Pages

Sunday, May 26, 2013

ARSENAL MSIMU UJAO HAWATASHEHEREKEA 'TOP FOUR?


LONDON, England
UTAKUWA msimu wa Arsenal, weka sarafu yako hapo. Kwa ilivyokuwa msimu uliomalizika hivi punde, Arsenal ni wazi kabisa waliomba mambo yaishe.
 Lakini, kilichotokea siku ya mwisho ya kufunga msimu, kimebashiri mwanzo wa hali itakavyokuwa msimu ujao.

Nyota hao wa Arsenal walidansi kwa furaha kubwa ndani ya uwanja na hata mashabiki wao jukwaani St James’ Park, walikuwa na furaha kubwa baada ya mechi yao hiyo ya kufunga msimu.
Ushindi mwembamba wa 1-0 Newcastle United ilitosha kabisa kwa Washika Bunduki hao wa London kukamata nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi na hivyo kunyakua tiketi ya kucheza mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao.

Waliweza kunyakua nafasi hiyo iliyokuwa na ushindani mkali dhidi ya Tottenham Hotspur, mahasimu wao wakuu, jambo hilo liliongeza utamu wa nafasi hiyo. Ukiweka kando kushika nafasi ya nne kwenye ligi na kufuzu michuano ya Ulaya msimu ujao, kingine kilichoifurahisha Arsenal na kushangilia kwa nguvu zote ni kuibwaga Spurs, iliyokuwa wakichuana vikali kuisaka tiketi hiyo ya kushiriki mikikimikiki ya Ulaya.

Msimu huu uliomazika, ulimshuhudia kocha Arsene Wenger akishutumiwa vikali na mashabiki wa timu hiyo na kuzua maswali mengi ni mahali gani atakuwa ameifikisha Arsenal, baada ya msimu kumalizika.
Kuna nyakati mashabiki hao walikata tamaa kabisa na mwenendo wa kikosi chao na pengine kudhani kwamba wasingeweza kufuzu michuano hiyo ya Ulaya, lakini mwisho wa msimu, Wenger alishinda vita hiyo na kuifanya timu hiyo kufuzu michuano ya Ulaya kwa msimu wa 16 mfululizo ikiwa chini yake.

Lakini, pamoja na kushangilia kuishinda vita hiyo ya nne bora, ukweli wa mambo ni kwamba, huu si wakati wa kusherehekea au kupongezana kwamba wamefanya kazi nzuri. Kubwa na muhimu ambalo linapaswa kufanywa na Arsenal ni kujijenga upya na kuwafanya kuwa timu yenye nguvu zaidi kwenye soka la England, kitu ambacho ni wazi kabisa wanaweza kukifanya.

Msingi mkubwa walionao ni kuwekeza kwenye kikosi, ambacho ni sawa hawana wachezaji mastaa, lakini wanamiliki wachezaji wenye vipaji vikubwa vya mchezo huo na hilo waliweza kulionyesha wakati waliposhinda mechi nane kati ya 10 toka walipopoteza kwenye mechi ya mahasimu zao hao wa London, Spurs mwezi Machi.

Kiwango na nguvu ni kitu ambacho kimekuwa kikitawala kikosi cha Wenger kwa wiki za hivi karibuni na kujenga timu imara ndicho kitu kilichopo kwenye mipango ya Arsenal kwa sasa, ili kuondoa pengo la ubora lililopo baina yao na klabu za Manchester na Chelsea.

Arsenal ina pauni milioni 123, fedha ambazo zimetulia tu benki na hivi karibuni wamesaini mkataba mpya wa udhamini wenye thamani ya pauni milioni 150 na kampuni ya vifaa vya michezo ya Puma, ambapo pia itagharimia vifaa vya timu hiyo kwa pauni milioni 30 kwa mwaka.
Miundombinu yao na mipango ya kibiashara inaifanya Arsenal kuwa moja ya klabu bora na tajiri barani Ulaya, hata bila ya fedha kiasi cha pauni milioni 30 ambazo itazipata kutokana na ushiriki wao kwenye Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu ujao.

Na sasa kocha aache kuzichungulia fedha hizo na badala yake atumie fursa hiyo kunyakua wachezaji watakaounda kikosi bora kitakachokuwa tayari kushindania mataji msimu ujao utakaoanza Agosti 17 mwaka huu.
Wenger ana kiasi kikubwa cha fedha hadi pauni milioni 90, ambazo atazitumia kwenye usajili na mishahara ili kukiboresha kikosi chake, ili kuweza kuhimili ushindani wa mataji ambao mara nyingi umekuwa ukianzia kwenye robo ya tatu ya msimu.

Kuna mambo machache tu yakifanyika, wababe hao wa London wataweza kuwa moja ya timu shindani katika kuwania ubingwa wa Ligi Kuu England, ubingwa ambao umekuwa adimu kwenye kikosi hicho cha Emirates.
Kitu muhimu kabisa ambacho Arsenal inapaswa kukifanya ni kwamba, isijaribu kurudia makosa kama waliyofanya ndani ya misimu miwili iliyopita kwa kuwauza wachezaji wake nyota, kama Cesc Fabregas, Samir Nasri na Robin van Persie.

Lakini, sasa Bacary Sagna moja ya wachezaji muhimu katika kikosi cha kwanza, ataondoka mwisho wa msimu huu, licha ya kwamba kumekuwa na mpango wa kumsajili beki wa kulia wa Sochaux, Sebastien Corchia kuziba pengo la Mfaransa huyo.
Nahodha Thomas Vermaelen naye atauzwa na hilo linatokana na mchezaji huyo kukosa namba kwenye kikosi cha kwanza, hivyo ni wazi kabisa asingeweza kuhitaji kuendelea abaki mahali hapo.

Lakini, kuondoka kwa Vermaelen hakuwezi kuwa pengo kwenye timu hiyo, kwasababu tayari Wenger alishamwona mrithi wake, ambaye ni beki wa Swansea, Ashley Williams.
Pamoja na hapo, usajili wa nyota wachache wataifanya Arsenal kuwa na nguvu zaidi na kuwa mshindani wa kweli kwenye vita ya mataji England na barani Ulaya.

Ujio wa kipa mwenye uzoefu, atakayeshindana na Wojciech Szczesny,  usajili wa beki wa kulia, kiungo mkabaji na mshambuliaji wa kweli, hilo litaifanya Arsenal kuwa na nguvu mpya, hasa ukizingatia kwamba haitakuwa na shaka katika kupata wachezaji wa kiwango bora kwasababu wamemaliza nafasi ya nne na hilo litawafanya kucheza michuano ya Ulaya.

Usajili wa mtu kama Stevan Jovetic unaweza kuifanya timu hiyo kupunguza pengo lililopo baina yake na wapinzani, huku kukiwa na dhamira ya dhati kabisa ya kumnasa Wayne Rooney, ili kutimiza ahadi ya kuwa tishio msimu ujao, hasa ukizingatia fedha za kufanya usajili wa wachezaji mastaa zipo.
Imani kubwa iliyopo ni kwamba, kiungo Jack Wilshere hatakuwa mwenye kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara tena na hivyo ataweza kuonyesha utawala wake katika sehemu ya kati ya uwanja.

Wilshere, 21, amecheza mechi 25 za Ligi Kuu msimu uliomalizika hivi karibuni, kutokana na kusumbuliwa na  majeraha na imani kubwa kwamba kwa mapumziko ya sasa nyota huyo ataweza kurudi dimbani msimu ujao akiwa na kasi, ari na nguvu mpya na kiwango bora kabisa.

Baada ya miezi 12 ya hali ngumu kwa Arsenal, hatima ya msimu ujao inaonekana kuwa na mwanga. Na sasa umewadia wakati wa Arsenal, dansi ambalo watalifanya ndani ya uwanja mwishoni mwa msimu ujao, halitakuwa la kufurahia kuipiku Spurs kwenye nafasi ya nne bali ni kumaliza ukame wa mataji uliodumu katika klabu hiyo kwa misimu kadha sasa.

No comments:

Post a Comment