Pages

Monday, May 13, 2013

ADEBAYOR AISHUSHA ARSENAL ENGLAND



MANCHESTER, England
ILIKUWA siku ya kihistoria kwenye soka la England wakati Sir Alex Ferguson alipoingia Old Trafford kwa mara yake ya 723 ambayo pia ilikuwa ya mwisho kwake kama kocha wa Manchester United katika mechi dhidi ya Swansea City. 

Katika pambano hilo, beki Rio Ferdinand alihakikisha Ferguson anastaafu kwa ushindi kwenye mechi yake ya mwisho Old Trafford kwa kufunga bao dakika za majeruhi na kuiwezesha Manchester United kushinda 2-1.
Aidha mechi ya jana pia ilikuwa ya mwisho kwenye Uwanja wa Old Trafford kwa kiungo mkongwe wa Manchester United, Paul Scholes, ambaye naye ametangaza kustaafu mwisho wa msimu huu.
Javier Hernandez ‘Chicharito’ aliifungia Man United bao la kuongoza katika kipindi cha kwanza lakini Michu aliisawazishia Swansea kipindi cha pili na kufanya matokeo kuwa 1-1 kabla ya Rio kuipa Man United bao la ushindi dakika za majeruhi.

Scholes alianza kwenye pambano hilo, ambalo mshambuliaji Wayne Rooney hakupangwa kabisa na kuishia kukaa kwenye chumba cha watu mashuhuri.
Ferguson aliingia uwanjani na kufanyiwa gwaride la heshima huku kukiwa na bendera na mabango kadhaa ambayo yalikuwa yakimfagilia kocha huyo mwenye umri wa miaka 71 pamoja na Scholes.
Baada ya pambano hilo Ferguson alishika kipaza sauti na kuongea mashabiki zaidi ya 70,000 waliokuwa kwenye Uwanja wa Old Trafford, kisha ikaanza hafla rasmi ya kukabiziwa kombe.

Man United walipewa rasmi kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2012-13, likiwa kombe la 20 kwa Man United na la 13 kwa Ferguson tangu alipoanza kuinoa timu hiyo mwaka 1986.
Fergie ndiye aliyeongoza wachezaji wa Man United kuchukua medali na kukabidhiwa kombe lao, huku akimkumbatia kila mmoja baada ya kuvalishwa medali yake. Nahodha Nemaja Vidic na Rio walipopewa kombe walimkabidhi Ferguson ambaye aliinyanyua juu.

Katika mchezo mwingine uliochezwa jana, mshambuliaji Emmanuel Adebayor aliendelea kuweka hai matumaini ya Tottenham Hotspur kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kufunga bao la ushindi kwenye pambano dhidi ya Stoke City uliochezwa Uwanja wa Britannia.
Adebayor alifunga bao hilo akimalizia krosi ya chini chini ya Clint Dempsey, zikiwa zimesalia dakika saba kabla ya mchezo kumalizika na kuihakikishia Spurs ushindi wa mabao 2-1.

Stoke ndio walikuwa wa kwanza kupata bao kupitia kwa Steven N’Zonzi kabla ya Dempsey kusawazisha huku mabao yote yakipatikana kipindi cha kwanza, na Adebayor kufunga bao la ushindi mpira ukielekea kumalizika.

Matokeo hayo yameibeba Spurs hadi kwenye nafasi ya nne baada ya kufikisha pointi 69 huku Arsenal wakishushwa hadi nafasi ya tano na pointi 67. Arsenal wana mechi moja mkononi dhidi ya mabingwa wapya wa Kombe la FA, Wigan, kesho Uwanja wa Emirates.

Matokeo mengine jana:-
Everton 2 v West Ham 0
Fulham 1 v Liverpool 3
Norwich 4 v West Brom 0
QPR 1 v Newcastle 2
Sunderland 1 Southampton 1

No comments:

Post a Comment