Pages

Wednesday, May 15, 2013

WAYNE ROONEY KWENDA ARSENAL NI DILI AU SIO DILI?



LONDON, England
SWALI gumu kwasasa ni kwamba ipi itakuwa klabu mpya ya Wayne Rooney? Hili ni swali ambalo linasubiri muda ufike kuweza kufahamika. Bayern Munich, Chelsea na Paris Saint Germain zinatajwa kuwania saini ya staa huyo wa Three Lions.
Habari za kwamba Rooney anasubiria kuihama Manchester United mwishoni mwa msimu huu, jambo ambalo anaripotiwa kulieleza mwenyewe kwamba anataka kuondoka Old Trafford.
Lakini, wakati Rooney akibainisha dhamira yake ya kutaka kuhama Man United, wapi atakwenda staa huyo, ambaye suala la kuondoka si jambo lenye uvumi tena kutokana na kocha anayeachia ngazi, Sir Alex Ferguson kuweka bayana kwamba mchezaji huyo anasisitiza kuondoka Old Trafford.
Ukweli ni kwamba, kama dhamira yake hataki kubaki Man United tena, wazi kabisa kutakuwa na klabu lukuki ambazo zitafukuzia saini yake.
Goal.com limedai kwamba, kwa klabu za Ligi Kuu England, Arsenal na Chelsea zinatarajia kuingia kwenye vita kali ya kumnasa Rooney mwishoni mwa msimu huu.
Lakini, je, kwa klabu hizo mbili, Chelsea na Arsenal kuna timu yoyote inaweza kuwa na ushawishi wa kumng'oa Rooney, 27, Old Trafford?
Akiwa katika umri huo, Wayne alipaswa kuwa katika kiwango bora kabisa cha soka lake. Lakini, badala yake msimu huu fowadi huyo alikuwa hatua nyingi sana mbali kufikia kwenye ubora wake.
Pamoja na kwamba haukuwa mwaka mbaya sana kwake, maendeleo ya fowadi huyo yanaonekana kukwaa kisiki kidogo na pengine jambo hilo ndilo linalomsukuma kuondoka Old Trafford ili akakumbane na changamoto mpya.
Kwenye hilo, huo utakuwa uamuzi sahihi kuliko kuendelea kubaki kwenye kikosi cha United, mahali ambapo kwa mwaka huu amejikuta akiwekwa benchi katika mechi kubwa na nafasi yake kuporwa na wachezaji mahiri kama Robin Van Persie.
Na kutokana na hilo, kama atahamia kwenye klabu kama Arsenal au Chelsea, mahali hapo ataweza kupokelewa kama mfalme.
Kwa kuweka kando mabaya yote ya Rooney, fowadi huyo amefunga mabao 16 katika mechi 36 alizocheza msimu huu, kiwango ambacho si kibaya sana kwa kukitazama kiundani.
Jambo hilo linaweka kando soka lake la kujitolea, nafasi za mabao anazotengeneza na mashambulizi anayoyaanzisha pindi anapochezeshwa kutoka katika sehemu ya katikati ya uwanja. Hivyo, habari za kwamba Rooney kiwango chake kimeporomoka zimekuwa zikikuzwa tu.
Kinachotarajiwa ni kwamba, Chelsea inafukuzia kusaini mshambuliaji wa kutoka ng'ambo (Radamel Falcao au Edinson Cavani). Arsenal, kwa upande wao hao, ni wazi kabisa wanahitaji fowadi mwenye kiwango kama cha Rooney.
Isingekuwa jambo la ajabu kama Arsenal ingekubali biashara ya kuwabadilisha Van Persie na Rooney, kwasababu jambo hilo lingeifanya Gunners kuwa na mchezaji ambaye umri wake ni mdogo kwa miaka miwili ukilinganisha na RVP, lakini wote wakiwa katika viwango bora za kucheza kiushindi.
Kama Rooney atatua kwenye kikosi cha Arsenal, jambo hilo huenda likamfanya kocha Arsene Wenger walau arudishe imani kutoka kwa mashabiki wake ambao mara kadha wamekuwa wakimlaumu kutokana na kushindwa kufanya usajili mkubwa.
Hakutakuwa na neno linalohusu gharama hapa kama Arsenal itamnunua Rooney, hasa ukweli uliopo ni kwamba, Moyes hatahitaji kuendelea kumbakiza kwenye kikosi chake mchezaji ambaye hana furaha ya kuendelea kuichezea timu yake.
Arsenal, pia kama wanahitaji kuwa kivutio cha kupata makampuni makubwa ya udhamini, wanapaswa kusajili wachezaji wenye kaziba kama ya Rooney kwenye kikosi chao. Huu ni ukweli usioshaka, Arsenal inapaswa kuingia sokoni na kumsajili Rooney kwa kipindi hiki.
Alivyo Rooney ni kwamba, anataka kucheza mahali ambapo atakuwa anasujudiwa kitu ambacho kwenye kikosi cha Man United kimeshindikana na ndio maana anaomba kuondoka. Arsenal ndipo mahali panapomfaa hasa ukizingatia aina ya wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho.

REKODI ZA ROONEY MAN UNITED
2004-05
Mabao: 14
Mechi: 35
Wastani wa bao kwa mechi: 0.40

2005-06
Mabao: 17
Mechi: 41
Wastani wa bao kwa mechi: 0.414

2006-07
Mabao: 18
Mechi: 47
Wastani wa bao kwa mechi: 0.38

2007-08
Mabao: 16
Mechi: 38
Wastani wa bao kwa mechi: 0.42

2008-09
Mabao: 16
Mechi: 43
Wastani wa bao kwa mechi: 0.37

2009-10
Mabao: 31
Mechi: 39
Wastani wa bao kwa mechi: 0.79

2010-11
Mabao: 16
Mechi: 37
Wastani wa bao kwa mechi: 0.43

2011-12
Mabao: 31
Mechi: 38
Wastani wa bao kwa mechi: 0.82

2012-13 (LIGI KUU PEKEE)
Dakika alizocheza: 2,126
Mechi alicheza (sub): 22 (5)
Mabao (Penalti): 12 (1)
Mashuti golini: 50
Usahihi mashuti: 65%
Pasi zilizofanikiwa: 960
Pasi butu: 212
Ubora wa pasi: 82%

No comments:

Post a Comment