Pages

Sunday, May 26, 2013

NGASSA AISUBIRI SIMBA KOMBE LA KAGAME


NYOTA mpya wa Yanga, Mrisho Ngassa, amesema kwamba anasubiri kwa hamu kuivaa klabu yake ya zamani aliyokuwa akiichezea kwa mkopo, Simba kwenye michuano ya Kombe la Kagame litakaloanza mwezi ujao nchini Sudan Kusini.
Ngassa, ambaye wiki hii alirejea katika klabu yake ya zamani ya Yanga, anaamini kuna uwezekano mkubwa kwa michuano hiyo ya Kagame ikashuhudia mechi ya watani wa jadi kitu ambacho anasubiri kitokee kwa hamu kubwa.
Akiungana na mchezaji mwenzake, Didier Kavumbagu, wawili hao walisema kwamba wanachopenda kitokee Sudan Kusini ni kumenyana na mahasimu zao hao wa hapa nchini, Simba.
Yanga, ambayo ni mabingwa watetezi wa kombe hilo watakwenda kwa nia moja ya kutetea ubingwa wao katika mikikimikiki hiyo itakayoanza Juni 18 hadi Julai 2 mwaka huu.
Ngassa amesema kwamba, anatamani aanze mapema kuifunga Simba ikiwa ni zawadi kwa wapenzi wake wa Yanga ambao alioachana nao kwa misimu miwili alipokuwa akichezea timu hiyo na Azam kabla ya kujiunga kwa mkopo Msimbazi.
Alisema hatua hiyo itawatibitishia wapenzi kwamba alikuwa kwenye timu hiyo ya Msimbazi kwa ajili ya kutafuta riziki, lakini mapenzi yake kwa kipindi chote yalibaki katika timu yake ya Yanga.
"Nitahakikisha naifungia mabao timu yangu katika michuano ya Kagame ili wapenzi wasahau yote niliyoyafanya nikiwa mwana mpotevu," alisema.
Kavumbagu ambaye awali alikuwa na hatihati ya kuendelea kuwepo kwenye kikosi cha Yanga msimu ujao kutokana na kushuka kiwango na baadaye kuahidiwa kuendelea na ulaji alisema, atahakikisha anarudisha makali yake kama fadhila yake kwa uongozi wa timu hiyo ulioonyesha kumjali.
Mchezaji huyo ambaye bado ana mkataba wa miezi sita zaidi kuichezea timu hiyo, alifunga bao la kwanza katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Simba katika mchezo wa funga dimba la Ligi Bara Kuu Tanzania Bara msimu huu.
Kavumbagu alimaliza msimu wa Ligi Kuu Bara akiwa amefunga mabao 10, idadi ambayo ilimfanya apitwe kwa mabao saba na fowadi wa Azam FC, Kipre Tchetche.
Kwenye Kombe la Kagame, Yanga imepangwa kwa Kundi C pamoja na timu za Express (Uganda), Ports (Djibout), VitalO(Burundi), wakati Simba ipo Kundi A sambamba na timu za El-Merrekh (Sudan), APR (Rwanda), Simba SC (Tanzania), Elman (Somalia).
Kundi  B litakuwa na timu za Al-Hillal (Sudan), Tusker FC (Kenya), Al Nasri (Sudan Kusini), Falcon (Zanzibar),  Al Shandy (Sudan).

No comments:

Post a Comment