Pages

Sunday, May 26, 2013

BAYERN NDIO HABARI YA MJINI BAADA YA KUTWAA KOMBE LA MABINGWA ULAYA


LONDON, England
PICHA limekwisha na Arjen Robben ndiye steringi; ndicho unachoweza kusema baada ya Mdachi huyo 'kupika' moja na kisha kufunga jingine wakati alipoisaidia Bayern Munich kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya baada ya kuinyuka Borussia Dortmund mabao 2-1 katika fainali iliyofanyika Wembley Stadium jijini London, England jana usiku.

Ikicheza fainali kwa mara ya tatu ndani ya miaka minne, Bayern usiku wa jana iliweza kuondoa jinamizi lililokuwa likiwakabili la kufungwa kwenye mechi za fainali kwa kuwabwaga Wajerumani wenzao hao na hivyo kufuta hasira za msimu uliopita wakati alipofungwa kwa penalti na Chelsea kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa Allianz Arena.

Makosa katika safu ya ulinzi kwenye kipindi cha pili yaliigharimu Dortmund na hivyo kushuhudia wakifungwa mabao mepesi licha ya kipa wao, Roman Weidenfeller kufanya kazi ya ziada katika kipindi cha kwanza kwa kuokoa hatari kadha kutoka kwa Robben, Mario Mandzukic na Thomas Muller.

Mchezo huo ulianza kwa timu zote kuwa makini na kushambuliana kwa zamu, ulishuhudia dakika 45 zikimalizika kwa sare ya bila kufunga, huku makipa wote wakilazimika kufanya shughuli ya ziada, ambapo kipa wa Bayern, Manuel Neuer, mara kadha alijikuta kwenye mtihani mzito wa kuokoa hatari za wachezaji wa Dortmund, akiwamo mshambuliaji Robert Lewandowski.

Ikitambua kukisa taji hilo mara mbili ilizotinga fainali ndani ya miaka minne iliyopita, wakipoteza mbele ya Inter Milan na kisha dhidi ya Chelsea mwaka jana, Bayern iliamini kitu kimoja tu kwamba usiku wa jana ndio ilikuwa siku yao kutwaa ubingwa huo, hasa ukizingatia ilikuwa ikikutana na timu ambayo inayoifahamu kutokana na kucheza ligi moja ya Bundesliga.

Kwenye kipindi cha kwanza, Dortmund walionekana kuwabana Bayern na kuwafanya washindwa kutengeneza nafasi nyingi za mabao, lakini hali ilikuwa tofauti kwenye kipindi cha pili, ambapo baada ya kurejea kutoka vyumbani, Bavarians walionekana kushiba maelezo ya kocha wao, Jupp Heynckes na hivyo kutawala kipindi hicho.

Kipindi hicho cha pili pia kiliwashuhudia Dortmund, inayonolewa na Jurgen Klopp, ikijichanganya kwenye safu yake ya ulinzi na hilo liliwafanya wapinzani wao kuwa na uhakika kwamba ilikuwa na nafasi ya kutumia makosa hayo kupata mabao ambayo yangeleta ushindi.

Katika dakika 60, Robben alifanya kitu kilicholeta tofauti kwenye mchezo huo baada ua kuwapita mgogoni mabeki wa Dortmund na kuunasa mpira ambao alikwenda nao hadi kwenye mstari wa kona na kupiga krosi, ambayo ilikoswa na Schmelzer na kumkuta Mandzukic, ambaye aliusukumia nyavuni na kuifanya Bayern kuongoza kwa bao 1-0.

Mchezo huo ambao ulikuwa na bahati kubwa kwa Mbrazil Dante, ambaye alistahili kuonyesha kadi nyekundu, alicheza rafu mbaya na kusababisha penalti ambayo iliwafanya Dortmund kupata bao la kusawazisha katika dakika 67.

Dante alimrukia daruga la tumboni mshambuliaji Marco Reus na hivyo kumfanya mwamuzi, Nicola Rizzoli kutoka Italia kupuliza kipyenga kuashilia upigwe mkwaju wa penalti, ambao IIkay Gundogan, hakufanya mzaha kwa kumpeleka kulia Neuer na yeye akipiga mpira kushoto kufanya ubao wa matokeo kusomeka 1-1.
Wakati mashabiki wengi ndani ya uwanja wa Wembley wakiwa wanasubiri kuona mpira huo ukiingia kwenye dakika 30 za nyongeza, mpira mrefu uliopigwa na kipa Neuer ulitua kwenye miguu ya Franck Ribery, ambaye aliugusa kwa kisigizo - huku uzembe wa mabao wa Dortmund ukimruhusu Robben kuwahi mpira huo na kuwalamba chenga mabeki kadha kabla ya kumchambua kipa Weidenfeller na kupiga bao la pili katika dakika 89.

Robben, ambaye alishuhudia akitoka kapa mara kadha na kikosi hicho wakati aliponyukwa na Inter na kisha dhidi ya klabu yake ya zamani, Chelsea - baada ya kupata nafasi hiyo jana usiku hakutaka kuichezea hasa ukizingatia mwanzoni alipoteza nafasi kadha ambazo angeweza kuifanya Bayern ishinde mapema.

Kwa Robben bao hilo lilikuwa na furaha ya aina yake baada ya mwaka jana kukosa penalti wakati walipomenyana na Chelsea, lakini safari hii alimwaga machozi ya furaha na kushangilia kuliko mchezaji mwingine yeyote Wembley kutokana na kuweza kuisaidia timu yake kutwaa ubingwa huo.
Na sasa Bayern ndio Wafalme wapya wa Ulaya – huku wakiweza kuwasambaratisha Juventus na Barcelona kabla ya kumaliza na Dortmund jana usiku.
Na sasa wameweka historia ya aina yake na kucha anayemaliza muda wake, Heynckes huku jambo hilo likiacha mtihani mgumu kwa kocha mpya Pep Guardiola, ambaye atachukua kijiti cha kuinoa timu hiyo msimu ujao.

Na sasa Bayern imenyakua ubingwa wake wa tano na kufungana na Liverpool, ambao nao wameubeba ubingwa huo mara tano.
Kwa usiku huo wa jana, ulikuwa wa mambo mengi ya kuvutia huku nusu uwanja ukiwa umepambwa kwa rangi za njano na nyeusi, wakati nusu nyingine ilikuwa na rangi nyekundu na nyeupe.
Bayern imefika fainali hiyo baada ya kuinyuka Barca jumla ya mabao 7-0, wakati Dortmund ilisonga kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3 dhidi ya Real Madrid.

Lakini, katika mechi nane za hivi karibuni ilizozikutanisha timu hizo, Dortmund imeshinda mara tano na kutoa sare mbili. Bayern waliwafunga wao kwenye Kombe la Ujerumani mwaka huu.
Dortmund: Weidenfeller, Piszczek, Subotic, Hummels, Schmelzer, Bender (Sahin 90+1), Gundogan, Blaszczykowski (Schieber 90+1), Reus, Grosskreutz, Lewandowski.
Bayern: Neuer, Lahm, Boateng, Dante, Alaba, Javi Martinez, Schweinsteiger, Robben, Muller, Ribery (Gustavo 90+1), Mandzukic (Gomez 90+4).
Refa: Nicola Rizzoli (Italia)

No comments:

Post a Comment