Pages

Sunday, May 26, 2013

VIKWAZO VIKUU VINAVYOMKABILI MOYES KAMA KOCHA WA MAN UTD




LONDON, England
BADO ni ngumu kuamini kwamba, Sir Alex Ferguson hatakuwa kocha wa Manchester United msimu ujao. Gwaride la kutembeza taji mitaani, hotuba, sherehe za ubingwa, zote hizo zimepita kwa haraka sana na hazikuweza kuwa na furaha iliyojitosheleza.

Ulikuwa mwaka mrefu wenye mchanganyiko wa mambo mengi, kusherehekea na kuomboleza matukio yote yaliyotokea kwa timu hiyo. Lakini, mtu huyu kama alivyofanya mstaafu Paul Scholes, aliona ni vyema kuondoka na kuyaacha yote kuliko kuendelea kubaki kwenye klabu hiyo.

Sir Alex ni Manchester United, vitu hivi viwili vimekuwa na muunganiko wa kipekee. Mashabiki wote wapya wa klabu hiyo, wamekubali kuishangilia Man United kwa ajili ya Ferguson.
Kwenye klabu ya Man United, kulikuwa na Sir Matt Busby, na kisha kuna Sir Alex Ferguson. Watu hawa wawili hawabadilishiki, huwezi kupata wabadala wake. Kuwarithi nyayo zao ni kibarua kigumu sana kukubali kukifanya.

Na hilo linabainisha kwamba, uzito wa mzigo ambao utamhusu kocha mteule wa kurithi mikoba ya Sir Alex, David Moyes ni wazi utamzidi uzito. Ndani ya Old Trafford ni wazi kabisa Moyes atakumbana na vikwazo lukuki, vya muda mfupi na muda mrefu. Vikwazo ni vingi na haya ni baadhi tu ya mambo ambayo yatamfanya Moyes kuwa katika wakati mgumu kwenye kibarua chake hicho.

Tatizo la Wayne Rooney

Hii ni bahati kwa Moyes kwamba, kitu cha kwanza kinachomkabili katika kibarua chake mpya Old Trafford ni kutuliza kasheshe la mchezaji anayetaka kuhama, tena akiwa staa wa kikosi hicho.

Wayne Rooney hakuwa na msimu mzuri, lakini wakati Sir Alex akieleza wazi kwamba Rooney ameomba kuondoka, jambo hilo liliibua mshituko.
Mshambuliaji huyo aliwahi kuomba kuondoka United mwaka 2010, wakati alipodai kwamba klabu hiyo ilishindwa kusajili wachezaji wanaoeleweka, lakini akashawishiwa na kubaki.

Sasa ni 2013, United ni mabingwa wa Ligi Kuu England na wana kikosi imara kwenye karatasi ikiwa ni mara ya kwanza tangu alipoondoka Cristiano Ronaldo. Rooney bado anataka kuondoka, safari hii pengine hilo linachangiwa na kuwekwa benchi katika baadhi ya mechi.
Sababu nyingine inayodhaniwa hapa ni kwamba, anataka kuondoka kwasababu ya kutokuwa na uhusiano mzuri na kocha wake wa zamani, Moyes, ambaye alimnoa wakati alipokuwa Everton.

Wawili hao walikuwa na mgogoro mkubwa na kufikishana mahakamani 2006, wakati Moyes alimshitaki Rooney kwa kumwaandika vibaya kwenye kitabu chake kilichofahamika kwa jina la 'My Story So Far.'
Swali lililopo hapa ni jinsi gani Moyes ataweza kumaliza tatizo hilo na kumshawishi abaki au atamruhusu kuondoka? Huo ni mtihani wa kwanza unaomkabili Moyes katika kibarua chake hicho.

Wachezaji kumheshimu

Kuna makocha wachache sana katika mchezo huo wa soka ambao wamekuwa na nguvu ya utawala kama alivyokuwa Sir Alex Ferguson.
David Moyes hatakwenda moja kwa moja Old Trafford, huku akiwa na uhakika kwamba atapata heshima zote kutoka kwa wachezaji, hilo anapaswa kulitambua.

Zaidi ya yote, wachezaji wengi wa United walikuwa wakijitolea kwa kila kitu kwa ajili ya Sir Alex, hivyo kuwataka waendelee kufanya kitu kama hicho kwa Moyes kwa haraka ni jambo ambalo litakuwa na tatizo kidogo.

Moyes anachopaswa kufurahia hapa ni kwamba, wachezaji hao walimwaga machozi kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakati Sir Alex alipotangaza kustaafu, hivyo anaamini naye wachezaji watatumia imani hiyo kumheshimu kwasababu ni chaguo la kocha aliyeondoka.
Lakini, kilichopo ni wazi kabisa lazima atakumbana na majaribu kwenye suala hilo la kuheshimiwa na wachezaji. Itakuwa ngumu kuwaongoza wote kama alivyokuwa akifanya Sir Alex kabla ya mechi na wakati wa mapumziko.

Kitu kizuri kitakachombeba Moyes ni kwamba, wachezaji kutoka kwenye klabu anayoondoka wamekuwa wakimheshimu na kumsifu kwa lugha zote, jambo ambalo wachezaji wa United wataona kwamba wanakutana na mtu mwenye heshima zake.

Nguvu mpya ya Chelsea

Manchester United imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu bila ya kukumbana na purukushani zozote. Msimu ujao utakuwa muhimu kwasababu klabu za Manchester City na Chelsea zitakuwa zimejipanga kiushindani zaidi. Na katika mchakato huo, kurejea kwa kocha Jose Mourinho Stamford Bridge, hilo litawapa wasiwasi mkubwa Mashetani Wekundu.

Kitu ambacho Mourinho amekuwa akikifanya ni kupata matokeo. Amekuwa na rekodi nzuri ya kutwaa ubingwa wa ligi katika klabu anayokwenda kuinoa, tangu alipotoka FC Porto, ikiwa pia mataji mawili ya Ligi Kuu aliyotwaa Chelsea.

Na kama Mourinho atakaporejea kwenye klabu yake hiyo ya zamani ni wazi kabisa, mmiliki wake, Roman Abramovich, lazima atamwaga fedha za kufanya usajili, kitu kitakachompa jeuri Mreno huyo na kuisumbua United katika mbio za ubingwa.

Ripoti za hivi karibuni zilibainisha kwamba, usajili unaotarajiwa kufanywa na Mourinho ni pamoja na Radamel Falcao, Hulk, Isco na Marouane Fellaini. Kama Chelsea itaweza kuwanyakuwa wachezaji hao na kisha wakaungana na waliopo kwenye kikosi hicho, ni wazi kabisa United itakumbana na upinzani wa nguvu msimu ujao katika harakati za kutetea ubingwa wake.

Kutokana na utajiri wa vipaji vilivyopo ndani ya Chelsea kwa sasa na kisha wakampata mfungaji mahiri kama Falcao, ni wazi kabisa haitakuwa timu rahisi kuizuia ndani ya uwanja.
Moyes hana rekodi nzuri dhidi ya timu tano bora za kwenye ligi kwa misimu ya hivi karibuni. Hata kama atakwenda kukinoa kikosi imara kabisa cha United, bado atahitaji kuboresha mbinu zake za kuzifunga timu ngumu kwenye ligi hiyo.

Mchecheto wa kuinoa timu kubwa

Kuna mambo mengi yanamkabili Moyes katika kibarua chake hicho cha Old Trafford. Alipokuwa Goodison Park, alifanya kazi chini ya bajeti ndogo kabisa na kwamba hakupata nafasi ya kuwanoa wachezaji mastaa ambao wangeifanya klabu yake kuwa na hadhi kubwa.
Lakini, Manchester United ni timu yenye hadhi tofauti kabisa. Mahali hapo ataweza kuwanoa wachezaji nyota huku akitambua kwamba mwisho wa msimu mataji yatahitajika.

Moyes sasa atafanya kazi kwenye klabu kubwa, timu ambayo nyingine zitahitaji kuiga kutoka kwao, kitu ambacho ni mtihani mkubwa unaomkabili bosi huyo mpya.
Kwenye klabu ya Manchester United, nafasi nyingine zaidi ya kwanza, inaonekana kuwa ni anguko, tofauti na ilivyokuwa Everton, ambapo kupata nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya ndio ilikuwa dhamira yao kuu.
Ni kitu kibaya kukitaja kwamba Moyes hajatwaa taji lolote Goodison Park, kitu ambacho ni dhahiri kabisa kitakuwa mtihani mzito atakapotua rasmi Old Trafford.

Kudumu muda mrefu

Kubwa katika mambo yote, changamoto inayomkabili Moyes ni kuweza kudumu miaka mingi katika klabu hiyo ambayo kocha wake anayeondoka, Sir Alex alikaa hapo kwa miaka 26.
Moja ya mambo yaliyomfanya Ferguson kuwa mtu spesho ni uwezo wa kubadilika kulingana na mchezo na pia kuunda timu ya ushindi. Jambo hilo limefanya miaka 26 aliyodumu kwenye kikosi hicho, suala la kutwaa mataji kuonekana la kawaida tu.
Hakuna anayemtaka Moyes ainoe timu hiyo kwa miaka 26, wala 16, lakini ukweli ni kwamba, mpango mbadala na hilo ndilo maana United haikufikiria kumpa kazi Jose Mourinho.

Familia ya Glazer na Sir Alex walihitaji msimamo, mtu ambaye hatababaishwa na mambo mengine au kushawishika na changamoto za kutoka nje. Sawa, Moyes anapaswa kushinda, tena mara kwa mara. Maofisa wa United hawawezi kuwa kama wa Chelsea au Manchester City kwa kutimua makocha pindi mambo yanapokwenda kombo kwenye msimu, lakini matarajio ya Old Trafford ni makubwa, hivyo suala la ushindi ni kitu kisichopingika.

Mashabiki watamvumilia, lakini hilo halionekani kwamba litaendelea kufanyika kama klabu itaonekana kuporomoka. Hii ni changamoto kubwa kwa Moyes, ambaye atajiunga na timu ambayo imetwaa mataji matano kati ya saba ya Ligi Kuu England ya hivi karibuni. Hizi ndizo changamoto zinazomkabili Moyes katika kibarua chake kipya Stamford Bridge.

No comments:

Post a Comment