Pages

Sunday, May 26, 2013

LIONEL MESSI WA JANA HADI LEO, NI FILAMU INAYOVUTIA KUTAZAMA


BARCELONA, Hispania
KWA maneno yake mwenyewe, Lionel Messi amekuwa akiishi kwenye ndoto kwa kipindi chote tangu alipovuka Bahari ya Atlantic wakati huo akiwa na umri wa miaka 13 kwenda kujiunga na Barcelona.
Kwa sasa amekuwa mwanasoka, anayeuzika kama utaamua kumtengenezea filamu na kuiingiza sokoni. Kwa kipindi cha miaka minne iliyopita, ameweza kutwaa 'Oscar' ya FIFA baada ya kunyakua tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa duniani, Ballon d'Or tangu mwaka 2009.

Ametwaa medali ya ubingwa wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya mara tatu na mataji sita ya La Liga. Mwaka jana alivunja rekodi ya Gerd Muller, iliyokuwa imedumu kwa miaka 40 na kuwa mtu wa kwanza kufunga mabao 91 ndani ya mwaka mmoja.
Kwenye rekodi zake, Messi ameweza kutwaa kila kitu, isipokuwa taji la Kombe la Dunia. Lakini, staa huyo wa Argentina amepanga kurudi Amerika Kusini kwa nguvu mpya na kwenda kukiongoza kikosi chake cha Argentina kutwaa ubingwa wa Kombe la Dunia 2014, katika fainali zitakazofanyika nchini Brazil, ili kutimiza ndoto zake.

"Naota kuwa bingwa wa dunia, kutwaa ubingwa nikiwa na Argentina," alisema staa huyo mwenye umri wa miaka 25, ambaye anatazamiwa kwa macho yote katika fainali hizo zitakazofanyika katika ardhi ya bara lao la Amerika Kusini kwenye kipande chake kidogo cha filamu yake iliyoandaliwa na Audemars Piguet.

Watayarishaji hao wa filamu, wamechukua matukio yote ya kimpira yanayomuhusu staa huyo mwenye sifa ya kipekee kwenye ulimwengu wa mchezo huo. Yamekusanywa matukio yote tangu ya utotoni kwake, wakati alipokuwa akiwatambuka mabeki wakati akiichezea klabu ya Newell's Old Boys, kabla ya kuibukia kwenye akademia ya La Masia na sasa kuwa No 10 wa kihistoria katika klabu ya Barca na kuwa mchezaji bora kabisa katika sayari hii.

"Kwa kile ambacho mama na baba yangu waliniambia ni kwamba, nilikuwa nachezea mpira tangu nilipokuwa na umri wa miaka miwili mitatu," anasema Messi.
"Wakati nilipokuwa mdogo sana nilitambua kwamba, hicho ndicho kitu nilichokuwa nakipenda na nilichokuwa nataka kukifanya. Na wakati nilipokuwa mkubwa na kuanza kutambua mambo, hapo nikaanza kupenda zaidi.

"Siku zote nilikuwa mdogo, lakini hakukuwa na kikwazo. Kimo changu na uimara, hicho hakikuwahi kuniangusha. Sikujilinganisha na watoto wengine. Unapokuwa mtoto, kitu unachohitaji wewe ni kucheza na kufurahia. Hivyo sikutaka kujilinganisha na yeyote.
"Tangu nilipokuwa kijana mdogo nilitaka kuwa mchezaji profesheno na nilikuwa na ndoto za kucheza kwenye ligi kubwa."

Kwa Messi, ndoto zake bado zinaendelea, mapenzi yake kwenye mchezo wa soka ndio kwanza yanaanza, akiendelea na kile ambacho siku zote amekuwa akikifanya uwanjani: kufurahia kucheza.
"Nimekuwa nikijaribu kuingia uwanjani na kufurahia kucheza kama nilivyokuwa mdogo," anasema Messi. "Nafahamu kwamba nina majukumu na siku hizi nacheza kwa ajili ya kushinda, najaribu kusaka ushindi. Lakini, bado naendelea kufurahia kucheza kama nilivyokuwa zamani."

Wakati jana ikiwa imefanyika fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kwenye dimba la Wembley jijini London, mara ya mwisho fainali ya michuano hiyo ilipofanyika kwenye uwanja huo kabla ya hiyo ya jana, Messi alitawala mchezo na kuigomea United ndani ya ardhi ya England kwa kuinyuka mabao 3-1.

Na kama isingekuwa majeraha, pengine msimu huu angeweza kurudia mafanikio hayo kwa mara nyingine, lakini badala yake usiku wa jana aliketi tu kuwatazama wababe wa Barca, Bayern Munich wakisaka taji hilo la Ligi ya Mabingwa barani Ulaya kwa kumenyana na Borussia Dortmund.

Lakini, kabla ya kufikia fainali hizo za Brazil, Messi amepanga kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya itakayochezwa kwenye dimba la Estadio de Luz nchini Ureno. Kwenye soka, Messi ndoto zake ni kufanya vyema kila kukicha na hilo limemfanya kuendelea kuwa bora ulimwenguni, akilidhihirisha hilo kabla kwa kutwaa tuzo nne mfululizo za Ballon d'Or.

Na kwa kuyaweka kwenye filamu maisha ya staa huyo wa Barca na Argentina ni wazi kabisa itakuwa 'movie' itakayokuwa na soko la aina yake na kuongoza kwa mauzo.


No comments:

Post a Comment