Pages

Wednesday, May 29, 2013

MADRID IMEUA PENZI LA MRENO SASA INATAKA LA MUITALIANO


MADRID, Hispania
WAKATI penzi linapofika mwisho, ni kawaida kwa mwanaume na mwanamke kusaka mpenzi mpya ambaye ana vigezo vyenye ubora kuliko yule aliyetangulia na kisha kuanzisha naye pendo.
Jambo hili linafanana na kisha kinachotokea Real Madrid kwa sasa; ambapo kutengana na Jose Mourinho kunafungua njia ya kusaka kocha mwingine, ambaye atakuwa na vitu tofauti; ambaye wao wanaona anayefaa ni Carlo Ancelotti.
Madrid ilitangaza Jumatatu iliyopita kwamba, Mourinho ataondoka mwisho wa msimu huu, baada ya misimu yake mitatu aliyodumu na klabu hiyo ya Santiago Bernabeu, wakati huo huo huko Paris, Ancelotti akiingia kwenye mazungumzo ya kutaka kung'oka Paris Saint-Germain.
Pamoja na kwamba klabu hiyo ya Ufaransa inaiwekea ngumu, matakwa ya Muitaliano huyo ni kujiunga na Madrid, kitu ambacho anaweza kukiwekea msukumo kiweze kutoka ndani ya siku chache zijazo.
Rais wa Real Madrid, Florentino Perez kwa muda mrefu amekuwa akimhusudu Ancelotti na alikuwa na mpango wa kumpa ajira bosi huyo wakati aliporejea kwa mara ya pili kuiongoza Los Blancos mwaka 2009.
Kipindi kile, Carlo aliamua kuchagua kujiunga na Chelsea baada ya kudumu kwa miaka saba na nusu katika kikosi cha AC Milan. Miaka minne baadaye, Florentino anakaribia kumpata mtu wake na anaonekana kuwa mtu sahihi kurithi mikoba ya Mourinho.
Faida kubwa ya bosi huyo wa PSG ni kwamba, mtu anayekwenda kurithi mikoba yake, Mreno Mourinho si mtu aliyefikia mafanikio makubwa sana kuliko yeye, hivyo ni jambo ambalo ataweza kumbadili bila shaka.
Baada ya kipigo chenye machungu kwenye el Clasico, Januari mwaka jana, beki Sergio Ramos alimjibu kocha Mourinho ambaye alimkosoa licha ya kumpa Pepe kazi ya kuzuia mipira iliyokufa na kumwambia Mreno huyo: "Hujui kitu kwasababu wewe hujawahi kucheza soka kwenye kiwango kama hiki."
Ancelotti yeye alikuwa kiungo fundi mkubwa, ambaye ametwaa mara mbili mataji ya Ulaya katika kikosi cha AC Milan mwishoni mwa miaka ya themanini na mwanzoni mwa tisini, alipokuwa akicheza sambamba na wakali Franco Baresi, Paolo Maldini, Ruud Gullit na Marco van Basten.
Kipindi chake alichokuwa mchezaji, alipata bahati ya kuwa chini ya makocha bora kabisa kama Arrigo Sacchi na Fabio Capello alipokuwa Milan, Nils Liedholm na Sven-Goran Eriksson, alipokuwa AS Roma na mshindi wa Kombe la Dunia, Enzo Bearzot, aliyekuwa akiinoa Italia.
Kwa kipindi hicho, Serie A ilikuwa ikitambulika kama ligi yenye nguvu zaidi katika suala la kitekniki, eneo ambalo Mourinho alijaribu kulitambua kwa misimu yake mitatu aliyokuwa nchini Hispania.
Wakati Mreno huyo akicheza soka la mashambulizi ya kushtukiza, huku akiwa na wachezaji bora kabisa kwenye kikosi chake, Ancelotti amekuwa akitumia mifumo na staili tofauti za uchezaji katika miaka yake ya ukocha na kwamba kutua kwake Santiago Bernabeu kunaweza kuboresha zaidi kwa upande wa kiufundi.
Fomesheni yake aliyokuwa akiipendelea zaidi Milan ilikuwa 4-3-2-1, ambayo iligeuka na kuwa 4-4-2 (Diamond) wakati alipokwenda Chelsea. Kumekuwa na mifano kwenye mifumo yake, ambapo amekuwa akimpanga mtu nyuma ya mshambuliaji wa kati, kiungo mchezeshaji au trequartista: Kama alivyokuwa akimtumia Zinedine Zidane pale Juventus na Kaka alipokuwa Milan.
Kwenye kikosi cha Madrid, wachezaji Mesut Ozil au Luka Modric anaweza kuwatumia kwenye mfumo huo. Lakini, pia yeyote atakayemchagua, Ancelotti ufundi wake kwenye kukochi siku zote amekuwa wenye kulenga ubora kama ilivyokuwa katika miaka ya themanini, tisini na 2000, ambapo hakuna soka la kucheza kwa kujihami kama anavyofanya Mourinho.
Ancelotti anaweza kuwa ametwaa mataji machache kuliko Mourinho kwenye maisha yake ya ukocha, lakini Mourinho mwaka jana aliyejipachika jina la 'The Only One', bosi wa zamani wa Milan, akitua Hispania anaweza kutwaa taji la nne la ligi katika nchi tofauti, baada ya kubeba ubingwa nchini Italia, England na Ufaransa.
Ancelotti, akiwa mshindi mara mbili wa taji la Ulaya akiwa kama mchezaji, alitwaa taji la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kama kocha (sawa na Mourinho), aliongoza Milan kutwaa ubingwa 2003 na 2007 (akiifikisha Rossoneri fainali pia ya mwaka 2005, ambayo Liverpool walionyesha maajabu kwa kutokea nyuma kwa mabao matatu na kushinda jijini Istanbul).
Lakini, yeye ni tofauti na Mourinho, ambaye siku zote amekuwa na mambo yenye utata. Ancelotti yeye watu wanamwelezea kama 'mpatanishi' kutokana na kuwa na uwezo wa kutuliza hali ya mambo inapoonekana kuna tatizo.
Ancelotti, 53, aliweza kutengeneza uhusiano wa kipekee na Silvio Berlusconi, ulizingatia zaidi kwenye kazi, licha ya bosi huyo aliyekuwa na nguvu kubwa nchini Italia mara kadha kumkosoa mara kwa mara, huku akiweza pia kuwa chini ya Roman Abramovich, bilionea mwenye utata kubwa pale Chelsea, anayeweza kubadilika muda wowote ule.
Ancelotti pia amewahi kuwanoa wachezaji mahiri kabisa hapa duniani kwa zaidi ya miaka 15, akiwamo Zidane (ambaye atafanya naye kazi Madrid), na yeye alivyo hilo linamfanya watu wamtambue kama Vicente del Bosque wa Italia, kutokana na staili yake ya uongozi ilivyo.
Na kwenye suala la makocha wachache wenye viwango vikubwa, Ancelotti anaonekana kuwa mtu sahihi wa kuziba pengo litakaloachwa na Mourinho.
Licha ya kwamba kuna wakufunzi wengine wenye uwezo mkubwa kama Jurgen Klopp, Jupp Heynckes, Joachim Low na Andre Villas-Boas, bosi huyo Muitaliano, anaonekana kuwa chaguo la kwanza la rais Perez, ambaye alikosa huduma yake mwaka 2009. Ndoa na Mourinho imefika mwisho na Madrid wanaamini kwamba, wamempata mtu mwingine wa kuchukua nafasi yake.

No comments:

Post a Comment