Pages

Wednesday, May 15, 2013

KIEMBA ANAYENITAKA AJE TUZUNGUMZE



KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Amri Kiemba, amesema yupo tayari kupokea ofa ya timu yoyote ikiwamo Yanga kama tu itamfuata na ofa nono, ili kuipata huduma yake msimu ujao.

Kiungo huyo, Kiemba, aliyewahi kuichezea Yanga, ambaye kwa sasa anamaliza mkataba wake katika klabu ya Simba, alisema hawezi kuchagua timu ya kuchezea na anachosubiri ni kupata ofa nono hilo ndilo analohitaji.

Kiemba amesema kwamba, kwanza ataanza kwa kuwafuata viongozi wa klabu yake ya Simba kujadili juu ya mkataba mpya, kama watasuasua kumpatia dau analohitaji basi ataangalia ofa nyingine zitakazoletwa mezani kwake.

"Bado sijazungumza na Simba juu ya mkataba mpya. Msimu utakapomalizika, nitawafuata viongozi na kutaka kutambua hatima yangu, nitatazama kama watakuwa wameniandalia ofa nzuri," alisema.

"Ninachokiangalia mimi ni maslahi, kama Simba hawatakuwa na ofa nzuri na kisha klabu yoyote ikaja na ofa yake nzuri, nitakuwa tayari kujiunga nao. Milango kwangu ipo wazi, kikubwa ni maslahi tu."

Kiungo huyo wa kimataifa wa Tanzania, anamaliza mkataba wake mwishoni mwa msimu huu na Jumamosi hii anatarajia kuwamo kwenye kikosi cha Simba kitakachomenyana na Yanga katika mchezo wa funga dimba wa Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo wa kwanza uliozikutanisha timu hizo msimu huu, uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, Kiemba ndiye aliyeifungia bao la kuongoza Simba kabla ya Yanga kusawazisha kwa mkwaju wa penalti kupitia Said Bahanuzi.

No comments:

Post a Comment