Pages

Wednesday, May 29, 2013

MOURINHO KUTUA NA KAMANDA WAKE CHELSEA


LONDON, England
JOSE Mourinho anatarajia kuandamana na msaidizi wake, Rui Faria, wakati atakaporejea kuchukua mikoba ya kuinoa Chelsea msimu ujao.

Wawili hao, Mourinho na Faria, walionekana wakiwa pamoja kwenye Uwanja wa Wembley juzi, wakati walipokwenda kushuhudia mechi ya mchujo ya kuwania kupanda Ligi Kuu England, iliyozikutanisha timu za Crystal Palace na Watford.

Kocha Faria, 37, naye atatangaza kung'oka Real Madrid wiki ijayo kuandamana na Mourinho kwenda dimba la Stamford Bridge.
Mourinho na Faria wamekuwa ni watu wasiotenganishwa na wamekuwa pamoja tangu walipokuwa katika klabu ya Leiria ya Ureno mwaka 2001, kipindi hicho Faria alikuwa kocha wa viungo.

Na tangu hapo, Faria amekuwa mtu mwaminifu kwa Mourinho na kuwa kama kamanda wake katika vita mbalimbali anazopigana, huku wakiwahi kuwa pamoja katika kikosi cha Chelsea kilichotwaa ubingwa wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo katika miaka ya 2005 na 2006, huku pia wakinyakua mataji mawili ya Kombe la Ligi na taji moja la FA.

Wawili hao walitwaa taji la Ligi ya Mabingwa wakiwa na kikosi cha FC Porto na Inter Milan na mataji ya ligi katika nchi za Hispania, Italia na Ureno. Mwaka 2010 Inter ilitwaa mataji matatu, Serie A, Coppa Italia na Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Na Faria ataendelea kuwa kocha msaidizi wa Chelsea wakati atakapoungana na Mourinho kwenye klabu hiyo ambayo waliihama miaka sita iliyopita.

No comments:

Post a Comment