Pages

Wednesday, May 29, 2013

LEWANDOWSKI KUFAHAMU HATIMA YAKE HIVI PENDE


MUNICH, Ujerumani
KOCHA Mkuu wa Borussia Dortmund, Jurgen Klopp, amesema kwamba hajapokea ofa yoyote rasmi kutoka Bayern Munich inayomhusu straika wake, Robert Lewandowski na kudai hatima ya mchezaji huyo itafahamika hivi punde.

Mmoja wa mawakala wa mchezaji huyo, Lewandowski, 24, Cezary Kucharski, alidai kwamba staa huyo wa kimataifa wa Poland atahama BVB na kutimkia Bayern mwishoni mwa msimu huu.
Lakini, wakala mwingine wa mchezaji huyo, Maik Barthel, awali alibainisha kwamba mshambuliaji huyo ameshakubaliana na dili la kujiunga na timu nyingine, ambayo si Bayern.

Na sasa Klopp ameweka utata kando na kudai kwamba hadi sasa hajapokea ofa yoyote au kufanya dili lolote na Bayern juu ya hatima ya fowadi huyo.
"Hatujapokea ofa yoyote rasmi kutoka Bayern Munich, hivyo bado natarajia kwamba Robert ataendelea kuichezea Dortmund msimu ujao," alisema Klopp, alipozungumza na Bild.

"Tutafanya kila tunaloweza kuhakikisha kwamba uvumi huu wote unaozagaa unakwisha ndani ya siku chache zijazo. Sitakuwa na hasira naye kwa chochote kitakachotokea. Nasubiria haya ni mambo ya kiprofesheno. Tutaona kitu gani kitatokea. Chochote kinawezekana.

"Kitu kinachochekesha ni kwamba kila mtu anachukulia kama dili hilo limeshakamilika. Jupp Heynckes alisema hivyo, mawakala wake wamesema pia, sisi hatujapata ofa rasmi... sasa ukweli upo wapi? Bila kujali nini kitatokea, lakini ukweli hiki si kitu kizuri."

Lewandowski mkataba wake na Dortmund utakwisha Juni 2014, lakini mshambuliaji huyo mahiri anataka kuihama klabu hiyo mwaka huu.
Ukiweka kando Bayern, fowadi huyo pia anahusishwa na timu za Manchester United, Real Madrid na Juventus, lakini mabingwa hao wa Bundesliga wapo kwenye nafasi kubwa ya kumnyakua.

No comments:

Post a Comment