Pages

Sunday, June 2, 2013

MOURINHO ATALETA FOMESHENI GANI CHELSEA MSIMU UJAO?


LONDON, England
JOSE Mourinho amehitimisha mjadala, amemaliza utata uliokuwa wa mshangao mkubwa, baada ya kurejea rasmi Chelsea, akitokea Real Madrid. Ameibua tumaini jipya Stamford Bridge, kutokana na mashabiki kulipata chaguo lao la kwanza na ni mmoja wa makocha wenye historia ya kipekee kwenye vyombo vya habari kwa miaka ya hivi karibuni.
Ni kocha aliyepata umaarufu mkubwa, mwenye ujuzi wa kiutawala, lakini ni kitu gani kipya Mourinho atakileta kwenye klabu hiyo kinachohusu suala la kiufundi?
Ikifahamika kwamba atakwenda kufanya kazi chini ya bilionea Roman Abramovich kwa mara nyingine, atakuwa na kibarua chenye utata mkubwa kwenye soka hilo la sasa.
Ndani ya Chelsea, Mourinho atakuwa na kikosi chenye vijana wengi wenye vipaji na njaa ya mafanikio, akiwa chaguo la mashabiki na timu hiyo ikiwa imefuzu kucheza mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao.
Baada ya timu hiyo kumaliza msimu ikiwa kwenye kiwango bora kabisa chini ya kocha Rafa Benitez, licha ya kukumbwa na misukosuko mingi, je, ni vitu gani muhimu vya kiufundi kocha huyo mpya atavifanya katika kikosi hicho cha Stamford Bridge?
Mfumo kwenye karatasi unaweza kuonekana kuwa unafanana. Mou alikuwa akitumia fomesheni ya 4-2-3-1 alipokuwa na kikosi cha Internazionale na Real Madrid, kutokana na kupendelea mtindo huo.
Benitez alimtumia 4-2-3-1 kwa kiasi kikubwa katika mechi za msimu uliopita, hivyo wachezaji wote kwenye kikosi cha Chelsea wamezoea mfumo huo.
Jambo hili litamfanya kocha mpya atakayejiunga na timu hiyo kuwa na kazi rahisi tu ya kimfumo kama atataka kuendelea na jambo hilo, huku tatizo litakalotokea kama tu ataamua kuja na mifumo iliyo tofauti.
Swali kubwa lililopo hapa ni je, ni mshambuliaji gani wa kati ambaye Mourinho atahitaji kuwa naye katika kikosi hicho cha Chelsea. Mara ya kwanza alipokwenda 'darajani', alikuwa na Didier Drogba, na alipohama hapo aliweza kuwa na Diego Milito kwenye kikosi cha Inter na Cristiano Ronaldo kwenye timu ya Madrid.
Kulikuwa na ripoti kwenye gazeti la The Mirror kwamba ripota wao, Matt Law aliandika kwamba Chelsea imeitaka Manchester United kutaja bei ya Wayne Rooney, na kama hilo likifanikiwa, fowadi huyo atakuwa mtu ambaye Mourinho atamweka kwenye kikosi chake.
Wakishindwa kufanya usajili huo, Mou bado atakuwa na watu mahiri kwenye kikosi chake kama Eden Hazard, ambaye kwa sasa tayari atakuwa amepata uzoefu mkubwa kuhusu mikikimikiki ya Ligi Kuu England.
Ni mchezaji mwenye kasi ya aina yake na uwezo mkubwa wa kubadilisha matokeo—kupiga mashuti kutoka umbali mrefu, kupiga chenga hata wachezaji watatu na kupiga pasi hatari za mwisho.
Juan Mata naye amekuwa mchezaji muhimu na mwokozi kwa kikosi cha Chelsea kwa misimu kadha na uchezaji wake unaifanya timu hiyo kuwa na mtu sahihi kwenye No. 10 na uchezaji wake unaweza kumsaidia Hazard kuwa ndani ya wachezaji nane bora duniani kwa msimu ujao.
Mourinho amekuwa akipenda kiungo ambaye anaweza kukimbia na mipira katikati uwanja na kwenye hilo, David Luiz anaweza kupata nafasi ya kutosha ya kucheza kati ya uwanja.
Frank Lampard nafasi yake kwenye timu ndiyo inayovutia zaidi, atapangwa kulingana na wapinzani. Cesar Azpilicueta ni beki wa kulia, ambaye Mou angependa kuwa naye kwenye kikosi cha Madrid, hivyo kutua Chelsea na kukutana na mchezaji huyo ni jambo bora kwake, huku akiwa hana shaka juu ya beki ya kushoto.
Hiki ni kipindi cha maswali mengi kuhusu Chelsea, lakini swali la kwanza ambalo litahitaji majibu: Mourinho atakuwa kocha, je, ni fomesheni gani ataitumia msimu ujao?

No comments:

Post a Comment