SIMBA imeifuata Yanga Zanzibar, iliyoweka kambi katika
kisiwa cha Pemba, ikijiandaa na mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara, itakayochezwa
Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga iliondoka wiki iliyopita ikiwa na kikosi cha wachezaji
24, Simba waliondoka jana na boti ya saa tisa Alasiri jijini Dar es Salaam
kwenda Unguja, Zanzibar.
Simba iliondoka na wachezaji 25 waliosajiliwa na klabu hiyo
huku wengi wao wakiwa chipukizi ambao wanatarajia kucheza dhidi ya Yanga.
Wekundu hao wa Msimbazi wamekuwa na utamaduni wao
uliozoeleka wa kwenda kuweka kambi kisiwa cha Unguja, huku ikifanya mazoezi
kwenye Uwanja wa Chuo cha Kiislamu wa Chukwani ulioko nje kidogo ya Mji wa
Zanzibar.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Oktoba mwaka jana, Simba
ilitokea visiwani humo, ambapo Yanga ilikuwa Kiromo Bagamoyo, ambao walitoka
sare ya bao 1-1.
Akizungumza na jana, Kocha Msaidizi wa timu hiyo,
Jamhuri Kihwelu ‘Julio’ alisema imekuwa ni kawaida kwa Simba kwenda kuweka
kambi visiwani huo.
Julio alisema wachezaji wote ambao wanatarajia kucheza
mchezo huo, wamekwenda kujiandaa na mechi hiyo, ambayo kwao ni muhimu kushinda
ili waweze kujenga heshima baada ya kupoteza ubingwa.
Alisema atahakikisha wanatibua sherehe za ubingwa wa Yanga,
kwani ana amini ataifunga kutokana na kikosi chake kuwa ni bora kuliko wao.
Julio alisema pamoja na Yanga kwenda Pemba kujiandaa na mechi
hiyo kipigo kitakuwa palepale kutokana na timu yake inaundwa na vijana wengi.
“Yanga hawanipi presha kabisa, kwani ninacho kikosi bora
kinachoundwa na vijana wanaojua majukumu yao wanapokuwa uwanjani, mbivu na
mbichi zitajulikana Jumamosi,” alisema Julio.
Julio alisema anachoomba mashabiki wajitokeze kwa wingi ili
waweze kuona jinsi gani watakavyoweza kuifunga na kutibua ubingwa wa timu hiyo.
Alisema wataongeza machungu mengine baada ya kuchapwa mabao
5-0, katika msimu uliopita, ambao walishindwa kulipa kisasi katika mchezo wa
kwanza uliochezwa Oktoba 29, mwaka jana.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, timu
hizo zilitoka sare ya bao 1-1, yaliyofunga na Amri Kiemba kwa upande wa Simba
na Said Bahanunzi kwa Yanga.
No comments:
Post a Comment