Pages

Wednesday, May 29, 2013

HUU NI MWANZO AU MWISHO WA BORUSSIA DORTMUND?


LONDON, England
KWA namna Arjen Robben alivyopita kasi kuwahi pasi ya kiufundi ya Franck Ribery, akapenya kwenye ngome ya Borussia Dortmund, akamiliki mpira, akamchambua kipa Roman Weidenfeller, kilichotokea, kimejieleza chenyewe.

Lilikuwa shambulizi la kushitua na kwamba lilikamilishwa barabara. Baada ya hapo, kelele zilizokuwa zikitoka kwa waliovaa jezi za njano na nyeusi, nyimbo zao za kushangilia, vilikwisha ghafla. Hii ilikuwa kwenye kipute cha aina yake kilichowakutanisha Wajerumani watupu.

2-1 ikawa matokeo ya mwisho na Bayern Munich ikapata matokeo chanya. Zama mpya zimeandikwa na Bayern imekuwa timu yenye nguvu zaidi Ulaya, kwa kiwango cha soka lao walichokionyesha ndani ya miezi 12 iliyopita, hakika walistahili kubeba ubingwa huo wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.

Kwenye mchezo wa fainali, Bayern ilipambana kuzikabili dakika 25 za kwanza, ambazo dhahiri walikuwa wamebanwa na Dortmund, jambo ambalo lilimsukuma kipa wao, Manuel Neuer, kuokoa hatari kadha - ambazo kwa msaada wake umeisaidia timu hiyo kutwaa taji lake la tano la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Mwisho wa mchezo huo, Bayern walionyesha ukomavu wao, walionyesha ujanja wao, ubora na kudhihirisha kwamba kikosi hicho cha Jurgen Klopp kilistahili matokeo hayo.

Robben, mchezaji mwenye daraja la aina yake, akiwa amewahi kuchezea klabu bora kabisa kama Chelsea, PSV Eindhoven na Real Madrid, ndiye aliyeamua matokeo ya mchezo huo, akitengeneza bao la kwanza kabla ya kufunga la ushindi katika dakika za lala salama.
Lakini, Die Borussen nao wametoka uwanjani vichwa juu. Pamoja na kwamba wamefanikiwa kuwa washindi wa pili, bado hilo haliwakatishi tamaa, kwani bado watastahili pongezi kubwa.

Ni mapema kuibeza timu hiyo ambayo msimu uliopita tu ilishangilia kutwaa taji lake la pili la Bundesliga, lakini kuna hisia za kutosha kwamba hiki kilikuwa kipindi kizuri kabisa kwa kikosi hicho kufikia mafanikio hayo makubwa.
Kwa upande wa pili, ni rahisi kusema kwamba Bayern itapanda ubora kutoka daraja moja hadi jingine baada ya mafanikio haya na wanapewa nafasi kubwa pia ya kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwakani, ambayo mechi yake itafanyika kwenye dimba la Estadio da Luz, Ureno, kitu ambacho kwa Dortmund hutarajii kuona kikitokea.

Kwa Dortmund, kikosi chenye wachezaji wengi vijana - kimeweza kuonyesha uwezo mkubwa kwa msimu huu na kucheza soka ambalo liliwaacha wengi vichwa wazi, kutokana na pasi zao, lakini kwenye majira yajayo ya kiangazi kitakuwa kipindi kigumu sana kwa upande wao katika kutambua nusura yao.
Tayari, Mario Gotze anawahama na amekubali kujiunga na Bayern, uhamisho ambao hautaishia kuwabakiza kuwa dhaifu na kupunguza nafasi yao ya mafanikio, bali unaowaongezea nguvu mahasimu wao wakuu.

Dalili zinaonyesha kubwa hata Robert Lewandowski atafungua milango ya kuondoka Westfalenstadion. Straika huyo wa kimataifa wa Poland, Lewandowski, ambaye amekuwa mtu muhimu kabisa katika kikosi hicho cha kocha Jurgen Klopp, amebakiza mwaka mmoja katika mkataba wake na tayari naye anahusishwa na mpango wa kutua Allianz Arena kuungana na nyota mwenzake wa Dortmund, Gotze.

Beki Felipe Santana, ambaye amekuwa akitumika kama mbadala wa Mats Hummels na Neven Subotic, amekubali kujiunga na Schalke, mahali ambapo anaamini atapata muda wa kucheza kwenye kikosi cha kwanza.
Na vipi kuhusu wengine? Beki wa kimataifa wa Ujerumani, Hummels umaarufu wake unazidi kuongezeka; kama ilivyo kwa kiungo mtaalamu Ilkay Gundogan. Marco Reus (licha ya kwamba ni shabiki wa ubora wa soka lake) umekuwa wa aina yake na hilo linaweza kumtoa tena kwenye kikosi hicho.

Sawa, suala la kupoteza wachezaji nyota ni kitu ambacho walikumbana nacho hapo kabla, ikiwamo kuondoka kwa kiungo fundi Shinji Kagawa, ambaye alitimkia Manchester United mwaka jana.
Lakini, kama wataondoka zaidi ya wachezaji watatu, jambo hilo litawachukua muda kuweza kujijenga upya na kuwa na makali ya kweli ndani ya uwanja.

Beki wa kulia, Lukasz Piszczek, tayari atakuwa pigo kwenye kikosi. Upasuaji wa nyonga aliopanga kufanyiwa mwishoni mwa msimu huu, utamuweka nje ya uwanja kwa takriban miezi mitano. Je, majeraha yatamuweka benchi mchezaji huyo pekee au ndo utakuwa mwanzo?

Kuna timu kama Real Madrid na Barcelona, Paris Saint-Germain, mabingwa wa Italia, Juventus, miamba miwili ya Manchester na mabingwa wa Europa League,  Chelsea ni wazi kabisa wataboresha vikosi vyao majira haya ya kiangazi na hilo linaiweka pabaya Dortmund kwamba msimu ujao hali inaweza kuwa mbaya kwao.

Na kwenye orodha ya timu hiyo, hapo mabingwa wa mwaka huu wamewekwa kando. Sawa, uhodari wa kocha Klopp hauna shaka na kwamba anaweza kuwa sababu kubwa ya BVB kurudi na kasi kubwa msimu ujao, kama tu hajaona inatosha na kuamua kuihama timu hiyo.

Kichapo walichokipata Wembley kinaonekana kama kinafikisha zama zao mwisho, kwa sababu baada ya hapo nyota wake wengi wanaweza kwenda kusaka malisho mapya. Acha tuamini kwamba jambo hilo halitokei na Borussia Dortmund ikaendelea kuwa timu inayosumbua barani Ulaya, lakini kinyume cha jambo hilo - hali inaweza kuwa mbaya kwa upande wa BVB na wakajikuta wanashindwa kuendeleza ubabe wao.

No comments:

Post a Comment