Pages

Sunday, May 26, 2013

JIKUMBUSHE TANGA INTERNATIONAL BENDI ILIVYOWASHIKA WAPENZI WA DANSI NA WIMBO WAKE WA 'VICKY MASOMONI'

ENZI zile za muziki wa dansi uliokuwa na hadhi yake kwenye miaka ya mwanzoni mwa 70 hadi mwanzoni mwa 90, kati ya bendi zilizokiuwa zikiwachanganya washabiki, ni Tanga International na Dar International.
Bendi hizi licha ya kufanana majina, lakini pia zilikuwa na sifa za kuchukuliana wanamuziki ambapo mpiga solo wake, Patrick Kamaley aliwahi kuzipigia bendi zote hizi mbili kwa nyakati tofauti.

Lakini umaarufu wa Tanga International haukuvuma sana jijini Dar es Salaam, kwa vile wakati bendi kubwa za hapa nchini kama Mlimani Park, JUWATA na nyingine zikinyang'anyana wapenzi, Tanga International iliendelea kupanua himaya yake kwenye mji huo wa Mwambao.
Wimbo wake wa kwanza ulioitambulisha bendi hiyo ni Vick Masomoni uliotungwa na kuimbwa na Malika Mwakichuri, aliyekuwa mwimbaji kiongozi wa bendi hiyo.

Lakini umaarufu wa bendi hiyo iliyokuwa ikitamba sana na aina fulani ya uimbaji wenye mahadhi ya mwambao ilikuwa na nyota mwingine mwenye kipaji cha uimbaji aliyefahamika kwa jina la Kaloja wa Kaloja.
Ukitaka kusikia sauti ya Kaloja basi hebu sikiliza nyimbo kama 'Zubeda wa mama mimi nakutafuta'.
Lakini pia kwenye wimbo wa Vick, Kaloja naye alifanya mambo makubwa, kwa vile yeye ndiye aliyeshiriki kuimba sauti ya pili akishirikiana na Banza Tax na Mwakichuri.

Bendi hiyo ilipokuwa ikitamba haikukosa kuwa na bendi hasimu ambapo kipindi hicho ilikuwa ni Dar Intyernational, ambapo chanzo cha kuwa 'Paka na chui' ni kutokana na mpiga solo Patrick Kamaley kuikimbia Dar International kwenda Tanga.
Ikumbukwe Kamaley au maarufu kwa jina la Bedui ndiye aliyekuja kuwa mpiga solo wa bendi ya Bimalee, hasa baada ya kuondoka Joseph Mulenga na Abdalah Gama walioijiunga mwaka 1984 na kisha kuitosa bendi hiyo.

Lakini wanamuziki kama Kaloja wa Kaloja yeye alionyesha uvumilivu wa hali ya juu pale alipomaliza muziki wake bila ya kuchukuliwa na bendi za jijini Dar, licha ya kuwa na uwezo mkubwa.
Kaloja baadaye alijiunga na bendi ya Mwambao Sound ambayo pia alipitia mwimbaji Fresh Jumbe Mkuu, aliyekuja kuwa nyota alipojiunga na bendi za Dar International, JUWATA, Mlimani Park, OSS na baadaye Bicco Stars.
Kwa ujumla wanamuziki wengi waliopitia bendi ya Tanga International baadaye waliweza kutingisha sana na bendi za Jijini Dar, kwani licha ya Fresh Jumbe, lakini akina Omar Zumo, John Maida nao kwa nyakati tofauti waliweza kupita katika bendi mbalimbali.

Malika Mwakichuri ambaye Tanga alikuwa na umaarufu kama wa chumvi ndani ya mchuzi kutokana na uimbaji wake baadaye alifanya kazi hiyo Arabuni kabla ya kurejea nchini na mwaka 2002, alishirikiana na wanamuziki kadhaa na kutumbuiza tamasha la kumuenzi marehemu Marijani Rajab.

Tamasha hilo lilifanyika kwenye ukumbi wa Traventine Magomeni, ambapo licha ya yeye wanamuziki wengine walioshiriki ni marehemu Kassim Mponda, Marehemu Tino Maseinge, Magomba Rajab, Marehemu Jumanne Uvuruge, marehemu Comson Mkomwa, Ali Adinani, Bonny Chande na Muharami Seseme.
Mwakichuri alionyesha uwezo mkubwa wa kuimba pale alipokabidhiwa kuimba sauti ya kwanza iliyokuwa ikiimbwa na marehemu Ali Rajab Mshangama, aliyekuwa mwimbaji mahiri wa bendi ya Safari Trippers na baadaye Dar International, kabla ya kujiunga na bendi ya Makassy akiwa ni mpuliza saxaphoni.
Lakini yote kwa yote, mpenzi msomani wa makala hii bila shaka ungependa kukumbuka mashairi yaliyokuwemo katika wimbi huo wa Vick masomoni.


Wimbo huo unaanza hivi:-
Nifanye nini yaliyotokea aa
Nikikumbuka mimi, ninalia mimi nifanye nini
Mpenzi wangu Vick anaondoka ee aenda kozini, Lakini Vick mama nenda salama ooo Vick.
Kiitikio

Vick ee kwa heri Vick tutanana safari ijayo
Mwakichuri
Safari yako mpenzi Vick ni ya muda mrefu, nenda huko ufikapo umalize kozi yako, jambo ninalokuomba uzidi kuwa mtulivi Vick Ulaya kuna mambo mengi Vick ee
Rudia kiitikio.

Mwakichuri
Tanzania na Ulaya mpenzi Vick ni mbali, mara huko ufikapo, uzidi kunikumbuka, nikumbuke kwa barua tupeane hali mama kwa heri Vick oo mpenzi mama.

Ukiuangalia wimbo huo utakumbuka kuwa kuna jibu lake lakini halikuimbwa na bendi hiyo, bali bendi iliyokuwa na makao yake jijini Dar iliyofahamika wa jina la Ushirika Tanzania Stars.
Wimbo huu wa pili ulitungwa na mwimbaji marehemu Suleyman Mbwembwe, ambaye naye pia alipitia Tanga International kabla ya kuja jijini na kujiunga na bendi hiyo na baadaye kutamba na bendi za Mlimani Park, Vijana Jazz na ile aliyomalizia uhai wake ya Msondo ngoma.
Kwenye wimbo wa majibu ya Vick Mbwembwe aliimba hivi: Karibu ee Vick nyumbani, karibu mama karibu ee mpenzi wangu Vick.
Mbwembwe

Safari ni shida jama ee lakini umerudi salama, safari ina matatizo lakini umerudi salama, nashukuru Vick nashukuru, Vijana wenzangu nashukuru.
Kwa ujumla walichojivunia wanamuziki wa miaka hiyo ni kuzifanyia kazi tunzi zozote zilizoibuka na kuhitaji mwendelezo kwa mashabiki wao.

Ndiyo maana mwimbaji mwingine maarufu, Ahmed Manyema Wangaka aliibuka na wimbo wa Furaha ya Harusi pale bendi ya Les Wanyika ilipopiga kibao kilichotamba sana enzi hizo kiitwacho Sina Makosa.
Vinavyoshabihiana katika nyimbo hizi ni staili ya uimbaji ambapo wimbo wa Wangaka uliwashtua mashabiki wakidhani umepigwa na bendi hiyo ya Les Wanyika ya Kenya.

No comments:

Post a Comment