Pages

Wednesday, May 15, 2013

NIYONZIMA: ROHO, MWILI VINAITAMANI SIMBA SC




KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima, amesema kwamba sasa ameweka kando mambo yote na kusisitiza kuwa moyo wake, mwili na akili vyote vinatamani kuona anaifunga Simba katika mchezo wao wa Ligi Kuu Tanzania Bara, utakaofanyika Jumamosi hii.

Nyota huyo wa kimataifa wa Rwanda, Niyonzima maarufu kama Fabregas, ambaye kwa sasa anaripotiwa kuwindwa kwa udi na uvumba na Simba, alisema hajali lolote kwenye hilo zaidi ya kuwafunga mahasimu wao hao wakati timu yake itakapomenyana nao katika mchezo wa funga dimba la Ligi Kuu Bara msimu huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi hii.

Niyonzima, ambaye anaaminika kuwa kiungo bora kabisa kwenye Ligi Kuu ya Tanzania Bara, aliliambia DIMBA ameweka pembeni masuala yote ya kuhusu hatima yake ya msimu ujao zaidi ya kuitumikia klabu yake ya sasa na kuhakikisha anaipatia ushindi ili kuweka heshima dhidi ya mahasimu wao.

"Kwa sasa akili yangu ipo kwenye mechi hii. Moyo na fikira zangu zote zipo kwenye kuifunga Simba na kuipa heshima Yanga," alisema.
Kuhusu ubora wa mkali huyo wa Amavubi, Katibu Mkuu wa zamani wa Simba, Mwina Kaduguda, alisema ametazama nyota wote wanaocheza soka hapa nchini na kusisitiza kwamba kiungo huyo ndiye anayestahili kuendelea kubaki hapa nchini miongoni mwa nyota wote wa kimataifa.

Kaduguda alisema ni wazi kabisa mchezaji huyo anastahili kulipwa mshahara mkubwa, kutokana na kazi yake isiyokuwa na shaka anayofanya ndani ya uwanja na kwamba Yanga inapaswa kushukuru kwa kuwa na mchezaji huyo kwenye kikosi chao.

Kiungo wa zamani wa Simba, Selemani Matola, amekikubali kiwango cha Niyonzima na kuwataka Simba kama wana mpango wa kumnasa mchezaji huyo basi watimize jambo hilo kwani ni mchezaji mwenye kila kigezo cha kuwachezea miamba hao wa Msimbazi.

Matola alisema uongozi wa klabu hiyo ya Simba unapaswa kutazama mahitaji ya benchi la ufundi na kama kutakuwa na ombi la kusajiliwa kwa mchezaji kama Niyonzima, basi wasilipuuzie hilo na walifanye kwa nguvu zote, kwasababu litakuwa na faida kubwa kwa klabu hiyo.

Alisema Niyonzima ni mchezaji mzuri ataweza kusaidia Simba msimu ujao endapo watafanikiwa kumnasa ila ana uhakika kiungo huyo kutoka kwa kipindi kirefu katika klabu hiyo, kwasababu dhamira yake ni kwenda kucheza soka ng'ambo.

“Endapo Simba watafanikiwa kumchukua na kumsajili atakuwa msaada mkubwa katika kikosi hicho cha msimu ujao, ambapo uongozi huo umeonyesha nia ya kutaka kufanya usajili ili kufanya kweli katika ligi msimu ujao,” alisema Matola.

Niyonzima kwa sasa analitikisa soko la usajili wa soka la Tanzania, baada ya kuwindwa na klabu kadha, Simba na Azam FC huku klabu yake ya Yanga ikidai kwamba imemsainisha mkataba wa miaka miwili mchezaji huyo kitu ambacho kiungo mwenyewe amekikana na kufanya mchakato wa kuwania saini yake kupamba moto.

No comments:

Post a Comment