastahili kuwa tajiri kwa kiwango chake hasa katika soka la kisasa).
Beki wa Tottenham Hotspur, Benoit Assou-Ekotto alitoa kauli yenye maana kubwa sana kwenye soka, kwamba majeraha yanaweza kuharibu maisha yako ya soka muda wowote - hivyo basi kwa jambo hilo mchezaji yeyote profesheno atahitaji kutumia kipindi hicho kilichopo kutengeneza fedha nyingi kwa kadri awezavyo.
Akiwa tayari, Falcao ameshapata malipo mazuri ya kazi yake nzuri, ikiwamo uhodari wa kutumbukiza mipira nyavuni, tena kwa uhakika, mchezaji huyo amekusanya fedha nyingi katika maisha yake ya kisoka katika miaka yake nane ya soka la kulipwa kutoka Argentina hadi Hispania akipitia Ureno.
Uhamisho uliotarajiwa baada ya hapo, ni wazi ulikuwa ni wa fedha nyingi. Tazama, Chelsea walikuwa wapo tayari kununua mkataba wa Mcolombia huyo, ambao ulikuwa na thamani ya euro milioni 60 ili tu aende Stamford Bridge na hapo angekwenda kulamba mshahara mnono.
Pamoja na kwamba fedha ndicho kitu kingemshawishi kwenda Chelsea, lakini bado angekuwa na watu ambao wangeunga mkono uhamisho wake kwamba umezingatia soka kwa sababu hapo angepata nafasi ya kutwaa taji la Ligi Kuu England au Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Kutokana na wababe hao wa London kutwaa taji hilo la ubingwa wa Ulaya msimu uliopita, wengi wangeamini kwamba uhamisho wake haukushinikizwa na mambo ya fedha.
Lakini, sasa kuna swali zito hapa - badala yake Falcao ameamua kwenda Monaco, uhamisho ambao unaaminika kwa asilimia kubwa kama si zote umetokana na tamaa ya fedha na si soka.
Kuna jambo gumu hapa kutaka kukubali kwamba uhamisho huo haukusukumwa na mpango wa mshahara wa euro milioni 14 kwa mwaka?
Kwenye hilo, kuna tofauti yoyote na ule uhamisho uliomhusisha mshambuliaji Samuel Eto’o, wakati alipokubali kufuata mshahara mnono Anzhi Makhachkala miaka miwili iliyopita?
Walau kidogo, kwa kesi ya Eto’o analo la kujitetea, kwa sababu mahali hapo ameweza kutwaa ubingwa wa ligi. Na pia fowadi huyo Mcameroon alikwenda Urusi akiwa tayari ametwaa mataji matatu ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya; Falcao yeye ametwaa mataji ya Europa League.
Falcao alisaini mkataba na wakala maarufu wa Ureno, Jorge Mendes mwaka 2011, wengi waliamini kwamba alikuwa anakwenda Madrid. Lakini, badala yake alikwenda Atletico na si Real Madrid.
Klabu hizo mbili zina uhasama kwa maana hakuna upande wowote unaweza kusajili mchezaji wa upande mwingine.
Jambo kama hilo ndilo lililomzuia Sergio Aguero kuvuka mtaa na kujiunga na Madrid, hivyo isingeweza kutokea pia kwa Falcao kujiunga na kikosi cha Madrid.
Mendes, ambaye mteja wake huyo alidaiwa kuweka kibindoni karibu euro milioni 40 kama ada yake ya usajili wakati alipotua Atletico mwaka 2011, anahusika pia na kocha Jose Mourinho, Cristiano Ronaldo, Pepe, Ricardo Carvalho na Angel Di Maria, ambao amekuwa akiwasimamia.
Na kumekuwa na uvumi kwamba Mreno huyo ameweka kipengele kwenye mkataba wa Falcao unaoruhusu Monaco kumuuza mchezaji huyo los Blancos.
Alipokuwa mtoto, Falcao alibainisha ndoto zake ilikuwa ni kuichezea Real Madrid, matakwa ambayo yalisisitizwa na baba yake mwaka jana.
Na sasa amekwenda Ufaransa, mahali ambapo atakuwa anavuna euro milioni 14 kwa mwaka. Na jambo hilo litamfanya kwa msimu wa nne mfululizo hatakuwamo kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Lakini, uhamisho huo pia wa kwenda Monaco kwa kiasi kikubwa unaporomosha sifa za mchezaji huyo.
Kutokana na tayari Paris Saint-Germain, wakionekana kuweka utawala wake kwa miaka ya hivi karibuni, hilo litawachukua miaka miwili hadi mitatu kwa Monaco kuweza kujipanga na kuingia kwenye orodha ya timu kubwa.
Na kitakapofika kipindi hicho, tayari Falcao atakuwa anasogelea miaka 30 na hapo soka litakuwa linamtupa mkono, hivyo tayari atakuwa hana nafasi tena ya kupata fursa ya kucheza kwenye klabu zinazoshiriki ligi za juu.
Katika suala la kimichezo, hilo ni pigo kubwa. Hapa unamzungumzia mchezaji, ambaye yeye peke yake aliweza kuisambaratisha Chelsea katika mechi ya Super Cup.
Ni mchezaji huyo, ambaye alifunga bao maridadi kabisa katika Uwanja wa Camp Nou, ambalo liliwaacha mashabiki vinywa wazi na kummwagia sifa fowadi huyo.
Ni mchezaji anayestahili kucheza kwenye Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na kukosekana kwake kunapunguza ladha kwa namna fulani kwenye michuano hiyo.
Kwa jambo hilo, hii ni huzuni kubwa kwa kushuhudia kipaji hicho kikishindwa kung'ara kwenye soka la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya na kutimkia Monaco, mahali ambapo fedha ndicho kitu kilichofanya uhamisho huo kutokea.

No comments:

Post a Comment