Pages

Monday, May 13, 2013

SIMBA YAITEKA YANGA ZANZIBAR



SIMBA imeifuata Yanga Zanzibar, iliyoweka kambi katika kisiwa cha Pemba, ikijiandaa na mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga iliondoka wiki iliyopita ikiwa na kikosi cha wachezaji 24, Simba waliondoka jana na boti ya saa tisa Alasiri jijini Dar es Salaam kwenda Unguja, Zanzibar.

Simba iliondoka na wachezaji 25 waliosajiliwa na klabu hiyo huku wengi wao wakiwa chipukizi ambao wanatarajia kucheza dhidi ya Yanga.
Wekundu hao wa Msimbazi wamekuwa na utamaduni wao uliozoeleka wa kwenda kuweka kambi kisiwa cha Unguja, huku ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Kiislamu wa Chukwani ulioko nje kidogo ya Mji wa Zanzibar.

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Oktoba mwaka jana, Simba ilitokea visiwani humo, ambapo Yanga ilikuwa Kiromo Bagamoyo, ambao walitoka sare ya bao 1-1.
Akizungumza na jana, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ alisema imekuwa ni kawaida kwa Simba kwenda kuweka kambi visiwani huo.

Julio alisema wachezaji wote ambao wanatarajia kucheza mchezo huo, wamekwenda kujiandaa na mechi hiyo, ambayo kwao ni muhimu kushinda ili waweze kujenga heshima baada ya kupoteza ubingwa.
Alisema atahakikisha wanatibua sherehe za ubingwa wa Yanga, kwani ana amini ataifunga kutokana na kikosi chake kuwa ni bora kuliko wao. 

Julio alisema pamoja na Yanga kwenda Pemba kujiandaa na mechi hiyo kipigo kitakuwa palepale kutokana na timu yake inaundwa na vijana wengi.
“Yanga hawanipi presha kabisa, kwani ninacho kikosi bora kinachoundwa na vijana wanaojua majukumu yao wanapokuwa uwanjani, mbivu na mbichi zitajulikana Jumamosi,” alisema Julio.

Julio alisema anachoomba mashabiki wajitokeze kwa wingi ili waweze kuona jinsi gani watakavyoweza kuifunga na kutibua ubingwa wa timu hiyo.
Alisema wataongeza machungu mengine baada ya kuchapwa mabao 5-0, katika msimu uliopita, ambao walishindwa kulipa kisasi katika mchezo wa kwanza uliochezwa Oktoba 29, mwaka jana.

Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, yaliyofunga na Amri Kiemba kwa upande wa Simba na Said Bahanunzi kwa Yanga.

No comments:

Post a Comment