Pages

Wednesday, May 15, 2013

STRAIKA WA APR AWATULIZA YANGA


WAKATI imeripotiwa kuwa mshambuliaji hatari wa timu ya APR, Jean Cloud Irangi huenda akawemo katika kikosi cha Yanga msimu ujao, mchezaji huyo amewataka mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara wasikurupuke katika kufanya usajili wake.

Akizungumza na Lenzi ya michezo kwa njia ya simu, Iranzi alisema atakuwa tayari kuchezea timu yoyote iwe Yanga, Simba au hata Azam FC, kama tu itaweza kufikia makubaliano na klabu yake ya APR, ambayo amedumu nayo kwa miaka mitano sasa.

Alisema kinachotakiwa ni viongozi wa timu zitakazohitaji saini yake, kuketi na uongozi wa APR na kufikia makubaliano kwa vile anatambua umuhimu wa kuondoka kwenye klabu hiyo akiwa na ridhaa ya viongozi wake.

“Unajua huku ni nyumbani inanipasa niondoke nikiwa na ridhaa ya ‘wazazi’ (APR),” alisema.
Hivi karibuni klabu za Simba na Yanga kwa nyakati tofauti vimeeleza kuelekeza macho yao katika klabu ya APR kwa ajili ya kumng’oa mshambuliaji huyo chipukizi wa timu hiyo.

Mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa ametimiza miaka 20, aliwahi kuichezea timu ya watoto ya Kiyovu kabla ya kujiunga na timu ya wakubwa kuanzia mwaka 2004 hadi 2008, kisha kujiunga na APR mwaka uliofuata, mahali ambapo anaendelea kucheza hadi sasa.

No comments:

Post a Comment