MANCHESTER, England
ILIKUWA siku ya kihistoria kwenye
soka la England wakati Sir
Alex Ferguson alipoingia Old Trafford kwa mara yake ya 723 ambayo pia ilikuwa
ya mwisho kwake kama kocha wa Manchester United
katika mechi dhidi ya Swansea
City.
Katika pambano hilo, beki Rio
Ferdinand alihakikisha Ferguson
anastaafu kwa ushindi kwenye mechi yake ya mwisho Old Trafford kwa kufunga bao
dakika za majeruhi na kuiwezesha Manchester United kushinda 2-1.
Aidha mechi ya jana pia ilikuwa ya
mwisho kwenye Uwanja wa Old Trafford kwa kiungo mkongwe wa Manchester United,
Paul Scholes, ambaye naye ametangaza kustaafu mwisho wa msimu huu.
Javier Hernandez ‘Chicharito’
aliifungia Man United bao la kuongoza katika kipindi cha kwanza lakini Michu
aliisawazishia Swansea kipindi cha pili na
kufanya matokeo kuwa 1-1 kabla ya Rio kuipa
Man United bao la ushindi dakika za majeruhi.
Scholes alianza kwenye pambano
hilo, ambalo mshambuliaji Wayne Rooney hakupangwa kabisa na kuishia kukaa
kwenye chumba cha watu mashuhuri.
Ferguson aliingia uwanjani na kufanyiwa
gwaride la heshima huku kukiwa na bendera na mabango kadhaa ambayo yalikuwa
yakimfagilia kocha huyo mwenye umri wa miaka 71 pamoja na Scholes.
Baada ya pambano hilo Ferguson alishika kipaza
sauti na kuongea mashabiki zaidi ya 70,000 waliokuwa kwenye Uwanja wa Old
Trafford, kisha ikaanza hafla rasmi ya kukabiziwa kombe.
Man United walipewa rasmi kombe lao
la ubingwa wa Ligi Kuu England msimu wa 2012-13, likiwa kombe la 20 kwa Man United
na la 13 kwa Ferguson tangu alipoanza kuinoa timu hiyo mwaka 1986.
Fergie ndiye aliyeongoza wachezaji
wa Man United kuchukua medali na kukabidhiwa kombe lao, huku akimkumbatia kila
mmoja baada ya kuvalishwa medali yake. Nahodha Nemaja Vidic na Rio walipopewa
kombe walimkabidhi Ferguson
ambaye aliinyanyua juu.
Katika mchezo mwingine uliochezwa
jana, mshambuliaji Emmanuel Adebayor aliendelea kuweka hai matumaini ya
Tottenham Hotspur kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao baada ya kufunga
bao la ushindi kwenye pambano dhidi ya Stoke City uliochezwa Uwanja wa
Britannia.
Adebayor alifunga bao hilo
akimalizia krosi ya chini chini ya Clint Dempsey, zikiwa zimesalia dakika saba
kabla ya mchezo kumalizika na kuihakikishia Spurs ushindi wa mabao 2-1.
Stoke ndio walikuwa wa kwanza
kupata bao kupitia kwa Steven N’Zonzi kabla ya Dempsey kusawazisha huku mabao
yote yakipatikana kipindi cha kwanza, na Adebayor kufunga bao la ushindi mpira
ukielekea kumalizika.
Matokeo hayo yameibeba Spurs hadi
kwenye nafasi ya nne baada ya kufikisha pointi 69 huku Arsenal wakishushwa hadi
nafasi ya tano na pointi 67. Arsenal wana mechi moja mkononi dhidi ya mabingwa
wapya wa Kombe la FA, Wigan, kesho Uwanja wa
Emirates.
Matokeo mengine jana:-
Everton 2 v West Ham 0
Fulham 1 v Liverpool
3
Norwich
4 v West Brom 0
QPR 1 v Newcastle 2
Sunderland 1 Southampton
1
No comments:
Post a Comment