Pages

Thursday, May 16, 2013

HOMA YA WATANI WA JADI:MAYAI VIZA DILI ZANZIBAR,YANGA YAKIMBIA PEMBA


TIMU kongwe za soka nchini ambao ni mahasimu wa jadi, Simba na Yanga zilizoweka kambi ya kujiandaa na pambano lao la kufunga msimu Ligi Kuu Bara visiwani Zanzibar, zimefanya bei ya vifaa ya madawa ya asili kuwa dili ghafla ikiwemo mayai viza kutokana na kudaiwa kuongezeka kwa matumizi yake.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na Lenzi ya Michezo na baadaye kufumania nyendo kutoka kwa baadhi ya wadau waliokuwa wakishughulikia mchakato huo, ulinasa orodha ya vifaa, timu moja ilivyotakiwa kununua na kisha kuvipeleka kwa 'mtaalamu' wao ambapo ubani, tende, sukari guru, kuku na mayai viza  vikisakwa kwa udi na uvumba.

Kwenye kambi mojawapo ya timu hiyo ambayo inatarajiwa kukutana na mpinzani wake kesho katika Uwanja wa Taifa, baada ya raundi ya kwanza kutoka sare, imani kubwa imetanda kuwa vifaa hivyo vikipatikana na kisha kufanyiwa mambo kwa 'mtaalamu' wao anaweza kubadili matokeo.

Lenzi ya Michezo lilifanikiwa kunasa mawasiliano yaliyokuwa yakifanywa baina ya viongozi wa timu moja yenye rekodi nzuri ya kumfunga mtani wake, akifanya mawasiliano na kiongozi mmoja aliyekuwa akiwasiliana na waganga kutoka Dar es Salaam na Pangani, Tanga.

Kwa mujibu wa mawasiliano hayo, tayari wamebaini kuwa timu yao ilishazidiwa ujanja mapema na itakuwa ni vigumu kunusurika na kipigo, hivyo jitihada za ziada zilihitajika ili 'mtaalamu' aweze kubadili matokeo.

Moja ya ujumbe mfupi (sms) ulionaswa kutoka kwa mganga kwenda kwa kiongozi, ulisema ili kubadili matokeo lazima zitengenezwe kadi nyekundu mbili kwa wapinzani wao na pia penalti moja na kwamba endapo akibadili matokeo hayo, kuna uwezekano wa kuzuka vurugu kubwa.

“Kutakuwa na vurugu kubwa, kama nikifanya hivi, lakini mimi nashauri mtimize yale niliyoyaagiza ili tupindue kwa njia nyingine na kazi yangu ni uhakika  kama mko tayari nianze kazi mapema,” ulisema ujumbe huo mfupi.

Ujumbe mwingine kutoka kwa mganga kwenda kwa kiongozi wa timu moja, ulikuwa ukiainisha vitu vinavyohitajika ili kuhakikisha kuwa timu inapata matokeo mazuri katika mchezo huo.
“Nataka nipate vitu hivi ili nivipeleke kwa Bimtuka. Vitu vyenyewe ni Halua kilo 3, tende kilo 3, Chungu 1, sahani nyeupe 1, visu 7, kibatari kimoja, mafuta ya taa lita 5, sindano za kushonea kwa mkono 11, nyembe 11 pamoja na vitambaa na majina yote ya wachezaji wa wapinzani wenu,” ulisomeka ujumbe huo.

Baada ya hapo kiongozi huyo alijibu kuwa kila kitu kiko sawa na atakamilishiwa kila anachohitaji mganga huyo na kumtaka afanye kazi ya uhakika kama ile ambayo aliwahi kuifanya na kuleta matokeo mazuri.
Ujumbe mwingine ulionaswa ukiwa ni kutoka kwa viongozi na mmoja wa wanachama wa klabu mkoani Tanga, ulisema, “mkuu hadi sasa tumeona kuwa tuna ushindi wa 3-0, hii ni kwa mujibu wa duru kutoka Pangani, lakini kwa kuwa siku bado, chochote kinaweza kutokea, maana wenzetu pia wanahangaika sana, cha msingi tuwe makini na nyie mlio na timu muwe makini zaidi na watu."

Kutokana na hali ya ushirikina kutawala katika kambi za timu hizo kongwe, kwa sasa inadaiwa wachezaji wamepigwa marufuku kupeana mikono na watu hovyo na wageni wamekatazwa kabisa kufika kwenye kambi zao.

Si jambo la ajabu kwa timu za Simba na Yanga kuonekana zikiendekeza vitendo vya kishirikina kabla na siku ya mechi, lakini hata hivyo, Lenzi ya Michezo tunaamini maandalizi mema na kujituma ndiyo njia pekee ya kuweza kuibuka na ushindi na ushirikina hauna nafasi katika soka.

No comments:

Post a Comment